Msukumo zaidi unahitajika kuimarisha elimu ya awali

Wanafunzi wa shule ya awali wakiwa darasani. Picha ya Maktaba

Muktasari:

  • Elimu ndiyo nyenzo inayompatia mwanadamu maarifa ya kumwezesha kufanya kazi kwa kutumia rasilimali zinazomzunguka.
  • Kimsingi maendeleo makubwa tunayoyashuhudia kwa sasa duniani, yametokana na maandalizi mazuri ya vizazi vilivyopita na vilivyopo katika katika suala zima la kukuza ujuzi na maarifa.

Maendeleo yoyote ya binadamu duniani yana chanzo chake na chimbuko kubwa la maendeleo hayo ni ni elimu.

Elimu ndiyo nyenzo inayompatia mwanadamu maarifa ya kumwezesha kufanya kazi kwa kutumia rasilimali zinazomzunguka.

Kimsingi maendeleo makubwa tunayoyashuhudia kwa sasa duniani, yametokana na maandalizi mazuri ya vizazi vilivyopita na vilivyopo katika katika suala zima la kukuza ujuzi na maarifa.

Maandalizi haya huanzia utotoni kwa maana ya kuwa na elimu ya awali. Kuna misemo miwili ya Kiswahili isemayo: “Nyota njema huonekana asubuhi” na “Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo” .

Misemo hii inamaanisha kuwa kadri mtoto anavyoandaliwa vizuri au vibaya katika maisha ya sasa, ndivyo anayoandaliwa kukabili maisha yake ya baadaye.

Mwaka jana asasi isiyo ya kiserikali ya Twaweza kupitia programu yake ya Uwezo, iliripoti kuwapo kwa wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi wakiwa hawajui kusoma na kuhesabu.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, baadhi ya wanafunzi wa darasa la saba hawawezi kufanya majaribio ya darasa la pili.

Aidha, wanafunzi wanne kati ya 10 (sawa na asilimia 44) hawawezi kusoma hadithi ya Kingereza ya kiwango cha darasa la pili, wawili kati ya 10 (sawa na asilimia 16) hawawezi kusoma hadithi ya Kiswahili ya kiwango cha darasa la pili na wawili kati ya 10 (sawa na asilimia 23) hawakuweza kufanya hesabu za kuzidisha za kiwango cha darasa la pili.

Suala kubwa linalojitokeza hapa ni kuwa watoto wetu hawapati maandalizi ya kutosha katika madarasa ya awali ambayo ndiyo yanayoanza kumwandaa mtoto kielimu.

Hali hii ikiachwa itaendelea kuathiri sana utoaji wa elimu ya msingi, na hatimaye kupata vijana wengi wasiokuwa na ujuzi na maarifa ya kukabiliana na maisha yao ya sasa na ya baadaye.

Hivyo, kama kweli tunataka kupata vijana walioiva kielimu na kimaadili, hatuna budi kuanza maandalizi ya watoto wetu mapema.

Ili kulitekeleza hilo kwa vitendo, hatuna budi kutilia maanani suala la elimu ya awali, kwani ndiyo ambayo humpatia mtoto stadi za awali kabla ya kujiunga na shule ya msingi.

Elimu ya awali

Kwa mujibu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, elimu ya awali ni mfumo wa elimu ulio rasmi kwa ajili ya watoto wenye umri kati ya miaka mitano hadi sita.

Elimu hii inachukua miaka miwili na hakuna mitihani ya kutoka ngazi moja kwenda nyingine katika mfumo huu. Ni elimu inayotolewa kwa mtoto ili kumjengea msingi mzuri wa kuanza elimu ya msingi.

Elimu hii ndiyo ya kwanza katika mfumo rasmi unaotambuliwa na Sera ya Elimu na Mafunzo.

Lengo la elimu ya awali ni kuhimiza na kukuza maendeleo ya mtoto, yanayojumuisha ukuaji wa haiba na uwezo wa mtoto kimwili, kiakili, kimaadili na kiroho.

Mtoto akishapata maendeleo hayo humsaidia katika hatua inayofuata, ambayo ni shule ya msingi na kimsingi anapaswa kufundishwa kusoma, kuandika na kuhesabu.

Serikali kwa kushirikiana na wadau wa elimu imefanikiwa kuanzisha madarasa ya awali, hivyo kutoa fursa nyingi kwa watoto wa Kitanzania.

Hata hivyo, pamoja na jitihada na mafanikio hayo, bado utoaji wa elimu ya awali nchini unakabiliwa na changamoto nyingi kama vile uhaba wa walimu wenye sifa stahiki, vyumba vya madarasa na vifaa vya kufundishia na kujifunzia.

Mwalimu ni kiungo muhimu katika kumjenga mtoto kifikra, kitabia, kinidhamu na kitaaluma. Mwalimu anayeweza kumjenga mtoto katika hayo yote ni mwalimu mwenye taaluma ya rika husika la wanafunzi.

Bado kuna tatizo kubwa la walimu wenye taaluma kufundisha madarasa ya awali. Kwa sababu ya uhaba wa walimu, baadhi ya shule za awali zinatumia vijana waliomaliza elimu ya sekondari ambao hawajapata utaalamu wa kufundisha watoto katika ngazi hii ya elimu.

Walimu hawa hawana ujuzi wa kutosha katika saikolojia, falsafa, mbinu za kufundisha na mambo mengine mengi kuhusu malezi na makuzi ya mtoto, hivyo kujikuta wakifundisha mambo yasiyoendana na umri na uwezo wa mtoto.

Katika baadhi ya shule hasa zile binafsi, vitabu na zana nyingine za kufundishia na kujifunzia, hazirandani na utamaduni wetu.

Kwa mfano, vitabu vinavyozungumzia michezo kama ya kuteleza kwenye barafu, havifai kumfundishia mtoto wa jamii kama za wafugaji au wavuvi, kwa kuwa havitawasaidia katika mazingira yao.

Ni vyema walimu na wadau wengine wa elimu wakaanza sasa kuandaa vitabu na zana za kufundishia zilizopo katika mazingira yetu wenyewe.

Mafunzo yanayotolewa kwa walimu ni vizuri yakatilia maanani uhamasishaji katika utayarishaji wa zana na uandishi wa vitabu kwa ajili ya watoto wetu katika shule za awali.

Kwa kuwa sera mpya ya elimu na mafunzo inasisitiza ulazima wa elimu hii, ni muhimu kwa Serikali na wadau wengine wa maendeleo kuwekeza vilivyo katika daraja hili muhimu la elimu. Ikumbukwe kuwa elimu ya awali, ndiyo msingi wa madaraja yote ya elimu.