Samia ndiye pekee hana presha na cheo chake

Rais John Magufuli akifurahia jambo na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, wakati Rais na Waziri Mkuu walipomtembelea Samia ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam, Novemba mwaka jana. Picha na OMR

Muktasari:

MAKAMU WA RAIS

  • Makamu wa Rais, Samia Hassan Suluhu alizaliwa mwaka 1960. Amewahi kuwa mbunge wa Jimbo la Makunduchi Zanzibar kati ya mwaka 2010 hadi 2015.
  • Pia, amewahi kushika wadhifa wa waziri anayeshughulikia masuala la Muungano katika Ofisi ya Rais tangu mwaka mwaka 2010.
  • Vilevile aliwahi kuwa waziri katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Rais Amani Karume. Mwaka 2014 alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba (BMK).
  • Julai 2015, alichaguliwa na mgombea wa kiti cha urais wa CCM, Dk John Magufuli kuwa mgombea mwenza.

Ipo habari iliyovumishwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, aliandika barua ya kujiuzulu baada ya kutofautiana na Rais John Magufuli.

Siku moja baadaye, Ofisi ya Makamu wa Rais, Ikulu, Dar es Salaam, ilitoa majibu ya kukanusha uvumi huo.

Kama uvumi huo ungekuwa chanya, maana yake Serikali ya Rais Magufuli ingeweka rekodi ya kubadili Makamu wa Rais ndani ya muda mfupi zaidi, yaani ndani ya mwaka wake wa kwanza madarakani.

Ingekuwa kweli basi Samia angeweka rekodi ya kuwa Makamu wa Rais aliyehudumia nchi kwa cheo hicho katika kipindi kifupi zaidi. Angemzidi hata Rais Ali Hassan Mwinyi, aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais kwa mwaka mmoja, kati ya mwaka 1984 mpaka 1985, akiwa Rais wa Zanzibar kabla hajachaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1985.

Kwa sasa, Makamu wa Rais wa muda mrefu zaidi ni Rais wa Pili wa Zanzibar, hayati Aboud Jumbe Mwinyi miaka 12, akifuatiwa na Rais wa sasa wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein miaka tisa kisha marehemu Dk Omar Ali Juma aliyedumu kwa miaka sita kabla ya mauti kumfika.

Tuweke pembeni uvumi

Unapoweka pembeni uvumi huo wa Samia kujiuzulu, hali halisi inamtambulisha yeye kama mtu ambaye hakuwa na presha na cheo chake katika cha takriban miezi 12 ya Rais Magufuli tangu aingie madarakani.

Kipindi hicho kilikuwa cha presha kwa watendaji wote wa Serikali ya Rais Magufuli. Hakuna ambaye alikuwa anaweza kujiona yupo salama zaidi ya Samia na Magufuli mwenyewe.

Uhakika wa Samia kwa cheo chake upo kikatiba. Magufuli hana mamlaka ya kikatiba kumng’oa Samia bila kulishawishi Bunge kisha nalo liridhie kumuondoa. Mzunguko huu ndiyo ambao unamlinda Samia na kumfanya asiwe na presha kama wengine katika Serikali ya Rais Magufuli.

Ibara ya 50 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inatamka ifuatavyo kuhusu Makamu wa Rais, kwamba (1) Atashika kiti cha Makamu wa Rais kwa muda wa miaka mitano tangu alipochaguliwa kuwa Makamu wa Rais.

Ibara hiyo inaendelea (2) Makamu wa Rais atashika kiti hicho hadi (a) muda wake utakapokwisha; (b) Akifariki dunia akiwa katika madaraka; (c) Atakapojiuzulu; (d) Atakapoapishwa kuwa Rais baada ya kiti cha Rais kuwa wazi; (e) Atakapotiwa hatiani kwa kosa lolote la jinai linaloonyesha utovu wake wa uaminifu;

(f) Atakapoapishwa Rais mwingine kushika nafasi ya Rais pamoja na Makamu wake; (g) Atakapoondolewa madarakani baada ya kushtakiwa bungeni kwa mujibu wa masharti ya ibara ndogo ya (3) ya ibara hii; (h) Atakapoacha kushika kiti cha Makamu wa Rais vinginevyo kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii.

