JICHO LA MWALIMU : Mwanafunzi kukosea ni hatua katika kujifunza

Muktasari:

Zaidi waliamini mawazo na mitazamo ya watu kuwa sahihi kuliko yao; hivyo kuchangia kuishi maisha ya kuigiza.

Watu wengi walioogopa kukosea mara nyingi, hawakuweza kujifunza kitu kipya na wala hawakuweza kuwa na ujasiri wa kutekeleza jambo la ubunifu.

Zaidi waliamini mawazo na mitazamo ya watu kuwa sahihi kuliko yao; hivyo kuchangia kuishi maisha ya kuigiza.

Katika maisha ya kawaida watu kutoka makundi mbalimbali hufanya makosa. Kwa mfano, uwepo wa amri kumi za Mungu na sheria ya makossa na adhabu pia ni ushahidi wa kuwa binadamu hukosea.

Mabingwa wa nadharia mbalimbali zinazotumika ulimwenguni walizifanyia majaribio na wakati mwingine zilikuja kuboreshwa sehemu zenye upungufu na waliofuata baada yao.

Wanasayansi maabara hufanya majaribio mengi na kukosea sana ili kuweza kupata majibu ya tafiti zao.

Katika muktadha wa darasani, mwalimu hana budi kuwahamasisha wanafunzi kuwa na morali wa kujifunza kwa vitendo, ili kuweza kukosea na kujifunza na wakati mwingine kuja na njia nyingine tofauti.

Kukosea ni sehemu mojawapo muhimu katika hatua za kujifunza na hili lina faida kama ifuatavyo:

Moja, humjengea moyo wa kujiamini katika kujaribu mawazo mapya. Mwanafunzi ataweza kupenda kuchangia katika majadiliano na wanafunzi wengine, hivyo kumwezesha kutambua uwezo wake hasa pale inapotokea mwalimu amewapa kazi ya darasani au nyumbani

Mbili, humfundisha thamani ya maisha yake hivyo kumfanya mwanafunzi kujifunza katika maisha yake yote kwa furaha kwa kuwa hana hofu ya kukosea. Hii pia hujengea maarifa na ufahamu wa kutambua kuwa mtu anapokosea, msamaha unaweza kutolewa.

Hivyo, makosa humfundisha mwanafunzi au mtu yeyote jinsi ya kusamehe kwa sababu hakuna binadamu asiyeweza kuishi maisha yake yote asifanye kosa. Hata ukweli wa nadharia za leo, baada ya miaka mingi ijayo zinaweza zisiwe kweli.

Tatu, humfundisha mwanafunzi na mtu yeyote kuishi maisha yasiyojaa kujilaumu na husababisha aishi maisha ya kujifunza yenye furaha.

Nne, makosa humwezesha mwanafunzi kufahamu mambo ya msingi katika masomo yake. Inawezekana kosa alilofanya limetokea kutokana na kufanya au kuzingatia jambo ambalo siyo la msingi. Hivyo, kwa njia ya kosa hilo mwanafunzi ataweza kubaini mambo ya msingi na yasiyo ya msingi katika mchakato wa kuwepo kwake shuleni.

Tano, makosa humfanya mwanafunzi kuondoa woga wa kuogopa kukosea. Mazingira hayo ya mwanafunzi kujifunza darasani kwa kuogopa kukosea husababisha wengine kutoeleza hisia na mawazo yao. Wakati mwingine husababisha wanafunzi wenye uoga wa namna hii, kushindwa hata kujibu maswali ya darasani hata pale wanapokuwa wanafahamu jibu.

Sita, makosa huchukua nafasi ya kitahadharishi kwa mwanafunzi. Kwa mfano, makosa anayokosa katika somo husika huweza kumpa picha ya uwezo wake wa uelewa wa hilo somo na kuchukua hatua sahihi za kuondoa tatizo hilo.

Pia, inawezekana kutokea kwa kosa fulani leo, kunaweza kumtahadharisha dhidi ya hatari au kosa lingine kubwa la siku za mbele.

Saba, humkumbusha mwanafunzi kuwa katika muktadha wa shule naye kama mwanafunzi, hufanana na wengine. Kwa mfano, katika maisha mara nyingi watu wanapofanikiwa hutokea wakajisahau kuwa wako sawa na wengine.

Lakini pale wanapokosea ndipo wanapobaini kwamba wanapaswa kuthamini wengine pia kwani nao wana udhaifu kama wao.

Nane, humwezesha kubaini nafasi ya chaguzi nyingine. Kwa mfano, inawezekana kuna uchaguzi fulani ambao mwanafunzi aliupuuzia au hakufahamu umuhimu na ubora wake.

Baada ya kukosea katika uchaguzi huo, hubaini kwamba uchaguzi au ushauri aliokuwa akipewa hapo awali na akaupuuzia ulikuwa na nafasi kubwa katika mafanikio yake ya kimasomo na maisha.

Tisa, makosa humwonyesha mwanafunzi udhaifu wa kimfumo na kumpa fursa ya kuendana na mfumo uliopo.

Pia, kwa watu wa kawaida makosa huwawezesha kubaini ni wapi kuna udhaifu katika maisha yao au jambo wanalolifanya. Kwa njia hii wanaweza kurekebisha udhaifu huo ili wawe na tija zaidi.

Lakini pia kuna madhara ya mwanafunzi kuamini kwamba hapaswi kukosea. Haya ni kama yafuatayo

Moja, humfanya kubaini jambo lisilofaa na linalofaa ama kitu kinachofaa na kisichofaa. Anapotumia kitu au njia fulani na ikamsababishia mfano kwenye somo la Hisabati au jingine lolote, ni wazi kuwa atakuwa amebaini kuwa kitu au njia hiyo haifai au siyo sahihi.

Mbili, humfanya ashindwe kutambua thamani ya msamaha. Endapo mwanafunzi atakuwa amemkosea mwenzake na ni wa thamani kwake, ni wazi kuwa atahitaji kumwomba msamaha ili kuendeleza uhusiano wake naye. Hivyo, kwa njia ya makosa anakuwa ametambua umuhimu wa msamaha.

Tatu, kuogopa kukosea humfanya mwanafunzi kushindwa kuwa mbunifu. Kwa mfano, makosa mengi yanayotokea katika muktadha wa kujifunza humfanya mwanafunzi awe mbunifu zaidi ili aweze kuyakabili makosa ya namna hiyo ama mengine.

Nne, humsababisha mwanafunzi kushindwa kutazama malengo yake upya. Kuna umuhimu mkubwa sana wa mwanafunzi kujiwekea malengo vyema katika masomo yake na maishani. Lakini anapokwama, moja kwa moja hujifunza jinsi ya kuyabadili au kuyaboresha.

Hivyo basi, maisha ya kukosea siyo tu yanamuimarisha mtu bali humpa ujasiri kuliko yule asiyejaribu kufanya jambo lolote.

Ni jukumu la jamii kutambua kwamba wanafunzi hujifunza vizuri pale wanapokosea. Mwanafunzi au mtu ambaye hujiaminisha kuwa hawezi kukosea, siku anapokosea

ama kushindwa jambo, anaweza kupatwa msongo wa mawazo mkubwa kwa maisha yake. Kufanya makosa katika mchakato wa kujifunza ni sehemu ya ujifunzaji.