Tumeshaona Gabon, safari ya Cameroon 2019 ipo?

Muktasari:

Kumalizika kwa fainali hizo zilizokuwa za aina yake nchini Gabon, ndio mwanzo wa safari ya Cameroon 2019, itakayokuwa mwenyeji kwa fainali hizo.

Fainali za Mataifa ya Afrika kwa mwaka huu, Afcon 2017 zimemalizika jana usiku kwa Misri na Cameroon kuonyesha kazi na matokeo kama yalivyokuwa.

Kumalizika kwa fainali hizo zilizokuwa za aina yake nchini Gabon, ndio mwanzo wa safari ya Cameroon 2019, itakayokuwa mwenyeji kwa fainali hizo.

Kumekuwa na mijadala mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii kuhusu nafasi ya Tanznaia, kabla, wakati na sasa baada ya michuano hiyo ya Gabon kumalizika.

Wapo waliosema hatuwezi, walipo wanaosema tunaweza lakini maandalizi. Asilimia kubwa wanasema maandalizi tu yataivusha Tanzania.

Kikubwa kinachosemwa cha maandalizi ni kwamba pamoja na kwamba hakuna wachezaji wa kulipwa wa kutosha kama ilivyo, Senegal, Nigeria, Ivory Coast, Ghana na nyingine, lakini ni mechi za kirafiki za kutosha na mataifa mbalimbali, zinajenga kujiamini kwa wachezaji.

Wasioamini safari ya Tanzania Cameroon 2019 wanaangalia kukosekana kwa wachezaji wengi wa kulipwa. Tanzania ingekuwa na nusu hata robo tatu wa kulipwa walau ingeweza.

Wengine wanaamini kuwa mkono wa Serikali ndio njia pekee ya kuivusha Tanzania.

 

Ratiba ya CAF

Tayari Shirikisho la Soka Afrika, CAF, limetoa ratiba ya makundi na Tanzania imepangwa kundi L pamoja na Uganda, Cape Verde na Lesotho katika mechi za kuwania kufuzu fainali za Afcon za Cameroon 2019.

Mechi ya kwanza ya Taifa Stars itakuwa katikati ya Juni, itaanza kwa kucheza na Lesotho Dar es Salaam kabla ya kuifuata Uganda Machi mwakani.

 

Afcon 1980

Mara ya mwisho Tanzania kufuzu katika mashindano hayo ilikuwa mwaka 1980 lakini tangu hapo kila mara timu yake imekuwa ikiishia njiani.

Katika mashindano hayo yaliyofanyika Nigeria Taifa Stars ilipangwa Kundi A pamoja na wenyeji Nigeria ‘Green Eagles’ sasa Super Eagles, Misri na Ivory wa Coast ingawa ilishika nafasi ya mwisho baada ya kufungwa mechi mbili dhidi ya Nigeria kwa mabao 3-0, Misri mabao 2-1 na kutoka sare ya bao 1-1 na Ivory Coast.

Bado wadau na mashabiki wa soka wanajiuliza, nini sababu inayotufanya tushindwe kufuzu kama zilivyo nchi nyingine kwani hata majirani zetu Uganda mwaka huu waliitoa kimasomaso Afrika Mashariki kuwa timu iliyofuzu kutoka ukanda huu.

Licha ya kuwa walitolewa hatua ya makundi katika mashindano hayo makubwa yaliyofanyika nchini Gabon lakini walithubutu jambo ambalo Tanzania tumeshindwa kwa miaka 37 sasa.

 

Spoti Mikiki ilizungumza na kocha wa Taifa Stars, Salum Mayanga, baadhi ya wachezaji wa zamani wa timu hiyo na wale wa sasa, somo ama nini wamejifunza kutokana na fainali za Gabon zilizomalizika jana usiku ikiangaliwa safari ya Tanzania kwenye Cameroon 2019 kwenye Fainali za 32 za Afcon.

 

Salum Mayanga

Kocha wa Taifa Stars, Salum Mayanga alikataa kuzungumza suala hilo akisema atafutwe baada ya wiki mbili.

Mayanga amepewa jukumu la kuandaa kikosi cha Taifa Stars kwa ajili ya mechi za kufuzu Afcon 2019 na mechi za awali zitaanza mapema Juni na nyingine Machi mwakani.

Mayanga atakuwa na jukumu pia la kuandaa kikosi cha wachezaji wa ndani kwa ajili ya mechi za kufuzu Fainali za CHAN zitakazofanyika Nairobi, Kenya baadaye Septemba.

