Sekta binafsi ni muhimu kukuza uchumi, kufanikisha utekelezaji malengo endelevu

Thursday November 9 2017

Mtendaji mkuu wa mtandao wa Umoja wa Mataifa

Mtendaji mkuu wa mtandao wa Umoja wa Mataifa kuratibu mpango wa maendeleo endelevu (Global Compact), Lise Kingo akizungumza na watendaji wa sekta binafsi nchini. 

By Mussa Juma, Mwananchi [email protected]

Tanzania ni miongoni mwa mataifa 193, wanachama wa umoja wa mataifa(UN)  ambayo yameridhia kutekeleza malengo 17 endelevu (SDG) tangu yaliporidhiwa Septemba mwaka 2015.

Miongoni mwa malengo hayo ni kutokomeza umasikini, kukabiliana na janga la njaa na kuongeza uhakika wa chakula, na kuhakikisha afya bora kwa wote.

Mengine ni usawa  wa kijinsia,  kuimarisha miundombinu ya elimu,  kulinda viumbe majini  na kuimarisha mbinu za utekelezaji na ushikiano wa kimataifa kwa ajili ya maendeleo endelevu.

Lengo kuu la mpango huo ni kuleta uwiano wa maendeleo katika nchi moja moja na kwa ujumla ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na umaskini ambayo ni ya haraka.

Hivyo kulingana na maazimio ya utekelezaji wa malengo hayo, kila nchi inapaswa kuwa na mkakati wa kuyatekeleza. Katika hili, umuhimu wa sekta binafsi unatajwa.

Nchini, sekta hiyo bado inakabiliwa na changamoto kadhaa. Tathmini ya Benki ya Dunia kwenye ripoti yake ya 10 ya tathmini ya mwenendo wa uchumi wa Tanzania inaonyesha kuongezeka kwa mikopo isiyolipika, kutoongezeka kw amikopo ya sekta binafsi na kupungua kwa uwekezaji kutoka nje.

Benki hiyo inaitaka serikali kushughulikia haraka changamoto zinazoikabili sekta binafsi ili kuongeza mchango wake kwenye pato la taifa. Inasema: “Sekta binafsi imara inaweza kufanikisha utekelezaji wa malengo na mikakati ya serikali kwani ni chanzo cha ubunifu na ajira za uhakika.”

Mkurugenzi mkazi Umoja wa Mataifa (UN), Alvaro Rodriguez anasema kampuni na taasisi binafsi zina nafasi kubwa ya kufanikisha utekelezaji wa malengo hayo kwenye mataifa mengi duniani.

“Utekelezaji utafanikiwa sana ikiwa sekta binafsi itashirikishwa kwani ni wadau muhimu,” anasema.

Rodriguez anasema Watanzania wengi ni masikini hivyo ni muhimu kuweka mikakati ya pamoja kukuza uchumi kuleta usawa wa maendeleo. miongoni mwa maeneo ambayo sekta binafsi inaweza kusaidia ni vita dhidi ya ya rushwa kwa sababu ni adui mkubwa wa maendeleo katika taifa lolote.

“Rushwa inasababisha watu kuwa masikini, inakosesha huduma bora za afya na kukwamisha mipango ya maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwapo elimu  hivyo ikipunguzwa, maendeleo yatakuja,” anasema.

Sekta binafsi imara, anasema ina mchango mkubwa katika kutatua matatizo ya kijamii, kiuchumi na kimazingira ili kuwezesha dunia kuwa salama kwa wote.

Anasema ingawa Serikali ya awamu ya tano, inafanya vizuri katika vita dhidi ya rushwa na kupunguza matumizi, bado kuna umuhimu wa kuishirikisha sekta binafsi kuhakikisha Tanzania inafanikiwa katika utekelezaji wa malengo endelevu ya dunia.

Mkurugenzi wa mtandao wa umoja wa mataifa kuratibu utekelezaji wa malengo endelevu 17 ya maendeleo, Lise Kingo anasema rushwa ni moja ya vikwazo vinavyochangia umasikini katika nchi nyingi za Afrika na kuzichelewesha kupata maendeleo ya haraka kijamii, kiuchumi na mazingira.

“Kutokana na hali hiyo UN inaona sekta binafsi ni wadau muhimu katika utekekezaji wa malengo endelevu ya maendeleo na ndio maana imeanza kuwashirikisha,” anasema.         

