Vyama vinapoendeshwa kwa nidhamu ya kijeshi

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akisikiliza risala ya vijana wa kikosi cha ulinzi cha chama hicho katika moja ya matukio ya kisiasa mwaka 2015

Muktasari:

Nyalandu, ambaye alikuwa Waziri wa Maliasili na Utalii katika Serikali ya Awamu ya Nne, pia ameachia nafasi yake ya ubunge wa Jimbo la Singida Kaskazini. Sambamba na kujivua nyadhifa pia alitangaza kuomba kujiunga na Chadema.

Wiki hii taifa lilishtushwa na kuzizima kwa habari za Lazaro Nyalandu kujiuzulu ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM pamoja na nafasi zake zote ndani ya chama hicho kuanzia Oktoba 30, 2017.

Nyalandu, ambaye alikuwa Waziri wa Maliasili na Utalii katika Serikali ya Awamu ya Nne, pia ameachia nafasi yake ya ubunge wa Jimbo la Singida Kaskazini. Sambamba na kujivua nyadhifa pia alitangaza kuomba kujiunga na Chadema.

Lazaro kaeleza mengi kuhusu sababu za kujitoa CCM na kujiuzulu nyadhifa zake, lakini tunaweza kueleza kujitoa kwake kwa maneno machache kuwa Nyalandu ametofautiana mawazo na uongozi wa chama chake.

Kitendo cha Nyalandu kujiuzulu kinanipeleka kwenye hoja yangu ya leo: Je, hivi ni lazima kweli watu ndani ya chama kimoja wakitofautiana mawazo na mitazamo, basi kundi moja lijitoe au lifukuzwe? Je, ni wakuu wa vyama vya siasa pekee ndiyo wenye haki ya kufikiri na kutoa maoni yao? Je, hakuna uhuru wa kufikiri vinginevyo kwa wanachama wengine?

Naandika makala haya kwa dhana kuwa Nyalandu aliwekwa katika mazingira magumu ya kiuadui ambayo yalisababisha ajiuzulu. Ingekuwa si hivyo nimehoji pia, kwa nini wanachama wenye mawazo tofauti wasipambane ndani ya chama kusukuma ajenda zao badala ya kujitoa?

Siulizi maswali haya kwa sababu ya suala la Nyalandu pekee, bali ni hoja ninayoiibua ifikiriwe na vyama na wanasiasa wote kwa sababu Nyalandu si mtu wa kwanza kulazimika kuachana na chama chake ama kwa kujitoa au kufukuzwa.

Kabla ya Nyalandu walikuwapo wakina Profesa Abdallah Safari aliyetoa CUF na kujiunga na Chadema, Hamad Rashid (aliyeondoka CUF na wenzake na kujiunga na ADC), na Zitto Kabwe aliyetoka Chadema na wenzake na kujiunga na ACT- Wazalendo.

Hawa nao waliondoka kwa sababu walikuwa na mawazo tofauti na viongozi wao. Walidhani, kama alivyodhani Nyalandu, kuwa vyama vyao vilipoteza dira. Kwa hiyo, kwa kanuni za Tanzania, ukiwa kwenye chama ukawa na mawazo tofauti, ni lazima utoke.

Ndiyo maana, kila palipoibuka tofauti ya mawazo, badala ya tofauti hizo kuchukuliwa kwa mtazamo chanya, kuwa ndiyo afya ya chama; ilikuwa kinyume. Tofauti ya mawazo iligeuzwa kuwa mgogoro ambao ili uishe lazima kundi moja litoke.

Hakuna siasa bila mijadala

Hakuna chama cha siasa kinachostahili kuitwa kwa jina hilo la chama cha siasa kama hakuna tofauti ya mawazo na kuwepo mijadala ya masuala ya kimaendeleo katika kuunda sera mtakazouza kwa wananchi.

Ni kwa sababu hii, inaniwia vigumu kuelewa mantiki ya kuwa na vyama bila uwepo wa uhuru wa fikra kwa wanachama, ikizingatiwa kuwa vyama hivyo vipo katika nchi ambayo inatajwa kufuata siasa za kidemokrasia, tena katika karne ya 21.

Moja kati ya kanuni muhimu za demokrasia ni uwepo wa uhuru wa fikra na uhuru wa kujieleza. Mijadala kuhusu masuala mbalimbali ni muhimu sana sio tu katika siasa bali katika kila sekta ya maendeleo ya nchi kwa jumla.

Ni kwa kutambua umuhimu wa kupata mawazo tofauti ndiyo maana kila Serikali inapotunga sera, sheria au kanuni, wadau mara nyingi hudai nao washirikishwe. Na Serikali hukubali. Ni wazi wadau hushirikishwa kwa lengo la kukusanya maoni tofauti, yanayokinzana, ikitegemewa kuwa kwa nafasi, majukumu na uzoefu wa kila kundi la wadau, watakuwa na uelewa fulani ambao kundi jingine halina.

