UCHAMBUZI: Nyerere aliposhtakiwa na wakoloni mwaka 1958

Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere

Muktasari:

Miongoni mwa wapambanaji wakuu wakati huo alikuwa ni Mwalimu Julius Nyerere ambaye aliamua kuacha kazi ya ualimu na kujikita kwenye siasa akiwa kiongozi wa Chama cha Tanu alijikuta matatani.

Watu wengi hawajui kuwa uhuru wa Tanganyika na baadaye Tanzania Desemba 9, 1961 ulipatikana kwa mapambano makali hata kama damu haikumwagika.

Miongoni mwa wapambanaji wakuu wakati huo alikuwa ni Mwalimu Julius Nyerere ambaye aliamua kuacha kazi ya ualimu na kujikita kwenye siasa akiwa kiongozi wa Chama cha Tanu alijikuta matatani.

Mwalimu Nyerere alistaafu ualimu Machi 23, 1955 akiwa anafundisha Shule ya Sekondari ya Pugu nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam ili ajikite zaidi kwenye siasa.

Wakati huo, Tanganyika kama nchi nyingine za Afrika ilikuwa na Serikali halali ya kikoloni iliyokuwa ikiongozwa na Gavana Richard Turnbull.

Kesi ya Nyerere

Mwandishi wa kitabu cha Kesi ya Julius Kambarage Nyerere 1958, Simon Ngh’waya anaeleza sababu ya Mwalimu Nyerere kushtakiwa kuwa ni kutokana na maandishi yake kwenye gazeti la ‘Sauti ya Tanu’ la Mei 7, 1958, baada ya kusema wakuu wa wilaya wanakihujumu Chama cha Tanu kwa kuyafunga baadhi ya matawi yake na pia kuwachukulia hatua kali machifu waliokuwa wanaunga mkono.

Katika makala hayo, Mwalimu Nyerere aliwaita wakuu hao wa wilaya kuwa ni ‘washenzi na maharamia’. Katika ukurasa wa saba wa kitabu hicho, Mwalimu Nyerere anaandika:

“Naiomba Serikali ya kibeberu, itamke wazi kwamba inaishambulia Tanu kwa sababu tumetangaza bila woga kuwa Serikali ya kimabavu tutaipiga vita. Tutaishambulia bila kupumua mpaka tumeiangusha …ndugu wananchi, jihadharini, adui anashindwa, anaanguka kwa sababu hana njia za kupinga kilio chetu. Njia yake ni moja tu nayo ni kutaka ghasia ili akatumie bunduki. Tusimpe nafasi …adui atateketea bila shaka.

“Nilipofikiria utu wa binadamu, ninapotambua kwa kuwa sijajaliwa kuwa mtu anayestahili sheria na furaha ya tabia, nachukia kutawala binadamu kwa nguvu na udanganyifu kama vile maharamia na wajinga. Naona uchungu kwa wale wanaokandamizwa.”

Kitabu hicho kinafafanua kuwa maneno kama Gavana wa msituni, washenzi, maharamia yalitafsiriwa kuwa ni kashfa kwa Serikali ya kikoloni, hivyo Mwalimu Nyerere alishtakiwa kwa kuikashifu Serikali.

Gazeti la Sauti ya Tanu wakati huo lilikuwa likisambazwa kwenye matawi ya Tanu nchi nzima na kwenye vyama mbalimbali vya kupigania uhuru barani Afrika.

Gazeti hilo pia, lilikuwa likitumwa kwa Watanganyika waliokuwa wakisoma nje ya nchi kama vile Asia, Ulaya na hasa Uingereza na Umoja wa Mataifa (UN).

Kwa kuwa lilikuwa likiandikwa kwa lugha ya Kiswahili, gazeti hilo lilitafsiriwa na vyombo vya dola vya wakoloni na kusomwa kwa Kiingereza kwa watawala wa Kikoloni ambao hawakuijua vizuri lugha hiyo.

Baada ya kusomwa, ilipita wiki moja, ndipo Serikali ya Kikoloni ilipoanzisha kesi. Ilikuwa Juni 5, 1958 saa 10 jioni ambapo makao makuu madogo ya Tanu katika Mtaa wa Lumumba wakati huo ukiitwa New Street Na.25, yalivamiwa na Polisi wa upelelezi wakiongozwa na Kaimu Kamishna wa Polisi aliyejulikana kwa jina la MT. Mackenly.

Mackenly alimwambia Nyerere kwamba walikuwa akitafuta gazeti la Sauti ya Tanu Na.29 na Nyerere alimpa nakala moja.

Pamoja na kupewa nakala hiyo, aliendelea kupekua jengo hilo na kutafuta nyaraka zikiwamo hati, majarida baada ya kumwonyesha Nyerere hati ya kufanya upekuzi huo.

Wakili Pritt

Baada ya kesi kuanza, Chama cha Tanu kiliipa uzito wa kipekee kwa kumwita wakili maarufu wakati huo kutoka Uingereza, hayati DN Pritt akiongoza mawakili KL Jhaveri na Mahamoud Rattansey kuja kumtetea Nyerere.

Wakili Pritt ndiye aliyemtetea Rais wa kwanza wa Kenya, Jomo Kenyatta katika kesi ya Mau Mau na akashinda.

