Mwalimu Bibi na hadithi ya watoto walivyomrejesha darasani

Muktasari:

  • Wito alionao kwenye kazi hiyo ya ualimu wa watoto ilimchochea aamue kujiunga na kusoma stashahada ya saikolojia alipohitimu mwaka 2012 katika Chuo cha Msimbazi jijini Dar es Salaam.

‘Mwalimu Bibi’ ndivyo anavyotambulika kwa watoto wengi waishio jirani na nyumbani kwake, ambapo amejenga madarasa mawili kwa ajili ya kutoa elimu ya awali.

Wito alionao kwenye kazi hiyo ya ualimu wa watoto ilimchochea aamue kujiunga na kusoma stashahada ya saikolojia alipohitimu mwaka 2012 katika Chuo cha Msimbazi jijini Dar es Salaam.

Eddah Kapange umri wake ni miaka 58, ni msomi mwenye shahada ya sayansi aliyoipata kwenye Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM) mwaka 1985, lakini ameamua kujiajiri kwa kufundisha watoto.

“Sikuangalia nitachekwa kwa umri nilionao kuvaa sare na kwenda chuo kutimiza maono yangu, huko nilisoma darasa moja na wanafunzi wenzangu ambao umri wao ni sawa na wanangu, sikujisikia vibaya nilijitahidi kuwa makini na masomo yangu hatimaye nikahitimu kwa kufaulu vizuri,” anasema.

Anasema baada ya kuhitimu kwa kuwa wana eneo kubwa na mume wake aitwaye Michael Mwaipyana walijenga madarasa mawili kisha wakaanza kufundisha watoto huku wakiendelea na taratibu za usajili.

Agosti mwaka huu wakaguzi kutoka ofisi ya afisa elimu wa wilaya walifika kituoni hicho kiitwacho Planet Earth Day Care.

Katika mazungumzo yake na Mdhibiti ubora wa shule wa Manispaa ya Ilala, Fredric Mtaita alieleza kuwa alikatishwa tamaa ya kusajili kituo chake baada ya kuombwa rushwa.

“ Kituo hiki nimekianzisha tangu mwaka 2012 kuna siku walikuja madiwani hapa kunitembelea hapa, wakaridhika na hali waliyoikuta ikiwamo ukubwa wa eneo langu, hivyo wakanishauri niende kwenye ofisi husika ili nisajili,” anasema.

Anaeleza alianza kuufanyia kazi ushauri huo mzuri , lakini alishtuka siku moja kiongozi mmoja wa kata akiwa ameongozana na mtu mwingine walifika na kumtaka awape rushwa ya Sh2.5 milioni ili apate huo usajili.

Kapange anasema pia baada ya kufuatilia ameona utaratibu na masharti ya usajili ikiwamo la kutakiwa kuwa na akiba ya Sh68 milioni kwenye akaunti yake, jambo ambalo kwake analiona ni gumu kulitimiza.

“Sharti hili ni gumu binafsi naliona kama linaweza kushawishi mtu kufanya udanganyifu wa kuweka fedha zionekane zipo kwa muda baadaye hali ya akaunti inakuwa ya kiwango kidogo,” anasema.

Anaiomba Serikali kuangalia upya umuhimu wa vigezo vya usajili ili kusaidia kuwepo kwa uadilifu kwenye hatua hiyo.

Kapange anaeleza kuwa yeye ni mtoto wa kwanza kwenye familia ya watoto 20, baba yake alikuwa ameoa wake wengi, ambapo waliishi wilayani Chunya mkoani Mbeya.

“Kulikuwa na changamoto kubwa katika malezi yetu kadri tulivyokuwa kwani mahitaji muhimu kwetu yalimlemea baba, ingawa pamoja na mazingira hayo nashukuru nilifaulu mtihani wa darasa la saba na kuchaguliwa kujiunga Mbeya Day,” anasema.

Anaeleza kuwa kutoka Chunya hadi Mbeya mjini ilipo shule hiyo ilikuwa ni mbali, hivyo wazazi walimtafutia chumba mjini , na kumkadbidhi mdogo wake mwenye miaka minne aishi naye.

“ Yule mtoto nilikuwa namuacha kwa majirani asubuhi ile hali haikunifurahisha, maisha yalikuwa ni magumu kuna wakati nilikosa hata mafuta ya taa hivyo nilishindwa kujisomea, nilitamani nipate shule ya bweni,” anasema.