 

Charles Boniface Mkwasa

Kocha wa zamani wa Taifa Stars ambaye alikuwemo katika kikosi cha Stars kilichofuzu Afcon mwaka 1980, anasema kinachotakiwa ni kujipanga vizuri na kupata mechi za maana.

“Kwanza inabidi tupate mapro wengi yaani wachezaji wengi waende kucheza soka la kulipwa nje ili kupata vitu vya ziada.

“Ukiangalia katika mashindano ya mwaka huu, timu nyingi zimebebwa na wachezaji wengi wanaocheza nje ya nchi zao, kitu ambacho sisi tunakikosa.

“Kingine nilichokiona kinachotuangusha huwa hatupati mechi nyingi za kujipima nguvu tena si mradi mechi, inatakiwa mechi zenye ubora za kuipa kipimo sahihi timu yetu ya Taifa.

“Tujipange vizuri, tuache siasa, tuweke mikakati ya maana na muhimu ni kuhakikisha tunashinda mechi zote za nyumbani katika mechi za kufuzu Afcon mwaka 2019 Cameroon,” anasema Mkwasa.

 

Zamoyoni Mogella

Mshambuliaji wa zamani wa Taifa Stars anasema kuna vitu vingi ambavyo wachezaji wa Tanzania wanatakiwa kujifunza lakini kubwa ni kujituma kwa asilimia 100.

“Fainali za Afcon 2017 ziwafungue wachezaji wa Tanzania. Ninaimani wameona jinsi wenzao walivyokuwa wakicheza kwa kujituma, na katika hali ya kujitoa muhanga

“Mfano mechi ya Senegal na Cameroon, ukiwaangalia Senegal wana wachezaji wenye majina lakini walipoteza mchezo kwa sababu Cameroon walijituma sana” anasema Mogella.

“Tatizo, kosa moja kubwa la nchi yetu tulitawaliwa na Uingereza na ndio maana tumekuwa na maneno mengi sana, matarajio makubwa lakini hakuna tunachokifanya

“Wachezaji wetu wanatakiwa kutengenezwa na kujengwa kisaikolojia. Lazima wajifunze kujitoa muhanga kwa ajili ya timu. Waichezee timu ya Taifa kwa moyo na si kama wamelazimishwa,” anasema Mogella.

 

Mohamed Rishard Adolf

Beki na kiungo wa zamani wa Taifa Stars, anasema tatizo kubwa linalotuangusha Watanzania ni kuchukulia vitu kirahisi rahisi.

“Kwa mfano, ukiangalia Fainali za Afcon mwaka huu, kwa jinsi tulivyoona, inabidi yatufungua macho na kuiangalia upya ligi yetu, tuangalie ubora wa wachezaji wetu, uwezo wa mchezaji mmoja mmoja na pia ari ya kupambana. Tumeona watu walivyokuwa wakipambana unaona kweli hapa soka imepigwa.

“Tujiulize kwanza je tunaweza kupambana? Hao jirani zetu tu Uganda, je tunawaweza? Maana ndiyo timu ya ukanda wetu kabla hatujaanza kujiuliza kwa hizo timu nyingine.

“Ukiangalia kuna tofauti kubwa ya maandalizi kwa timu yetu ukilinganisha na timu nyingine, sisi tunachukulia vitu kirahisi rahisi na wakati mwingine tunafanya mambo ya zimamoto. Ukweli tuna safari ndefu na ngumu ya kufika tunapotaka.

“Unapoangalia Afcon 2017 na kuona jinsi timu zinavyopambana, wachezaji wanavyopambana unabaki ukijiuliza njia yetu iko wapi? Wachezaji wetu wana ujanja wa kuzipenya ngome zinazojengwa na mapro? Nani anaweza kupenya ?” anasema Rishard.

Anasema kinachotakiwa ni kuundwa kwa kamati ya kuelekea Cameroon 2019, hii itakuwa na kazi ya kusaka fedha, wadhamini na kusimamia timu ikijumuishwa na mkono wa Serikali, hakika mambo yatakuwa tu, lakini kwa ubabaishaji huu mambo hayatakuwa.

 

Mbwana Samatta

Nahodha wa Taifa Stars anasema amekuwa akizishuhudia Fainali za Afcon 2017 na kwa jinsi alivyoziona kwamba endapo siasa zitawekwa kando wanaweza kufuzu fainali zijazo za 2019.

Samatta anayeichezea KRC Genk ya Ubelgiji anasema kundi walilopangwa safari hii sio gumu lakini kunahitajika maandalizi ya maana ili kuhakikisha malengo yao yanatimia, lakini kama tutaifunga timu kwa macho, hakuna maandalizi, hakuna mechi za majaribio za kutosha, itabakia vile vile kama zamani.