Mijadala huchochea ushindani wa akili ambazo ndiyo zinazalisha mawazo. Taifa au taasisi isiyo na mijadala ni mfu. Je, vyama vya siasa vinataka kufa kifikra? Au labda viongozi wanataka kuendesha vyama kama jeshi, wakuu wanatoa amri wengine wanatekeleza.

Ukifuatilia baadhi ya migogoro iliyopelekea baadhi ya wanachama kufukuzwa, hususan katika vyama vya upinzani, utagundua kuwa kosa pekee waliofanya ni kuamini kuwa vyama vyao vinahitaji mabadiliko makubwa ya kisera au kiuongozi. Hilo linakuwaje ni kosa katika chama chenye demokrasia?

Mwisho wa siku unagundua kuwa watu wanafukuzwa katika vyama si kwa sababu ya maslahi ya chama bali kulinda viongozi waliopo, wasiopenda kukosolewa. Mara nyingi katika kuhalalisha hatua za kupambana na washindani ndani ya chama hutokea wale viongozi madikteta wa vyama kwa kuhofia kupokwa madaraka, hukimbilia kuwapakazia wakosoaji kuwa ni ‘wasaliti’ na kudai kuwa wana ushahidi wa kiintelijinsia kuwa anashirikiana na chama tawala. jiulize, Profesa Safari alikuwa msaliti CUF aliyekihujumu chama lakini ni huyo huyo ambaye alipokewa Chadema. Kwa kinachoitwa ‘inteligensia’ kali ya Chadema, wameshindwa kujua hilo? Au ndiyo ukitaka kumuua mbwa, mpe jina baya kwanza?

CCM na mwelekeo mpya

Nimekuwa nikiamini kuwa CCM ni chama chenye demokrasia imara, si tu wakati wa uchaguzi hata muda mwingine. Kabla ya uchaguzi wa 2015, tofauti za fikra zilizodhihiri kupitia makundi ziliichangamsha CCM, kiasi kwamba baadhi ya watu walidhani chama kingegawanyika.

Kuelekea uchaguzi, kulikuwa na ukosoaji mkali dhidi ya Rais Jakaya Kikwete. Kikwete aliitwa kila aina ya majina na baadhi ya watu: dhaifu, fisadi, mswahili…. lakini, licha ya tofauti hizo, maamuzi yalifanyika kupitia mifumo, sera, sheria na kanuni za chama, kukawa na washindi na walioshindwa.

Kwa kiasi kikubwa, walioamua kujitoa, haikuwa kwa sababu walitimuliwa bali kwa ni sababu walitaka kwenda kutafuta nafasi ya kugombea katika vyama vingine.

Sasa, hali inaonekana kubadilika. Tayari zipo dalili za CCM kupoteza demokrasia ya ndani ya chama. Yale ambayo tumekuwa tukiyaona wakitendewa wapinzani, yaani kukandamizwa kwa uhuru wa kutoa mawazo, yanajitokeza ndani ya CCM sasa.

Baada ya kuondoka Nyalandu, baadhi ya wana CCM tayari wameanza kutaja majina ya watu wengine ambao wanadhani nao wangepaswa kuondoka kwa sababu tu wana mawazo tofauti, jambo ambalo linatishia kuua demokrasia hususan uhuru wa fikra ndani ya CCM.

Kama hali hii itaendelea, tusishangae CCM ikarudi nyuma hadi enzi zile za ‘Zidumu fikra za Mwenyekiti’.

Kurejea kwa enzi zile ni jambo la kuogopwa kwa sababu tushaipitia na kuona madhara yake. Mwalimu Nyerere, labda kwa nia nzuri tu, alitaka kutekeleza ndoto na mradi wake wa ujamaa kwa Tanzania. Hata hivyo, kwa sababu ndoto zake hazikupitia michakato ya ushindani huru wa mawazo; zilishindwa.

Mwendelezo wa watu kufukuzwa kutoka katika vyama au kushinikizwa mpaka wanajitoa, ni dalili ya kuendelea kuporomoka kwa demokrasia ndani ya vyama vya siasa. Viongozi wanataka wanachosema kiwe ndio ukweli pekee, kusiwe na mawazo mbadala.

Vyama vingi vya siasa Tanzania vinapenda demokrasia tu katika siasa za kitaifa zinazopambanisha vyama, lakini havitaki demokrasia ndani ya vyama vyao. Kwa mfano, katika historia ya vyama vingi tumeona mara nyingi vyama vinalalamikia Serikali kukandamiza uhuru wao wa kisiasa lakini wakati huohuo, vyama hivyo hivyo vinavyolalamika vinakandamiza uhuru wa fikra na mawazo wa wanachama wake.

Ifike wakati tutofautishe muundo wa utendaji wa vyama vya siasa na taasisi nyingine. Kwa ilivyo sasa, vyama vinaendeshwa kama jeshi. Amri moja. Umefika wakati sasa, turudi darasani na kusoma upya ni maana ya chama cha siasa hasa katika muktadha wa mifumo ya siasa za kidemokrasia.