MAONI YA MHARIRI: TRA, wafanyabiashara wawajibike kwa hili la EFD

Muktasari:

Ni kwa sababu hii, watu wengi wakiwamo wafanyabiashara wamekuwa wakiutumia udhaifu huo kama mwanya wa kukwepa kulipa kodi na hivyo kuikosesha nchi mapato.

Hivi karibuni tuliandika tahariri tukiinyooshea kidole Mamlaka ya Mapato Tanzania ( TRA) kwa kutokuwa na miundombinu bora ya ukusanyaji wa mapato.

Ni kwa sababu hii, watu wengi wakiwamo wafanyabiashara wamekuwa wakiutumia udhaifu huo kama mwanya wa kukwepa kulipa kodi na hivyo kuikosesha nchi mapato.

Kwa mfano, takwimu za Serikali zinaonyesha kuwa katika mwaka unaoishia Juni 2017, TRA ilifanikiwa kukusanya Sh14.4 trilioni ikiwa ni pungufu kwa Sh700 bilioni. Upungufu huo ni kwa sababu ilijiwekea lengo la kukusanya Sh 15.1 trilioni.

Hiki siyo kiwango kidogo cha nakisi na ndio maana tukaishauri TRA kuimarisha mifumo yake ya utendaji ili nchi ipate kodi zaidi kwa maendeleo yake. Moja ya njia za kukuza makusanyo ya kodi ni matumizi ya mashine za kielektroniki za risiti (EFD).

Hata hivyo, inasikitisha kuwa matumizi ya mashine hizo yamekuwa yakipigwa danadana. Kilichopo ni kuwa wafanyabiashara wanakwepa kwa makusudi kuzitumia. Lakini pia tunaamini kutotumika kwake kunatokana na udhaifu kutoka kwa vyombo husika.

Kipimo kikubwa cha watu kukwepa kodi nchini tunaweza kukiona kwa wamiliki wa vituo vya mafuta. Biashara ya vituo hivyo sio ndogo kwa kiasi cha wahusika kujivuta katika matumizi ya mashine hizi za kisasa.

Tunaamini kwamba wafanyabiashara wa mafuta hawashindwi kuwa na mashine hizi japo wenyewe wanadai kuwa zinauzwa kwa bei ghali. Tuna kila sababu ya kuamini kuwa baadhi ya wamiliki wa vituo hivi ni wakwepaji wa kodi na pengine kulikuwa na nguvu inayowakingia kifua.

Aidha, tunashauri wimbo wa matumizi ya mashine hizi kwa wafanyabiashara wote ufike kikomo. Tuliusikia wimbo huu miaka kadhaa iliyopita wakati wa mzozo mkubwa wa matumizi yake kati ya wafanyabishara wa kati na TRA, leo wimbo huohuo unajirudia kwa wafanyabiashara wa vituo vya mafuta.

Haiwezekani kama tunajua umuhimu wa mashine hizi katika mchakato wa ukusanyaji kodi, vyombo husika vinashindwaje kujipanga mpaka Rais ajitokeze hadharani na kuwaonya wafanyabiashara wa mafuta wasiotaka kufunga mashine hizo kwenye vituo vyao?

Tunaamini suala la matumizi ya EFD kwa wamiliki wa vituo vya mafuta na hata wafanyabiashara wengine, lilipaswa kumalizwa tangu siku nyingi pasipo hata Rais kuingilia kati. Ni dhahiri kuna udhaifu mahala ambao mamlaka husika lazima ziwajibike kwa kuufanyia kazi.

Tunapoishauri TRA kujipanga kikamilifu kwa kuwa na mifumo imara ya kukusanya kodi, tunawasihi pia Watanzania wajue kuwa kodi ni kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu.

Tunapolipa kodi, tunaharakisha maendelo ya nchi na ustawi wa wananchi.

Kila mtu aone fahari kulipa kodi hasa katika kipindi hiki ambacho imani ya walio wengi ni kuwa fedha zinazokusanywa zinakwenda kwenye mikono salama kwa ajili ya maendeleo ya nchi.