Anasema kinachotakiwa tu ni mikakati ya dhati katika mambo yanayohusu timu hiyo ili kuhakikisha Tanzania inafuzu fainali hizo baada ya kuzikosa za Gabon mwaka huu.

“Ukiangalia katika vipindi vyote tulivyopita sasa hivi hatujapangwa katika kundi gumu lakini mambo yanaweza kuwa magumu kwetu kama tutafanya maandalizi ya zimamoto.”

 

Mohammed Ibrahim ‘Mo’

Kiungo wa Taifa Stars, Mohammed Ibrahim anasema timu nyingi zilizoshiriki fainali za mwaka huu zimeonekana kubebwa na wachezaji wengi wanaocheza soka nje ya mataifa yao jambo ambalo Tanzania hatuna wachezaji wa kulipwa.

“Mashindano ya mwaka huu yanavutia kwani timu nyingi zimeonekana kujiandaa na nyingine zimeshangaza kwa kupata matokeo yasiyotarajiwa.

“Ila nilichojifunza ni kwamba wachezaji wa Tanzania tunatakiwa kutoka wengi na kwenda kucheza soka nje ya nchi ili kuisaidia timu yetu ya taifa kwani ukiangalia timu nyingi zimebebwa na wachezaji ambao kwa sehemu kubwa hawachezi ligi ya mataifa yao,” anasema Mo Ibrahim.

 

Haji Mwinyi

Beki wa Zanzibar Heroes anasema ugumu wa Tanzania kushindwa kufuzu mashindano kama hayo mara kwa mara ni kutokana na wachezaji wengi kukosa uzoefu.

“Nimeangalia fainali za Afcon 2017, nimejifunza mengi na kikubwa ni uzoefu na ndio unaotuangusha kwani ukiangalia wenzetu, timu zao zimejaza wachezaji wengi wanaocheza soka ya kulipwa nje ya nchi zao lakini sisi tunao wachache tu.

“Unajua wachezaji wakicheza nje ya mataifa yao wanapata uzoefu wa makocha tofauti lakini timu yetu ina wachezaji wengi tunaocheza hapa nchini na tunafundishwa na makocha wa aina ile ile, ligi ni ileile, wachezaji ni walewale tofauti na nje, unapata ladha ya tofauti,” anasema Haji

Anaongeza kusema: “Mechi nyingi tunakutana na timu ambazo zina uzoefu na zina wachezaji wengi wa kimataifa hapo ndipo tunapofeli…tunakuwa wanyonge, tunakuwa na woga na ile wanaita inferiority na hapo lazima tufungwe kwa kuwa hatujiamini.”

 

Saimon Msuva

Winga wa Taifa Stars anasema alichojifunza katika Fainali za Afcon 2017 kuwa mpira umebadilika sana kwani hata timu ndogo zimeonyesha ubora, walioshiriki mara ya kwanza wameonyesha wanaweza japokuwa walikosa uzoefu. “Fainali za mwaka huu zimeshangaza na kuonyesha kuwa kumbe mkijituma mnaweza, angalia jinsi timu ndogo zisizotarajiwa zimeweza kuonyesha soka la kiwango kikubwa kuliko zenye majina mfano Guinea Bissau.

“Tunachotakiwa kufanya sisi ni kupata maandalizi mazuri na maandalizi yenyewe ni mechi nyingi za kujipima nguvu, hatuna wachezaji wengi wa kulipwa lakini mechi nyingi zitatujengea kujiamini lakini vilevile mikakati bora isiyokuwa na siasa ndani yake,” anasema Msuva.

 

Jonas Mkude

Kiungo wa Taifa Stars, anasema amejifunza mengi. Timu zilizokuwa Gabon inaonekana wazi kuwa zimeandaliwa kwa kila hali kuhakikisha zinafanya vizuri.

“Kitu cha msingi na muhimu ni kuanza maandalizi mapema na kuweka malengo ya maana ili kuhakikisha Tanzania inafuzu katika mashindano hayo. Mashindano yale si lelemama, kila mmoja anakuwa amejikamilisha akijua kuwa anakwenda kucheza fainali.

“Hakuna kingine zaidi ya maandalizi ya uhakika tena ya mapema na mikakati madhubuti, nafikiri safari hii tukipambana vilivyo tutafuzu, mashindano magumu lakini kukubwa ni kwamba tuvuke hapa ndipo tutakapokata tiketi tujipande kwa umakini zaidi,” anasenma Mkude.