Msikie Samatta-Mambo yanaanza kunyooka

Muktasari:

  • Kwanza habari mbaya kwa Samatta ni kwamba amefanyiwa upasuaji baada ya kuumia goti. Alifanyiwa upasuaji wiki iliyopita na atalazimika kukaa nje ya uwanja kwa wiki nane.

Achana na kuumia, achana na kupasuliwa goti na kukaa nje ya dimba kwa wiki nane, mshambuliaji na nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta anaamini mambo yanafunguka.

Kwanza habari mbaya kwa Samatta ni kwamba amefanyiwa upasuaji baada ya kuumia goti. Alifanyiwa upasuaji wiki iliyopita na atalazimika kukaa nje ya uwanja kwa wiki nane.

Samatta aliyewashukuru madaktari kwa tiba, alilazimika kutoka katika mchezo kati ya KRC Genk dhidi ya Lokoren. Mechi hiyo ya Ligi Kuu ya Ubelgiji.

Mshambuliaji huyo alipumzishwa katika dakika ya 40 na nafasi yake kuchukuliwa na Nikolaos Karelis.

Kutokana na hali hiyo, Samatta amekosa mechi ya jana ya Taifa Stars na Benin na akipata nafuu vizuri, ataanza kuonekana uwanjani mwakani ikiwemo mchezo wa Machi 23 dhidi ya Uganda wa kutafuta nafasi ya kufuzu Fainali za Afrika (Afcon).

Anachokisema

Samatta, anasema ndoto ya kutambulika katika medani ya soka duniani inatarajia kutimia muda mfupi ujao.

Anasema hatua ya jina lake kuwemo katika orodha ya nyota 30 wanaowania tuzo ya mchezaji bora wa Afrika mafanikio makubwa.

“Nina matumaini ya kufanya vizuri, huu ni mwanga ninaouona. Nimefurahi kwa kuwa kile ninachokifanya hapa Ubelgiji kinaonekana, ninaamini pamoja na kuteuliwa kuwania tuzo, ni kama mambo yamefunguka na ni njia ya kufika mbali zaidi ya hapa nilipo.”