Ibara hiyo ya 50 inazidi kueleza namna Makamu wa Rais anavyoweza kutolewa, (3) Bunge litakuwa na madaraka ya kumuondoa Makamu wa Rais madarakani kama yale liliyonayo kuhusiana na Rais, isipokuwa kwamba hoja yoyote ya kumshtaki Makamu wa Rais itatolewa tu kama inadaiwa kwamba:-

(a)  Rais amewasilisha hati ya Spika inayoeleza kwamba Makamu wa Rais ameacha au ameshindwa kutekeleza kazi za Makamu wa Rais; (b) ametenda vitendo ambavyo kwa jumla vinavunja Katiba au Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma;

(c) Ametenda vitendo ambavyo vinakiuka maadili yanayohusu uandikishwaji wa vyama vya siasa yaliyotajwa katika ibara ya 20(2) ya Katiba; au (d) amekuwa na mwenendo unaodhalilisha kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano au kiti cha Makamu wa Rais.

Pamoja Katiba, zipo sheria zinazoulinda muda wa Makamu wa Rais kushika madaraka. Ipo Sheria ya mwaka 1994 ibara 11, Sheria namba 12 ya mwaka 1995 ibara ya 6 na Sheria namba 3 ya mwaka 2000 ibara ya 10.

Hivyo Samia kutokana na ulinzi alionao kisheria na kikatiba, ni sahihi kusema kuwa hakupitia vipindi vya presha kwamba angeweza kuamka na kukuta nafasi yake imetenguliwa kisha nafasi kupewa mtu mwingine.

Wengine ni uamuzi wa Rais

Upande wa makatibu wakuu, makatibu tawala, wakurugenzi na wengine ambao ajira zao siyo uteuzi wa kisiasa, wengi wameondolewa kwenye nafasi zao kwa lugha ya kupangiwa kazi nyingine. Maana kuwaondoa kazini ni suala la kukatisha ajira ambalo lina hali zake ngumu.

Hii imekuwa sababu ya kuwepo kwa kundi kubwa ambalo Rais Magufuli ameliahidi kazi nyingine, lakini wanaendelea kuvuna mishahara ileile kutokana na taratibu za utumishi wa umma na ajira kwa jumla.

Upande wa mawaziri wakiongozwa na waziri mkuu, wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya, wao ndiyo hakuna gharama yoyote, anapoamua tu wa kwenda pembeni atakwenda. Wao hata hawana haja ya kuambiwa wasubiri kazi nyingine kwa sababu nafasi zao ni za kisiasa.

Ilitokea kwa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anne Kilango Malecela kwa bahati akaambiwa asubiri kazi nyingine. Ni bahati, maana kisiasa ukitenguliwa kwa mtindo wa kufanya makosa, hupaswi kupelekwa kwingine. Unatakiwa kukaa benchi ukiwashuhudia wengine wakitenda. Kilango mpaka sasa hajapangiwa kazi nyingine.

Presha kwa uteuzi wa nafasi za kisiasa ni kwa sababu kuwepo kwenye nafasi kunategemea matakwa ya Rais. Unaweza usifanye vibaya lakini kama humvutii anakuweka pembeni.

Ni uamuzi wake, maana nchi imekabidhiwa kwake kwa miaka mitano, mwaka 2020 atatakiwa kusema aliitumiaje dhamana aliyopewa. Hivyo, anapoona mtu fulani hafanyi anavyotaka anambadilisha bila hata kutoa maelezo. Kutoa maelezo kwa Rais anapomuondoa waziri kwenye Baraza la Mawaziri ni uungwana tu lakini si lazima.