Anasema siku moja Mkuu msaidizi wa shule aliwatembelea darasani kwao na kuzungumza nao kwa muda kisha kuwapa nafasi wenye matatizo wamfuate ofisini kwake, ndipo akatumia fursa hiyo kueleza changamoto anazokumbana nazo.

Kapange anabainisha kuwa baada ya kujieleza mwalimu alimsaidia akapata nafasi na kuhamishiwa kwenye shule ya Sekondari ya Loleza (bweni).

“Nilifurahi kutimiza ndoto yangu nikamjulisha mama amchukue mdogo wangu na kuondoka naye Chunya, nijitahidi kusoma kwa bidii hadi nilipomaliza kidato cha nne, matokeo yalipotoka nilichaguliwa kuendelea kidato cha tano Sekondari ya Rugambwa mkoani Kagera,” anasema.

Anasema ilikuwa ni mwaka 1978 alipokwenda kuanza masomo yake ya kidato cha tano mwaka ambao Idd Amin aliyekuwa Rais wa Uganda alianzisha chokochoko na Tanzania, vita ikaanza hivyo kuna mahandaki walichimbiwa ili kujificha.

“Vita ile ilitutesa wanafunzi wengi nakumbuka kuna siku wengine walikimbilia kwenye handaki kujificha mimi na wenzangu wachache tuliona kama kuna utulivu tukawa tunaendelea kuandika ghafla tukashtushwa na sauti kubwa ya mlipuko,” anasema.

Anasema alianguka na kupoteza fahamu kisha akazinduka na kujikuta yupo na wenzake kwenye handaki wanatetemeka kwa hofu, njaa na baridi kwa sababu mvua ilikuwa inanyesha hivyo walikaa kwenye maji.

“ Hali ile siwezi kuisahau maishani, baadaye tulijulishwa kuwa mlipuko ule ilikuwa ni ndege ya nduli imetunguliwa na JWTZ, kisha taratibu za kutuhamisha kwenda Mwanza zikafanywa tukabebwa kwenye malori ya jeshi,” anasema.

Anasema baada ya hali ya amani kurejea walirudishwa shule na kuendelea na masomo, wali nilitamani kuwa daktari lakini nilikataliwa kwa sababu katika mchepuo niliosoma sikusoma physic, hivyo nikaenda UDSM kusoma Sayansi kwa ujumla.

Anasema aliamua kujikita kwenye elimu ya mimea, baada ya kumaliza chuo alipangiwa kwenda kufanya kazi Wizara ya maji.

“Nilianza kazi 1985 mara baada ya kumaliza chuo, mshahara ulikuwa ni shilingi 1980 ukienda kupokea lazima uende na shilingi 2000, wakati huo kiwango hicho kilikuwa kikubwa na tuliweza hata kuweka akiba, “ anasema.

Anasema akiwa katika wizara hiyo kitengo cha maabara ambapo baada ya miezi kadhaa alitakiwa kwenda kufanya kazi Sumbawanga mkoani Rukwa, wakati huo ulikuwa ukitajwa kukithiri kwa vitendo vya ushirikina, hivyo baba yake alimkataza kwenda kuripoti.

Kapange anabainisha kuwa baada ya hatua hiyo aliamua kuomba kufundisha katika Sekondari ya Shabani Robert, ambapo alifundisha kwa miaka miwili kabla ya kuona tangazo la nafasi ya kazi ya mkemia kiwanda cha kutengeneza karatasi cha Kibo Papers.

Anabainisha kuwa alifanikiwa kupata kazi hiyo, mwaka 1992 alipata nafasi ya kwenda nchini Norway kwenye kozi ya mwaka mmoja ya stashahada ya utengenezaji karatasi.

“Baada ya kumaliza kozi hiyo mwaka 1993 nilikwenda nchini Sweden kwa ajili ya kozi ya shahada ya uzamili ya utengenezaji wa karatasi unaozingatia utunzaji wa mazingira.

“Niliporejea nchini na kuendelea na kazi mwaka 1994 hatua ya ubinafishaji iliyofanywa na Serikali kwa mashirika ya umma ilikikumba Kibo Paper, ambapo mwaka 1998 tuliachishwa kazi wote na tulilipwa mafao kiduchu.

Anasema amejishughulisha na ujasiriamali wa aina mbalimbali ikiwamo ufugaji wa samaki, kabla ya kuamua kwenda kusomea saikolojia na ufundishaji wa watoto.