UCHAMBUZI: Sh50 milioni kwa kila kijiji zitoke wananchi wafanye kazi

Muktasari:

Mirija kadhaa imeminywa na vijana wengi wanakosa kazi. Kwa mfano, taarifa za Bandari ya Dar es Salaam kusitisha kuzitumia baadhi ya bandarikavu ambazo zilikuwa na watumishi waliokuwa wakiendesha maisha yao na kuhudumia familia, hivyo kuwa na mchango kwenye jamii inayowazunguka.

Fedha za mipango ya dakika moja, zimeanza kutoweka Tanzania. Mifuko ya vijana wa mijini imekauka. Kila kijiwe utakachopita utakutana na malalamiko haya lakini ukiwauliza awali walikuwa wakizipata vipi, hawana maelezo ya kutosha.

Mirija kadhaa imeminywa na vijana wengi wanakosa kazi. Kwa mfano, taarifa za Bandari ya Dar es Salaam kusitisha kuzitumia baadhi ya bandarikavu ambazo zilikuwa na watumishi waliokuwa wakiendesha maisha yao na kuhudumia familia, hivyo kuwa na mchango kwenye jamii inayowazunguka.

Mambo yamebadilika, watu waliozoea kupata fedha nyingi baada ya kazi ndogo wamepoteza uelekeo, lakini wenye mipango mizuri ya maisha wanakwenda sambamba na sera za Serikali zilizopo.

Pamoja na yote hapo juu, ipo haja kwa Serikali kuanza kutoa fedha kwa miradi ya maendeleo ili Watanzania wengine wapate ajira. Watanzania hawajasahau ahadi zilizotolewa wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.

Wengi wanakumbuka kwamba miongoni mwa ahadi za Dk John Magufuli wakati wa kampeni ni kutoa Sh50 milioni kwa kila kijiji nchini kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Kwa bahati nzuri, Rais Magufuli anaikumbuka vyema ahadi hiyo na tayari kwenye bajeti yake ya kwanza ametenga Sh811 bilioni kwa ajili ya kuitekeleza.

Wakati wa vikao vya Bunge la Bajeti, ilielezwa kwamba Serikali imeshaanza kushirikisha wadau mbalimbali kupata maoni ya jinsi ya kufanikisha mpango huo, kwa ufanisi na tija kwa ajili ya Watanzania.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alinukuliwa akisema Serikali imetenga Sh59 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa ahadi hiyo. Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, Anthony Mavunde alizungumza bungeni kwamba Serikali itaanza kutekeleza ahadi ya Rais Magufuli ndani ya mwaka huu wa fedha.

Si hao tu, walioeleza juu ya azma hiyo. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama alieleza kwamba Serikali inaweka utaratibu mzuri wa kuzifikisha vijijini, fedha za ahadi ya Rais ili Watanzania wote wanufaike bila kujali itikadi zao za kisiasa.

Vilevile, ilielezwa kwamba Baraza la Uwezeshaji Kiuchumi limepewa jukumu la kuandaa utaratibu wa kuzifikisha fedha hizo kwa wahusika. Pamoja na maelezo mazuri ya Serikali, ipo haja ya kuanza kutekeleza ahadi hii kwa vitendo.

Vijana, wazee na wanawake wanazisubiri kwa hamu fedha hizo ili wafanye shughuli zao za maendeleo. Vijiji vingi vimejaa vijana wanaofanya shughuli ndogondogo za kiuchumi mfano biashara, kilimo, ufugaji na hivyo wanaamini wakizipata zitawaongeza mtaji.

Baraza liharakishe mchakato huu na kutoichelewesha ahadi ya Rais. Kama zitatolewa kwa mfumo wa mkopo kupitia vikundi vya ujasiriamali, ni vizuri baraza likaeleza ili kuondoa utata wowote unaoweza kujitokeza hapo baadaye.

Baraza litangaze utaratibu na kuepuka kuwa kikwazo cha wananchi kupata fedha za ahadi ya Rais. Wananchi wanazihitaji kwa ajili ya biashara, kununua mazao, kuchimba mabwawa ya samaki, ufugaji wa kuku, ng’ombe wa maziwa na kilimo cha mbogamboga.

Kabla ya kuanza kutolewa ni vizuri wananchi watakaobahatika kuzipata wasaidiwe kwa mafunzo, ili watakapoanza kuzifanyia kazi ziweze kuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi kwao na kwa Taifa.

Pia, Sh50 milioni kwa kila kijiji zisaidie kuongeza ajira kwa Watanzania ili ‘mifuko’ yao ianze kujaa fedha.

Lauden Mwambona ni Mwandishi Mwandamizi wa Mwananchi mkoani Mbeya. Anapatikana: [email protected]