Ukitokea mtikisiko wa uchumi nchini, wataalamu walaumiwe

Muktasari:

Mijadala mingi inaonyesha kuwapo na dalili za mtikisiko wa uchumi katika ngazi mbalimbali. Watu binafsi, kaya na taasisi za umma au kampuni, zote zinalalamika juu ya hali ngumu ya uchumi lakini baadhi wanaopinga kuwa hamna mtikisiko wa uchumi.

Kusitishwa kwa mikopo na taasisi za fedha, kuuzwa kwa mahoteli, mabasi na kufilisika kwa baadhi ya kampuni nchini ni miongoni mwa mambo makuu yanaoongoza mjadala wa uchumi na biashara kwa nusu ya mwisho ya mwaka 2016 juu ya hali ya uchumi nchini.

Mijadala mingi inaonyesha kuwapo na dalili za mtikisiko wa uchumi katika ngazi mbalimbali. Watu binafsi, kaya na taasisi za umma au kampuni, zote zinalalamika juu ya hali ngumu ya uchumi lakini baadhi wanaopinga kuwa hamna mtikisiko wa uchumi.

Wakati takwimu za taasisi za Serikali mfano Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zikionyesha kuimarika kwa uchumi, sekta binafsi ina walalamikaji wengi ambao hawaridhishwi na mwenendo wa uchumi hasa kutokana na kuadimika kwa fedha.

Ili kujua kama kuna mtikisiko wa uchumi ni vizuri kufahamu maana na vyanzo vya suala hilo. Makala haya, kwa kuzingatia utafiti uliofanywa na mwandishi tangu mwaka 2008, unaangalia kwa kina mitikisiko ya uchumi iliyowahi kutokea duniani hasa ule wa mwaka 2008.

Mtikisiko wa uchumi ni hali ambayo mambo makuu na ya msingi katika uchumi yanakuwa hayaendi vizuri kama inavyotakiwa ambayo yanajumuisha uzalishaji bidhaa na huduma, mauzo na faida katika biashara, uwekezaji katika sekta mbalimbali, ajira, upatikanaji wa mikopo na kukua kwa uchumi.

 

Dalili

Zipo dalili za mtikisiko wa uchumi duniani ambazo hujirudia tangu ule wa kwanza wa miaka ya 1930. Zilionekana kwenye mtikisiko wa uchumi wa Asia katika miaka ya 1970 na katika mtikisiko mkubwa wa uchumi duniani wa mwaka 2008.

Zilinekana pia kwenye mtikisiko wa uchumi wa nchi za Umoja wa Ulaya zinazotumia sarafu ya Euro mwaka 2010. Dalili ambazo zimekuwa zikijirudiarudia wakati wa mitikisiko ya uchumi ni nyingi. Hizi ni pamoja na kutokuwepo na fedha katika mzunguko katika wingi uliizoeleka.

Pia, masoko na taasisi za fedha kama vile benki yanakuwa hayana fedha za kutosha kukidhi mahitaji ya wateja wao hasa mikopo kwa ajili ya mitaji ya kufanyia biashara.

Kutokana na kutokuwepo kwa fedha za kutosha katika mfumo wa uchumi kunakuwapo kudorora na kudhoofu kwa shughuli za uchumi na biashara. Shughuli hizi ni pamoja na utafiti na maendeleo; uzalishaji mali na huduma, usafirishaji wa huduma na bidhaa kwa njia mbalimbali, uhifadhi katika maghala na utumiaji wa bidhaa na huduma kwa matumizi ya nyumbani au kuzalishia bidhaa nyingine.

Dalili nyingine ni mkwamo wa mikopo, kupotea kwa fedha na hali ngumu ya kibiashara. Kama sehemu ya viashiria vya mtikiso wa uchumi, baadhi ya kampuni huelekea kufilisika na kuuza mali zake.

Dalili za mtikisiko wa uchumi huweza kuonekana muda mrefu kabla haujatokea. Ikumbukwe, mtikisiko wa uchumi unaweza kuonekana, siyo kwenye sekta ya fedha tu, bali uchumi mzima pia.

 

Mtikisiko wa 2008

Mtikisiko wa uchumi duniani mwaka 2008 ulianza kuonekana waziwazi katika juma la pili la Septemba mwaka 2008. Huu ni wakati sekta ya fedha na benki nchini Marekani iliyumba.

Baadhi ya benki zilianguka na nyingine ziliwekwa chini ya uangalizi wa Serikali. Baadhi ya benki na taasisi kubwa za fedha zilizoathirika ni pamoja na Goldman Sachs, Morgan Stanley, J. P Morgan, Bank of America, Merrill Lynch, Citigroup, Wells Fargo, Bank of New York Mellon na State Street. Sababu za msingi zilizosababisha mtikisiko huo wa uchumi mwaka 2008 ni pamoja na wasiwasi kuhusu uimara wa kifedha wa benki kubwa za biashara na zilizokuwa zinaongo Marekani na Ulaya.

