Vifo vya kina mama wakati wa kujifungua vyaongezeka nchini

Muktasari:

Msiba huo unasababishwa na wanawake wanaofariki dunia wakati au miezi michache baada ya kujifungua; hivi ni vifo vya uzazi.

Kitendo kinachotarajiwa kuwa cha furaha katika jamii, kimeendelea kuwa ni msiba kwa familia zaidi ya 9,000 kila mwaka zinazopoteza akina mama.

Msiba huo unasababishwa na wanawake wanaofariki dunia wakati au miezi michache baada ya kujifungua; hivi ni vifo vya uzazi.

Ripoti mpya ya jamii na afya (DHS) ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa mwaka 2015/16 inaonyesha kuna vifo 556 vya uzazi katika kila vizazi hai 100,000.

Kiwango hiki ni kikubwa kuliko kile cha mwaka 2012 ambapo wanawake 432 walikufa kwa uzazi. Hata hivyo idadi hiyo ni ndogo ukilinganisha na ya mwaka 2004/05 iliyoonyesha wanawake 578 hupoteza maisha. Mwaka 2010/11, ripoti ilionyesha kuna vifo 454. Ripoti hii ni ya sita kufanyika nchini, ya kwanza ilifanyika mwaka 1991/92.

Vifo vya uzazi vinasababishwa na mambo kadhaa ikiwamo kuzaa katika umri mdogo na ukosefu wa huduma za afya zenye kiwango kinachostahili kimataifa, vifaa tiba na utoaji holela wa mimba.

Rais wa Shirika la Afya la Pathfinder, Louis Quiam, anasema ni vyema wanawake wakapewa nafasi ya kupanga uzazi kwani kwa kufanya hivyo wanaweza kujihakikishia usalama na kuepuka vifo wakati wa kujifungua.

“Kujifungua ni jambo la furaha lakini kama vijana wasipopata nafasi ya kupanga uzazi, watapata mimba za utotoni na kuzaa katika umri mdogo hivyo kuchangia vifo vya uzazi,” anasema.

Takwimu za DHS zinaonyesha kuwa asilimia 27 ya wasichana wenye umri kati ya miaka 15 na19 tayari wameanza kuzaa. Hiyo ina maana asilimia 27 ya vijana wadogo wapo katika hatari ya kupoteza maisha wakati wa kujifungua.

“Tatizo ni upatikanaji wa njia za kuzuia mimba, hii ingezuia vifo hivyo,” anasema Quiam. Kingine kinachoelezwa na Quiam ni kutumia njia za uzazi wa mpango ili kuepuka mimba zisizotarajiwa.

Wataalamu wa afya wanasema watoto wanapaswa kupishana walau miezi 36 au miaka mitatu, kitendo ambacho kitapunguza hatari ya vifo vya mama na mtoto. Hivi sasa, nusu ya watoto nchini hupishana kwa wastani wa chini ya miezi 35.

Kwa mfano, kwa sasa mwanamke wa Kitanzania anapata wastani wa watoto 5.2 katika maisha yake. Mwakilishi wa Pathfinder nchini, Kudrati Mustapha anasema mimba za utotoni ni chanzo cha vifo vingi vya uzazi.

“Kama wangekuwa wanatumia njia za kupanga uzazi huenda vifo hivyo vingepungua,” anasema.

Anasema Pathfinder linatoa huduma za afya na vifaa tiba ili kupunguza hatari ya mama wajawazito kufariki wakati wa kujifungua.

“Tunatoa elimu ya uzazi kwa vijana, kwa mfano tumeanzisha klabu mkoani Kigoma zinazojumuisha vijana waliozaa katika umri mdogo kurudi shule na wengine kujizuia na mimba hizo,” anasema.

Mustafa anasema njia za uzazi wa mpango ni mbinu muhimu zaidi katika kupunguza vifo hivyo. “Kitendo cha wanawake 9,000 kufariki kila mwaka wakati wa kujifungua ni zaidi ya janga,” anasema.

Anasema ingekuwa ni mabasi yameua watu hao kwa ajali za barabarani ingetangazwa hali ya hatari katika vyombo vya habari na Serikali ingechukua hatua kali lakini hili la vifo linaonekana la kawaida. Wakati Shirika la Afya Duniani (WHO) likionyesha mimba za utotoni ndicho chanzo kingine kinachosababisha vifo hivyo ripoti ya DHS inaonyesha kuwa asilimia 32 ya watoto wa kike vijijini walipata mimba.

Asilimia 19 ya watoto wa kike mijini walipata mimba hizo na Zanzibar ni asilimia nane.

Hata hivyo, mimba hizo zilipungua kuanzia mwaka 1992 ambapo asilimia 29 ya watoto wa kike walipata mimba za kwanza hadi mwaka 2010 kulipokuwa na asilimia 23. Lakini kwa mwaka 2015/16 idadi imeongezeka na kufikia asilimia 27.

WHO inaeleza ongezeko hili linaweza kuirudisha nyuma Tanzania katika jitihada zake za kupunguza vifo wakati wa kujifungua.

Mganga Mkuu wa Kituo cha Afya cha Round Table cha Mbagala, Dar es Salaam, Dk Lugano Mtafya anasema kituo hicho kinatoa elimu ya uzazi wa mpango kwa wanawake kama njia ya kuzuia vifo hivyo.

“Tunatoa elimu kuhusu mimba za utotoni, elimu kwa mwanamke ambaye mimba imeharibika au waliotoa mimba,” anasema.

Anasema mimba zisizotarajiwa zinasababisha wanawake kutoa mimba kwa njia hatarishi na kuongeza vifo vya wajawazito nchini. “Kwa siku, kituo chetu kinapokea kati ya wanawake 40 hadi 100 wanaohitaji huduma za uzazi wa mpango,” anasema.

Pamoja na hayo ili kupunguza vifo hivyo, kituo hicho kinatoa elimu ya uzazi wa mpango kwa vijana walio katika balehe.

Kuhusu dhana na fikra potofu ya madhara kutokana na matumizi ya njia za uzazi wa mpango, Dk Mtafya anapinga na kusema faida ni nyingi kuliko wengi wanavyofikiri.

“Wenye fikra kuwa zina madhara waziondoe mara moja. Kuna njia mbalimbali ambazo mtu anaweza kuchagua; sindano, kitanzi, vidonge, mipira ya kiume na kike au vijiti,” anasema.

Hata hivyo Serikali inaendelea na jitihada za kukabiliana na tatizo hilo. Mei mwaka jana, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ilisema inakusudia kutoa taarifa ya wanawake wanaofariki kutokana na matatizo ya uzazi kila baada ya miezi mitatu ili kukabiliana na tatizo hilo.

Waziri wa wizara hiyo, Ummy Mwalimu anasema: “Nimeamua kuhakikisha kuwa wanawake wanapiga hatua na kuthaminiwa katika jamii, nitaanza kutoa ripoti ya robo mwaka kwa kila halmashauri kuhusu wanawake wanaofariki kutokana na matatizo ya uzazi.”

Ameeleza kuwa, katika uteuzi atakaoufanya kwenye bodi zilizo chini ya wizara yake, atahakikisha kuwa asilimia 30 ya wajumbe ni wanawake.

Baadhi ya taasisi zilizo chini ya wizara hiyo ni Bohari ya Dawa (MSD), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na Bodi ya Wafamasia.