TEHAMA : Ubunifu unaorahisisha maisha

Muktasari:

  • Makala haya yanaangazia orodha mpya ya mambo mapya ya kiteknolojia yanayoendelea kwingine duniani. Hii iwe changamoto kwetu katika kujiandaa na changamoto za maisha.

Ukijua mwenzako anafanya nini, utaweza kujua jinsi ya kujipanga au hata kusaidia wengine wajipange kwa ajili ya maisha yajayo.

Makala haya yanaangazia orodha mpya ya mambo mapya ya kiteknolojia yanayoendelea kwingine duniani. Hii iwe changamoto kwetu katika kujiandaa na changamoto za maisha.

Exohand ni mkono wa bandia uliobuniwa kisha kuundwa na kampuni ya Nuada yenye makazi nchini Ureno. Mkono huo una uwezo wa kubeba mzigo wenye kilo 40 bila hata kugusa mkono halisi.

Mbunifu wa mkono huo anaitwa Filipe, anasema alibuni kitu hiki baada ya kuumia mkono wakati wa mazoezi ya kujilinda, kitu kilichomfanya kushindwa kabisa kufanya baadhi ya kazi.

Sehemu nyingine za dunia kama Urusi, ubunifu wa Exo kwa ajili ya kusaidia shughuli za binadamu unaenda kasi na matarajio ni kwamba mambo yakienda vizuri, masuala ya elimu, tiba na matibabu ya viungo yatabadilika haraka.

VICTORY ni mradi wa Jeshi la Marekani wenye lengo la kuhakikisha wanajeshi, vifaa, silaha na waongoza vita wanawasiliana kwa wakati mmoja kwa kutumia sauti, video na njia nyingine mbalimbali za kidigitali.

VICTORY ni kifupi cha Vehicle Integration for C4ISR/EW Interoperability. Mradi huu utasaidia kwa kiasi kikubwa kufanya vyombo hivi kuwasiliana na kupunguza gharama nyingi za kuendesha operesheni mbalimbali.

Kupitia teknolojia hii, viongozi wataweza kujua kila alipo mwanajeshi na kile anachofanya akiwa na vifaa mbalimbali. Jeshi la Marekani litaanza kutumia teknolojia hii baadaye mwaka huu.

Jiji la New York nchini Marekani limeanza kuwasiliana na kampuni kadhaa ili kuanzisha mradi wa kupiga picha na kutambua madereva wote wa magari wanaoingia na kutoka ndani ya jiji muda wote.

Teknolojia ya kutambua sura ya mtu inaitwa ‘Facial Recognition’ katika kona zote, vituo vya mafuta, kwenye mataa, madukani na maeneo mengine nyeti kutakuwa na kamera zitakazoweza kupiga picha na kujua dereva wa gari, namba za gari na kama dereva ana makosa yoyote.

Hii itasaidia kutambua wahalifu kabla ya kutekeleza tukio au hata kujua baada ya jambo hilo. Kutokana na mradi huo maeneo mengi ya Jiji la New York yataboreshwa ili kuweza kuendana na utumiaji wa teknolojia za kisasa.

Teknolojia kama hii ipo pia katika Jiji la Moscow nchini Urusi. Imeboreshwa zaidi kwani ukishapigwa picha, hata akaunti zako kwenye mtandao ya kijamii zinaweza kujulikana na wahusika.

Serikali ya India imeanzisha kitengo maalumu cha kupambana na uhalifu wa kimtandao kinachoitwa Computer Emergency Response Team. Kitengo hicho hakijulikani kitakua chini ya wizara gani, lakini kitahusisha wataalamu mbalimbali wa masuala ya kompyuta na wanasayansi pia kitashirikiana na taasisi mbalimbali za fedha.

Kitengo hicho kimeanzishwa kutokana na kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu kwa njia ya mtandao. Kwa mfano, mwaka 2016 pekee, kadi za benki zaidi ya milioni 2 ziliingiliwa kwa minajili ya uhalifu.