Kulikuwepo pia wasiwasi kuhusu uimara wa kifedha wa kampuni kubwa za bima na benki zitoazo dhamana. Kushindwa kufanya kazi kwa taasisi kubwa za fedha nchini Marekani kulikuwa na kusababisha mtikisiko.

Taasisi za fedha Ulaya na masoko kadhaa ya mitaji yalidondoka na kukawepo anguko la thamani ya hisa katika masoko hayo. Pia thamani za bidhaa kama vile mafuta, nafaka na madini zilianza kushuka duniani kote. Hii ni kwa sababu ya kushuka kwa uhitaji (urari) wa bidhaa hizi sokoni.

Kudondoka na kufilisika kwa taasisi kubwa ya fedha ya Lehman Brothers, Septemba 2008 ilikuwa ni alama kuu ya dunia kuingia katika mtikisiko wa uchumi.

Kwa ujumla, kulionekana kukosekana kwa udhibiti wa sekta ya fedha na benki hasa Marekani hivyo kuwa sababu kubwa ya kutokea kwa mtikisiko wa uchumi duniani mwaka huo, 2008.

Vyanzo vya mitikisiko

Kimsingi mitikisiko ya uchumi husababishwa na mambo mengi yanayoendana kwa karibu sana. Ni vigumu na pengine siyo sahihi kutoa sababu moja inayoweza kusababisha mtikisiko wa uchumi.

Tafiti zinaonyesha, kati ya vyanzo vya mitikisiko ya uchumi ni benki na taasisi nyingine za fedha kutoa mikopo kwa watu na taasisi zisizokuwa na sifa ya kukopa. Hawa ni wakopaji wasioweza kulipa mikopo na riba yake pale inapotakiwa kufanya hivyo.

Hii inaweza kusababishwa na usimamizi mdogo wa vyombo vya fedha kama vile benki. Ikumbukwe kuwa usimamizi wa masuala ya fedha na benki katika nchi ni jukumu la mamlaka kuu za fedha ambazo mara nyingi huwa ni Benki Kuu ya Serikali husika.

Sekta ya fedha ikiwa na udhibiti mdogo na kuachwa huru kupita kiasi huweza kusababisha wasiostahili kupata mikopo kunufaika nayo hivyo kuleta changamoto za kuzirejesha pale inapohitajika.

Ikumbukwe, benki hukopesha fedha za watu, waliotunza akiba zao huko ili kutengeneza faida kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli za kila siku hivyo kuwakopesha watu wasio na sifa watakaoshindwa kuzirejesha ni mwanzo wa kuyumbisha uchumi.

 

Tanzania

Kadri ya taarifa na mazungumzo ya watu, taasisi na kampuni kadhaa kwa upande mmoja na tafiti kuhusu mtikisiko wa uchumi kwa upande mwingine inaonekana kuna dalili za mtikisiko wa uchumi Tanzania.

Dalili hizi ni pamoja na taasisi za fedha kuwa katika wakati mgumu kama ilivyoripotiwa kwa nyakati tofauti, kuwapo uhaba wa fedha katika mzunguko, kushuka na kufungwa kwa baadhi ya shughuli za kibiashara.

Kufilisika kwa Benki ya Twiga Bancorp ambayo sasa inatafutiwa wawekezaji wapya na kusitishwa kwa mikopo kutoka taasisi hizo ni suala linalohitaji umakini kulishughulikia.

Hivi karibuni tumesikia benki zikiliambia Shirikisho la wenye Viwanda (CTI) kwamba zijibane au kutafuta vyanzo vingine vya mitaji kwani mikopo haiwezi kupata kama ilivyokuwa awali.

Hata hivyo dalili hizi ni viashiria na siyo lazima kuwapo kwa mtikisiko wenyewe. Hata hivyo havipaswi kupuuzwa wala kupewa majibu rahisi na kejeli. Majibu rahisi kwa maswali magumu hayatamsaidia mwanafunzi kufaulu.

 

Cha kufanya

Kuna haja ya kufanyia kazi viashiria vya mtikisiko wa uchumi vilivyopo bila kuchelewa. Utaalamu wa namna ya kuzuia mtikisiko upo na ni vizuri ukatumika.

Wakati wa mtikisiko wa 2008 wataalamu walilaumiwa na kuulizwa walikuwa wapi hadi kuruhusu mtikisiko utokee. Itakuwa aibu na tutakuwa hatujifunzi kama viashiria vilivyopo vitaruhusiwa kusababisha mtikisiko kamili.