Mamlaka hayo aliyonayo ukijumlisha na moto ambao Rais Magufuli alikuwa nao tangu alipoingia ofisini Novemba 5, mwaka jana, imekuwa sababu ya watendaji wengi serikalini kuwa na presha pamoja na hofu ya kuenguliwa kama siyo kutumbuliwa.

Uamuzi uliotisha zaidi

Aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue aliwekwa pembeni muda mfupi baada ya kula kiapo cha kuendelea na majukumu yake.

Katibu Mkuu kiongozi ambaye ni mtumishi wa umma namba moja katika nchi alipoondolewa kwa mtindo ambao Dk Magufuli aliufanya, ni ishara kuwa hakukuwa na aliyejiamini yupo salama.

Sefue ndiye alikuwa msoma majina ya waliotumbuliwa. Katika siku 100 za mwanzo za Rais Magufuli Ikulu, kila Sefue alipoonekana kwenye runinga, watu walisogea kuona nani ambaye anatumbuliwa.

Hata hivyo, wakati wake naye ulifika na Balozi John Kijazi, aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu Kiongozi. Uamuzi huo ulizidisha hofu kwa watendaji wengine kuzidi kuona kuwa Rais Magufuli hana uswahiba wala kujuana.

Kilango ni mke wa Waziri Mkuu katika Serikali ya Awamu ya Pili, Dk John Malecela ambaye pia alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hivyo ni mke wa kigogo katika nchi.

Machi 15, mwaka huu wakati Dk Magufuli akiwaapisha wakuu wa mikoa, Ikulu, Dar es Salaam, alimtania Dk Malecela: “Namuona mzee Malecela amesindikiza mke wake. Hii inaonyesha watani zangu Wagogo walivyo na upendo kwa wake zao.”

Pamoja na utani huo, Kilango ndiye aliyeweka rekodi ya kuwa mteule wa Dk Magufuli aliyetenguliwa ndani ya muda mfupi zaidi, maana alikaa ofisini siku 27 kisha akamuondoa kwa maelezo kuwa alitoa taarifa batili kuhusu watumishi hewa.

Kilango, aliteuliwa Machi 13, mwaka huu kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Machi 15, aliapishwa na Aprili 11, mwaka huu, yaani siku 27 baada ya kiapo chake cha kazi, Rais Magufuli alitangaza kutengua uteuzi wake.

Swahiba wake Kitwanga

Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga ambaye ni Mbunge wa Misungwi (CCM), anatajwa kuwa rafiki hasa wa Dk Magufuli. Hata hivyo pamoja na urafiki wao alimuweka kando.

Kuthibitisha urafiki wao, Dk Magufuli alimuombea kura Kitwanga kwa wapiga kura wa Misungwi, akisema kuwa anamfahamu, ni rafiki yake, wamesoma wote Chuo Kikuu Dar es Salaam na anampenda.

“Naomba mumchague Kitwanga nikafanye naye kazi, namfahamu sana, nimesoma naye Chuo Kikuu Dar es Salaam na nampenda sana,” alisema Magufuli mbele ya maelfu ya wananchi waliohudhuria mkutano huo wa kampeni.

Dk Magufuli alitengua uteuzi wa Kitwanga Mei 20, mwaka huu, hivyo kumtupa nje ya Baraza la Mawaziri kwa maelezo kuwa aliingia bungeni akiwa amelewa na kutoa majibu yasiyotosheleza kuhusu wizara yake.

Kasi hiyo ya kutumbua na kutengua uteuzi wa watu, ndiyo ambayo ilifanya wengi wajione hawapo salama katika mwaka mzima wa kwanza wa Rais Magufuli Ikulu. Hata rafiki ameshughulikiwa wengine je? Ila Samia hakuwa na presha.

Mwandishi wa makala haya ni mwandishi wa habari, mchambuzi wa siasa, jamii na sanaa. Ni mmiliki wa tovuti ya Maandishi Genius inayopatikana kwa anuani ya mtandao www.luqmanmaloto.com