UCHAMBUZI: Mapambano makinikia ni ya Watanzania wote

Muktasari:

Mwenyezi Mungu amesikia kilio cha muda mrefu, akampa Rais Magufuli ujasiri na uthubutu wa kukabiliana na tatizo hili la ufujaji wa rasilimali za Taifa. Hakuna silaha muhimu atakayoihitaji zaidi ya umoja wa kitaifa.

Sakata la mikataba mibovu ya madini, hususan machimbo ya dhahabu lina historia ndefu. Baadhi ya walioshiriki, hawakutegemea wangekuwa miongoni mwa wanasiasa mashuhuri nchini.

Mwenyezi Mungu amesikia kilio cha muda mrefu, akampa Rais Magufuli ujasiri na uthubutu wa kukabiliana na tatizo hili la ufujaji wa rasilimali za Taifa. Hakuna silaha muhimu atakayoihitaji zaidi ya umoja wa kitaifa.

Watanzania wote bila kujali wanatoka vyama gani vya siasa, mkoa au kabila lipi, ni muhimu wakatumia busara na hekima walionayo kuchunga kauli na matendo yao ili wasije wakalifanya zoezi hili kuwa gumu zaidi kwa faida ya mahasimu wetu.

Ikumbukwe, vita hivi ni baina ya Watanzania kwa ujumla wetu na kampuni za nje ya nchi. Kwa mantiki hiyo, lazima tuwe na msimamo na kauli moja bila kusahau dhamira moja ya kuondokana na mikataba mibovu ya uchimbaji wa madini na rasilimali nyinginezo nchini.

Huu siyo wakati wa kutafuta sifa za nani ameanzisha mjadala huu wa kuwapo kwa mikataba mibovu ya madini. Huu siyo wakati wa kulaumu wengine, kwamba, ‘sisi’ tunaibua sakata la mikataba hii mibovu, tulipuuzwa, hatukusikilizwa au baadhi yetu walidhalilishwa. Wakati huo umepita.

Sasa hivi, Watanzania wote tunatakiwa tuungane kwa pamoja kuhakikisha nchi inaondokana na mikataba yote mibovu. Kwamba, tulipofika sasa, basi yatosha. Kama tulipigwa basi ilikuwa kwa sababu ya ujinga wetu. Lakini kuanzia sasa, mikataba mibovu haitaendelea tena.

Kitendo cha Rais Magufuli kustuka kuhusu udanganyifu unaofanyw akwenye usafirishaji wa mchanga wa dhahabu, siyo jambo rahisi kulifanya kiongozi yeyote wa serikalini. Halikufanywa na viongozi waliopita, lakini sasa limewezekana.

Watanzania kutoka vyama vyote vya siasa lazima waungane pamoja ili kushinda hatua hii ya kwanza ya vita kubwa na ngumu ya kiuchumi ambayo itachukua muda mrefu kuifanikisha. Na watanzania lazima wawe tayari kwa lolote litakalojitokeza mbele ya safari. Lakini umoja wetu ndiyo utakao tuokoa, siyo tofauti za kiitikadi.

Tukimhakikishia hilo Rais, kwa anachokifanya sasa, atapata nguvu zaidi ya kupambana. Huu siyo wakati wa kujutia kwa kiwango chochote cha madini kilichokwisha vunwa katika miaka ya nyuma.

Haitatusaidia sana. Ni wakati wa kuhakiksha mikataba yote mibovu inavunjwa, na mikataba mipya yenye maslahi kwa pande zote mbili, inazingatiwa kwa ridhaa ya kila upande.

Atakayeonyesha kutofautiana au kutokukubaliana na msimamo wetu, awe huru kuchukua kila kilicho chake akawekeze mahali pengine popote ambako atakubaliana na sera zake.

Watanzania wanapenda na wanaheshimu ushirikiano wa kimataifa. Kila jitihada zinafanyika kuvutia wawekezaji binafsi kutoka nje ya nchi. Lakini uwekezaji au ushirikiano huo lazima uwe na maslahi na wa ridhaa za pande zote mbili.

Zimbabwe ilikuwa na utajiri mkubwa wa dhahabu miaka ya 1320 lakini ilivunwa kwa fujo na kusafirishwa na watumwa kupitia bandari ya Sofala (Beira), hadi Kilwa Kisiwani, kwa wakati huo ukiwa ndiyo mji mkubwa wa kibiashara kuliko miji Pwani ya Afrika Mashariki. Kutoka hapo, dhahabu ya Zimbabwe ilisafirishwa kwenda Mashariki ya Kati, India na China.

Hivi sasa imebakia historia ambayo hawaijui. Kilwa Kisiwani kwa sasa haijulikani kimataifa na Zimbabwe haina dhahabu tena.

Tusipo muunga mkono Rais Magufuli katika hili, Tanzania itabakia kuwa historia tu katika utajiri wa dhahabu duniani.

Miongoni mwa nyakati muhimu za Watanzania kuonyesha mshikamano, huu nao umo.

Mchambuzi anapatikana kwa namba: 0683 555 124