Motisha kwa walimu ilivyozipaisha shule za Ilala

Muktasari:

Ni katika matokeo ya mtihani wa kumaliza darasa la saba mwaka 2017

“Kisutu hatutaki shari! tunafanya bidii kuona ufaulu unapanda! Kisutu hoyee,”

Hiki ni kipande cha wimbo wa wanafunzi wa Shule ya Msingi Kisutu wakisherehekea tuzo waliyopewa na Halmashauri ya Manispaa ya Ilala kwa kuweza kuongeza ufaulu.

Japo mvua kubwa ilinyesha, walimu na wanafunzi wa shule za msingi za manispaa hiyo hawakujali.

Walikuwa wakiimba na kufurahia tuzo walizopewa baada ya kufanya vizuri katika mitihani ya taifa ya darasa la saba, mwaka jana.

Wakati tuzo hizo zinatolewa, utafiti wa ‘Uwezo’ uliofanywa na Taasisi isiyo ya kiserikali ya Twaweza mwaka juzi, unaonyesha kati ya wanafunzi 10 wanaomaliza darasa la saba, watatu hawawezi kufanya hesabu za darasa la pili wakati nusu ya wanaomaliza elimu hiyo sawa na asilimia 49.1 hawawezi kusoma hadithi kwa Kiingereza.

Baada ya utafiti huo, Twaweza walikuja na utafiti mwingine uliobainisha kuwa motisha kwa walimu ni nyenzo muhimu katika kuongeza ufaulu shuleni na kuondoa mbumbumbu.

“Nimefurahi shule yangu kupata tuzo, huu ni mwanzo tu wa kufaulisha mwakani tutafundisha kwa bidi zaidi ili tufaulishe zaidi ya hapa,”anasema Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Lusasaro, Iren Mhamba.

Mwalimu Mhamba anakiri kuwa kinachoweza kusaidia ufaulu ni motisha kwa walimu.

Motisha ndiyo iliyomsukuma Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema na jopo lake kuamua kuwatunuku walimu na shule za manispaa hiyo.

Ukweli ni kwamba kujua kusoma, kuhesabu na kuandika hutegemea mwalimu na hakuna mwanafunzi aliyewahi kuvuka hatua hiyo bila jitihada za mwalimu.

Mjema anasema moja ya mambo yanayomwongezea mwalimu ari ya kutekeleza majukumu yake kiufanisi, ni kumpatia motisha na kutambua matokeo ya kazi aliyoifanya jambo ambao wao wamelifanya.

“Hivyo katika kuitambua kazi yenu kubwa walimu wangu, tunawapatia tuzo ikiwa ni sehemu ya pongezi kutokana na matokeo mazuri ya darasa la saba mwaka jana,” anasema.

Mjema anasema pia wanataka kuwajengea walimu hao ari mpya katika ufundishaji na utoaji elimu kwa ufanisi katika manispaa hiyo.

Hiyo ni mara ya kwanza kwa manispaa hiyo kutoa tuzo kwa walimu na shule zilizofanya vizuri, bila kujali za watu binafsi au za Serikali.

Shule zilizopata tuzo

Ofisa Elimu Msingi wa Manispaa ya Ilala, Elizabeth Thomas anasema miongoni mwa vigezo vilivyotumika kutoa tuzo kwa shule hizo ni nafasi zilizoshika.

“Kwa hiyo tunazo shule 10 bora kwa Serikali na binafsi lakini zipo zile zilizoongeza ufaulu,” anasema.

Shule 10 bora za Serikali za Manispaa hiyo zilizopenya ni Mtendeni, Zanaki, Kiwalani, Msimbazi Mseto, Diamond, Lumumba, Msimbazi, Mkoani na Maktaba.

Shule binafsi ni Lusasaro, Fountain Gate, Tusiime, St Joseph Millenium, Genius King, Montivale, Heritage na Green Hill.

Ufaulu katika manispaa

“Mwaka jana tulisemana na tukapeana mikakati ambao leo imefanya tung’ae kwa kuingia kwenye 10 bora kitaifa na nafasi ya pili kimkoa. Hii haitoshi, natamani kuona mwakani tunafanyua vizuri zaidi,” anasema Mjema.

Katika matokeo hayo, Manispaa ya Ilala ilishika nafasi ya pili kimkoa na nafasi ya nne kitaifa.

Elizabeth anasema kati ya wanafunzi 21,569 waliofanya mtihani huo, wanafunzi 19,236 walifaulu.

“Ufaulu wetu ni asilimia 89 hivyo ni matumaini yetu mwakani ufaulu utakuwa juu zaidi,” anasema.

Mjema anasema hatapenda kuona tena manispaa hiyo inapata matokeo mabaya.

Walimu wazungumza

Baadhi ya walimu wa shule zilizopata tuzo, wanasema jitihada, kujituma na motisha kwa walimu ndiyo siri kubwa ya mafanikio kwa shule hizo.

Mwalimu Mhamba anasema kinachoifanya shule yake ifaulishe ni utaratibu waliojiwekea wa kuwapa motisha walimu.

“Mwalimu akiwezesha darasa la mtihani kupata A, anapewa Sh50,000 hadi 100,000. Hii inawafanya wajitoe katika kufundisha,’ anasema na kuongeza:

“Walimu wanaanza kufundisha asubuhi na wanatoka madarasani jioni kabisa; hii yote inasaidia kuongeza ufaulu.”

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi, Fountain Gate Academy, Julius Lugemalira anasema licha ya motisha kwa walimu wao, mazingira bora ya kujifunza na kufundishia yanachangia ufaulu kwa wanafunzi.

“Kwa hiyo hii motisha ya tuzo inatufanya tuongeze bidii na tujitume zaidi ili mwakani tupewe tena tuzo,” alisema.

Mkakati

Elizabeth anasema ipo mikakati mingi waliyojiwekeza kuongeza ufaulu.

Anaitaja mikakati hiyo kuwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa walimu wanawafundisha wanafunzi katika muda wa ziada.

Naye Mjema anasema mkakati mwingine ni kuwasaidia wanafunzi wazito kuelewa darasani, kwa kuwapa muda wa ziada tofauti na wenzao.

Wadau wazungumza

Mdau wa elimu kutoka taasisi ya Nielimishe, Daud Shaki anasema ualimu unahitaji mbinu mbadala katika kuhakikisha hakuna mtoto anayevuka hatua moja bila kuelewa kile alichofundishwa.

“Ili awasaidie watoto vizuri zaidi anapaswa kupewa motisha itakayoonyesha kumbe kazi yake ni muhimu na inatambuliwa. Bidii inatokana na motisha sio tu kwa walimu ni mahali popote pa kazi,” anasema.

Anashauri wilaya nyingine kuwa na mikakati ya aina hiyo ya kuwatunuku walimu na shule zinazofanya vizuri, ili kusaidia katika kuongeza ufaulu.