Simba ilikomba pointi 20, Kanda ya Ziwa na Nyanda za Juu Kusini

Muktasari:

  • Haikuwa rahisi miaka ya nyuma, Simba kupata mteremko katika mechi zake za mikoani hasa Kanda ya Ziwa na Nyanda za Juu Kusini.

Ni mwaka wao. Hii ndio kauli unayoweza kuwaambia Simba ambao ndoo yao ya ubingwa wamekabidhiwa juzi na Rais John Magufuli kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam licha ya kupigwa bao 1-0 na Kagera.

Haikuwa rahisi miaka ya nyuma, Simba kupata mteremko katika mechi zake za mikoani hasa Kanda ya Ziwa na Nyanda za Juu Kusini.

Toto Africans iliwapa shida, kadhalika Kagera Sugar na Mbao lakini katika harakati zao za ubingwa msimu huu, mambo yalikuwa ubwete kwa sana. Simba iliingia Uwanja wa Kaitaba wakawapiga Kagera mabao 2-0 kwa mabao ya kawaida kabisa, wala hawakupata tabu licha ya wenyewe kulipa kwa 1-0.

Timu nyingine ngumu Kanda ya Ziwa ni Mbao FC, waliowafunga Yanga mabao 2-0, lakini wao walijitutumua na kutoka sare ya mabao 2-2 huku wakiipa kipigo cha mabao 5-0 Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Simba iliibutua Stand United ‘Chama la Wana’ ambao waliwafunga mabao 2-1 katika dimba la Kambarage, na wakatoka sare ya mabao 3-3, Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mabingwa hao waliwachapa Mwadui mechi zote, iliifunga mabao 3-2 Dar es Salaam na kwenye marudiano wakawapiga 2-0 huko huko Shinyanga.

Nyanda za Juu Kusini sasa. Simba ilivuna pointi sita Uwanja wa Sokoine kwa Prisons na Mbeya City, wakifungwa bao 1-0 kila mmoja, lakini katika mechi za marudiano Taifa, City iliambulia kipigo cha bao 2-0, wakati Prisons ikipigwa 3-1. Simba walikumbana na magumu kwa kutoka kwa Lipuli, huku wakivuna pointi sita za Njombe Mji, wakiwafunga 4-0 Uwanja wa Taifa na ugenini wakitoka mabao 2-0.

Simba watamaliza mchezo wao na Majimaji ya Songea ambao waliilaza 4-0 jijini Dar es Salaam.