BIASHARA LEO : Ujasiriamali wa China una funzo kubwa nchini

Muktasari:

  • China imekimbia haraka na kuwa miongoni mwa nchi kubwa zenye nguvu duniani kiuchumi ndani ya muda mfupi, kutokana na kuruhusu wajasiriamali kuwekeza kwenye utafiti na ubunifu wa mtu mmoja mmoja ambao baadaye unazalisha jamii ya watu wenye uchumi unaoruhusu kuvuka mipaka ya nchi.

Uchumi wa China kwa kiasi kikubwa umetokana na mchango wa sekta binafsi hasa wananchi wengi wanaofanya shughuli ndogondogo ambazo huzaa kampuni kubwa zinazotoa huduma na kuzalisha bidhaa duniani kote.

China imekimbia haraka na kuwa miongoni mwa nchi kubwa zenye nguvu duniani kiuchumi ndani ya muda mfupi, kutokana na kuruhusu wajasiriamali kuwekeza kwenye utafiti na ubunifu wa mtu mmoja mmoja ambao baadaye unazalisha jamii ya watu wenye uchumi unaoruhusu kuvuka mipaka ya nchi.

China kwa sasa ndiyo nchi yenye viwanda vikubwa vya kuzalisha nguo nzuri, kampuni kubwa za ukandarasi wa miundombinu ya reli, barabara na majengo yenye ubora na mvuto mkubwa.

Licha ya kukimbilia kununua bidhaa na kuzileta nchini, Tanzania ina vitu vingi vya kujifunza kutoka China. Urafiki uliopo uwe fursa ya kufungua macho na kujifunza. Historia ya kiuchumi ya nchi hiyo inatufundisha mambo mengi ambayo ni chachu ya ujasiriamali na biashara zenye nguvu kwa dunia ya sasa hivi.

China imewekeza kwa vijana ambao ni mahiri katika ubunifu na uvumbuzi wa teknolojia, utendaji na uamuzi. Nchi hiyo imefanikiwa kwa kasi kubwa kwa sababu vijana kutoka miji midogo pia wamekuwa wakipata nafasi ya kujaribu na kufanya mambo mazuri wanayomudu kwa uhakika.

Miji ya Beijing, Shenzhen, Shanghai haizuii watu wengine kutoka miji midogo kukua vizuri na kuwa wamiliki wa mitaji na ubunifu. Dhana ya ujasiriamali nchini China inaenda mbali zaidi kwani wajasiriamali hawafikirii kupata faida pekee, bali namna biashara yao inavyoweza kusimama bila kutetereka kwa muda mrefu kwa kuzingatia sheria zilizopo.

Wachina wanafanya biashara ambazo masoko yake yapo ndani na nje ya China. Mtazamo wao kwa soko la nje umekuwa ukiongezeka kila siku, hivyo wajasiriammali hutengeneza bidhaa zinazokidhi mahitaji yake na kutengeneza faida kubwa zaidi.

Angalia magari ya abiria kutoka kampuni za Yutong, Zhontong, Higer au King Long yametengenezwa mahsusi kwa Bara la Afrika, hivyo wanahakikisha lazima bidhaa ifike sokoni kwa wakati.

Muunganiko mzuri wa viwanda vikubwa na wafanyakazi wadogo, kupitia ushirikiano wa Serikali na wajasiriamali wametengeneza uhusiano mzuri wa kufahamu wanategemeana kuifanya nchi na biashara kuwa bora kadri inavyotakiwa.

Ni rahisi kwa Wachina kushirikishana kwa kupeana teknolojia, mtandao wa kuvuka nje ya mipaka kutafuta malighafi na masoko ili kuhakikisha mambo yanakwenda sawa na uchumi unaimarika.

Taifa hilo lina maeneo mahsusi ya biashara, viwanda na miundombinu mizuri ya usafirishaji, majengo na uhakika wa upatikanaji wa malighafi. Maeneo hayo yanawahakikishia wajasiriamali usalama wa wa mali na ofisi zao, hivyo kutekeleza mipango yao ya maendeleo.

Upo utulivu na ubobezi kwenye bidhaa na huduma moja miongoni mwa wajasiriamali wengi ambao wanafahamu umuhimu wa kutofautisha na kuwekeza nguvu zao kwenye sekta moja.

Kutokana na ukubwa wa teknolojia na ubunifu wao ni rahisi kwao kusimamia eneo moja la uzalishaji na kufanikisha kuyateka masoko ya nje. Tunanunua simu na nguo nyingi kutoka china kwa sababu ya ukweli kuwa walioanza kwenye ufundi wa vifaa vya kielektroniki wamewekeza eneo hilo kwa nguvu na kukua mpaka kupata kampuni kubwa.

Kuanzia miaka ya 1990 wameibuka wafanyabiashara wakubwa kama Jack Ma au Alibaba ambao ni zao la mipango mizuri ya Serikali na wadau wa ujasiriamali. Watanzania tuitumie China kujifunza kuboresha shughuli zetu ili kuongeza thamani ya bidhaa na huduma zetu.