Sekta binafsi

Mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Godfrey Simbeye anasema ni ukweli uliowazi kuwa sekta binafsi ni mdau mkubwa kufanikisha utekelezaji wa malengo endelevu 17 ya maendeleo.

Hata hivyo, anasema bado ushirikishwaji si mkubwa nchini katika kuhakikisha utekelezaji makubaliano unafanikiwa.

Anasema moja ya mambo makubwa ambayo sekta binafsi imeanza kushiriki ni vita dhidi ya rushwa na kwamba wanachama wake tayari 60 wamejiunga na mtandao wa kutekeleza malengo endelevu ya umoja wa mataifa.

Hata hivyo, anasema miongoni mwa sababu za rushwa ni urasimu uliopo serikali na kukosekana uwazi katika baadhi ya taasisi.

“Tunajua, watoa rushwa kubwa ni sekta binafsi kwenda kwa watendaji wa serikali. Tunaweza kuondoa tatizo hili tukishirikiana kuondoa vichocheo vilivyopo vya rushwa,” anasema.

Anasema kwa kawaida rushwa kubwa inatolewa katika kushinda zabuni za utekelezaji wa miradi mbalimbali hivyo ushirikiano ni muhimu kukabiliana na hali hii.

“Tunahitaji kushirikiana na serikali, jumuiya na taasisi za kimataifa na miongoni mwetu. Tumeanzisha mtandao wa utekelezaji wa maendeleo endelevu na tunataka kampuni na taasisi nyingi zijiunge,” anasema.

Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Tigo, Simon Karikari anasema  sekta binafsi ni kichocheo kikubwa cha maendeleo ni muhimu kushirikishwa katika mikakati ya taifa.

Anasema Tanzania iliyo katika harakati ya mapinduzi ya viwanda ni muhimu kufanyakazi na sekta binafsi ambayo itajenga viwanda na kuongeza uwekezaji.

Karikari anasema hata hivyo sekta hiyo inahitaji mazingira mazuri ya uwekezaji, kutokuwapo kwa urasimu na rushwa katika uwekezaji.

“Kwa sasa serikali imefanikiwa kudhibiti rushwa jambo linaloungwa mkono na sekta binafsi,” anasema.

Anasema anaamini Tanzania itafikia baadhi ya malengo kutokana na uboreshwaji wa sheria mbalimbali, kupungua kwa urasimu na rushwa.

“Tigo tutaendelea kuongeza uwekezaji kwani bado kuna fursa na kwa ujumla hakuna vikwazo vingi vya kibiashara,” anasema.

Mkurugenzi mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk Charles Kimei anasema sekta binafsi inaenda vizuri licha ya changamoto chache zilizopo na kuimarika kwa taasisi nyingi kunaongeza imani.

“Uimara wa sekta binafsi ni muhimu kwa maendeleo ya wananchi kwa ujumla. Licha ya changamoto zilizopo, tumeweza kutoa huduma nzuri na kuaminiwa hata na taasisi za kimataifa ambazo zimekubali kutukopesha ili tuwahudumie wajasiriamali nchini,” anasema.

Anasema kila taasisi inapaswa kupambana na rushwa kuanzia ndani kabla ya kwenda kwa watumishi wa umma na taasisi zao. “Kwa upande wetu CRDB, tunachukua hatua kali kila tunapopata taarifa za watumishi kujihusisha na vitendo hivyo,” anasema.

Mtendaji mkuu wa mfuko wa mashirika yasiyo ya kiserikali (CSF), Francis Kiwanga anasema ushiriki wa sekta binafsi ni muhimu sana katika kufikia malengo ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa.

Anasema utekelezaji wa malengo hayo, ambao unafanyika hatua kwa hatua utafanikiwa zaidi kama ukifanywa kwa uwazi na kushirikisha wadau wote muhimu.

“Ingawa utekelezaji wa malengo haya ni hiyari kwa kila taifa lakini ni muhimu ili kuchochea maendeleo ya wananchi pia na kuondokana na umasikini,” anasema Kiwanga ambaye ni wakili wa kujitegemea pia.

Akifungua mkutano huo, Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Vijana, Anthony Mavunde alisema serikali italifanyiakazi suala hilo kuhakikisha inatekeleza malengo hayo endelevu.

Katika kukuza uchumi, anasema sekta binafsi imepewa fursa kubwa ya kuwekeza wakati serikali ikiendelea kuboresha mazingira ya usimamizi na ufanyaji biashara kuhakikisha uchumi unakua na kupunguza umasikini.

Advertisement