Nyerere alifikishwa mahakamani Juni 9, 1958 kwa makosa matatu ya kashfa na kesi yake ilipewa nambari 2207/58.

Ilikuwa kesi hiyo isikilizwe mwezi mmoja baadaye yaani Julai. Julai 7, 1958, Tanu ilikuwa ikifanya maadhimisho ya miaka minne tangu kuanzishwa kwake.

Maadhimisho hayo yalifanyika katika Uwanja wa Uhuru ambao awali ulikuwa ni uwanja wa ndege. Ulifanyikia kule kwa sababu mikutano ilizuiwa kufanyika Uwanja wa Mnazi Mmoja kwa sababu ya kuongezeka kwa wasikilizaji.

Akihutubia katika mkutano huo, Mwalimu Nyerere aliwatahadharisha wana Tanu kuwa makini siku ya kesi hiyo iliyokuwa ikimkabili baada ya siku mbili.

“Tulieni kimya hata kama mtachokozwa. Mashtaka yangu haya ni hatua nyingine ya kuendelea mbele mapambano yetu,” alisema Nyerere (Uk.9).

Alisema hakuna hata nchi moja duniani iliyopigania uhuru wake bila kutoka jasho. Alisema chama hicho kitaendelea kufungua matawi yake katika wilaya nyingine.

Siku ya kesi

Kitabu hicho kinaendelea kueleza hali ilivyokuwa mahakamani baada ya hakimu LA Davis kuingia mahakamani. Mwendesha mashtaka maarufu wakati huo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, JC Summerfield alimtaka Mwalimu Nyerere kusimama kizimbani, Nyerere akaingia.

Watu waliokuwa mahakamani hapo wakasimama ghafla kwa mshtuko na kusema ‘uhuru’ Nyerere hakujibu.

Nyerere akasomewa mashtaka yake ambayo ni pamoja na kumkashifu DC Weeks wa Musoma katika makala ya Sauti ya Tanu Na.29 la Mei27, 1958. Pili, alimkashifu DC Scott wa Songea na tatu kuwakashifu kwa pamoja maofisa hao.

“Unakiri kosa hilo, alihoji Summerfield. ‘Hapana,” alijibu Nyerere.

Summerfield alisema, “Jambo lenyewe ni dogo tu, mahakama hii itabidi kuchunguza, je, ni kweli mshtakiwa alikuwa na ridhaa ya kuandika na kuchapisha maneno hayo? Kama hivyo ndivyo, je, maneno hayo yaliwahusu kweli Ma-DC hao wawili? Je maneno hayo yanaweza kuwa kashfa kwa Ma DC hao wawili?

“Hayo ndiyo masuala ya msingi ambayo mahakama hii tukufu, itabidi kuyachunguza na kuyathibitisha. Kwa ufupi maneno yaliyoandikwa katika Sauti ya Tanu hayana kingine isipokuwa kuvunja uaminifu wa watu waliokuwa kwa Ma-DC wao ambao umekuwa tangu zamani,” alisema Summerfield.

Hukumu

Baada ya kesi hiyo kusikilizwa na mashahidi kutoa ushahidi wao, mahakama ilikumta Nyerere na hatia kwa baadhi ya mashtaka.

Hatua hiyo ilifikiwa baada ya mabishano ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na mawakili wa Nyerere aliolalamikia baadhi ya mashahidi kuhamishwa maeneo yao ili washindwe kufika mahakamani.

Agosti 13, 1958, Nyerere alikutwa na hatia ya mashtaka mawili ya kuwaita watawala wa kikoloni ‘washenzi na maharamia.’

Tanu ilichukua tahadhari kubwa kuwaandaa watu wasije kufanya ghasia, hata kama hukumu hiyo itakuwa ya kifungo.

Maelfu ya wananchi hasa wanawake wakiongozwa na Bibi Titi Mohamed, mwanasiasa maarufu wakati huo na kiongozi wa kina mama, walijaa ufukweni wengine wakiwa na watoto, kungojea litakalompata kiongozi wao.

Dakika chache kabla ya mahakama haijaanza, Mwalimu Nyerere akiandamana na John Rupia, Makamu Rais wa Tanu wakati huo, waliwasili mahakamani. Pritt alikwisharuka kurejea London Uingereza na kwa upande wa mashtaka uliongozwa na Rattansey akisaidiwa na Jhaveri.

Polisi wengi walikuwapo mahakamani siku hiyo wakati huo Mahakama ya Hakimu Mkazi ikiwa barabara ya Kivukoni Front.

Hakimu Davies alipotoa hukumu alizungumzia mwenendo mzima wa kesi hiyo na kumaliza kwa kusema:

“Halikuwa jambo la kawaida kujitenga na adhabu ya kifungo kwa makosa kama haya na mimi sitaki kujitenga na desturi hiyo. Namtoza mshitakiwa faini ya Sh3,000 au kwenda jela miezi sita. Nampa mshtakiwa muda wa siku mbili kulipa faini hiyo.”

Baada ya hukumu hiyo kutolewa, nyimbo na nderemo ziliikumba Mahakama ya Hakimu Mkazi.

0754897287 na [email protected]