Ni vema tukawa na uelewa mmoja tunapoelekea kwenye uchumi viwanda

Muktasari:

  • Ili kufikia lengo la kuwa na uchumi imara na shindani, imekusudia ifikapo 2025 uchumi wa nchi utokane na viwanda.

Serikali imedhamiria kutekeleza kwa vitendo Dira ya Taifa ya 2025 ambayo pamoja na mambo mengine, inaelekeza kuwa na uchumi imara na shindani.

Ili kufikia lengo la kuwa na uchumi imara na shindani, imekusudia ifikapo 2025 uchumi wa nchi utokane na viwanda.

Pamoja na azma hiyo nzuri ni vema Serikali kupitia vyombo vyake itoe elimu pana ya maana ya viwanda na mnyumbuliko wake.

Sera ya Viwanda ya mwaka 2003 imevigawa katika makundi manne kwa kuzingatia idadi ya watu na kiasi cha mtaji.

Makundi hayo ni pamoja na la viwanda vidogo kabisa (micro) ambavyo vinajumuisha idadi ya watu kati ya 1-4 na mtaji usiozidi Sh5 milioni.

Pili ni viwanda vidogo (small) vinavyohusisha idadi ya watu kati ya 5 hadi 49 na mtaji wa kati ya Sh5 hadi 200 milioni.

Tatu ni viwanda vya kati (medium), vinavyojumuisha idadi ya watu kati ya 50 na 99 na kiwango cha mtaji wa kati ya Sh200 hadi 800 milioni.

Kundi la nne ni lile la viwanda vikubwa, hivi vinajumuisha idadi ya watu zaidi ya 100 na mtaji unaozidi Sh800 milioni.

Pamoja na madaraja haya ya viwanda, bado kuna ukinzani mkubwa wa uelewa kwa mfano, kiwanda chenye idadi ya watu kati ya mmoja hadi wanne na mtaji wa Sh10 milioni kitaingia kundi gani?

Utekelezaji wa viwanda unaweza kufikiwa kirahisi kama watumishi wa sekta ya umma, binafsi na jamii itaweza kufahamu kiundani nini maana ya kiwanda na sifa zake.

Kauli mbiu ya “Uchumi wa viwanda” isiishie kwa kutamkwa na viongozi tu, bali kila raia kwa makundi yao waelewe maana na mikakati ya utekelezaji ili kurahisisha kufikia lengo kabla au ifikapo 2025.

Sera ya viwanda ya mwaka 2003 ifanyiwe maboresho ili kuondoa mkanganyiko uliopo sasa wa aina na makundi ya viwanda.

Kila kiongozi kuanzia ngazi ya ofisa mtendaji wa kijiji hadi viongozi wakuu serikalini wawe na uwezo wa kuelezea dhana nzima ya viwanda kwa upana wake.

Kufahamu maana ya kiwanda na sifa zake za msingi ni nusu ya kufaulu safari ya kuelekea uchumi wa viwanda.

Itachukua muda zaidi ya uliopangwa kama tafsiri ya kiwanda itabaki kwenye vichwa vya viongozi wachache wa Serikali.

Ni muhimu Serikali iweke mikakati shirikishi ili kufikia lengo la uchumi wa viwanda ambao kwao utawakwamua wananchi hasa wanyonge na masikini katika dimbwi zito la umaskini, ujinga na maradhi.

Ni muhimu pia kwa Serikali kuweke wazi aina ya viwanda, uendeshaji na umiliki ambao inaona utatuvusha kwa wepesi kuelekea uchumi wa viwanda.

Je, tunahitaji viwanda vinavyoendeshwa na kumilikiwa na Serikali? Au Serikali inataka kuwezesha sekta binafsi ikiwamo makundi maalum kuendesha na kumiliki viwanda?

Na je, tunataka kuwekeza nguvu kwenye uanzishwaji wa viwanda vidogo sana, vidogo, kati au vikubwa?

Kama Taifa bila kuelewa Serikali inataka kuona nchi yenye viwanda vya aina gani, umiliki na uendeshaji wa mfumo gani haitakuwa rahisi kufikia lengo.

Ni jukumu la Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji pamoja na Wizara ya Ofisi ya Rais Tamisemi, kutoa mafunzo maalumu kwa viongozi wa taasisi zote za Serikali zikiwamo Mamlaka za Serikali za Mitaa juu ya dhana ya viwanda.

Viongozi watakaopatiwa mafunzo wawe chanzo cha maarifa kwa viongozi na wananchi waliopo katika maeneo yao.

Kupitia uelewa wa pamoja, kazi ya Rais John Magufuli itakuwa ndogo kuelekea uchumi wa viwanda.

Kila litakalotamkwa na Serikali kuhusu viwanda, kila mwananchi atakuwa na uelewa juu ya utekelezaji wake.

Ushauri kwa Serikali, ili kufikia ndoto nzuri ya kuwa na uchumi wa viwanda ifikapo 2025 ni vema tukajikita kwenye uanzishwaji wa viwanda vidogo sana na vidogo.

Hii inatokana na tafiti nyingi zilizofanyika juu ya aina ya viwanda hivyo.

Viwanda vidogo sana na vidogo ni aina ya viwanda ambavyo vimeonyesha kuajiri idadi kubwa ya watu hasa wenye elimu ya kawaida, mitaji kiasi na teknolojia ya chini.

Nchi nyingi duniani hasa za Asia, zimeendelea kiviwanda kwa kuwawekea miundombinu wezeshi wananchi wake kujiajiri kwenye viwanda vidogo sana na vidogo.

Mwandishi ni Mtakwimu na Ofisa Mipango.