WAKALI WA NJE- Festi 11 ya mapro hii hapa

Muktasari:

  • Kabla ya Ligi Kuu kuanza mapema Agosti, tulishuhudia timu zikifanya usajili ambao ulihusisha wachezaji wazawa na wale wa kigeni kwa ajili ya kuimarisha vikosi vyao.

Ligi Kuu soka inaendelea baada ya kusimama kupisha mechi za kimataifa za kirafiki pamoja na zile za kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia.

Kabla ya Ligi Kuu kuanza mapema Agosti, tulishuhudia timu zikifanya usajili ambao ulihusisha wachezaji wazawa na wale wa kigeni kwa ajili ya kuimarisha vikosi vyao.

Hata hivyo usajili wa wachezaji wa kigeni umekuwa ukilalamikiwa na wadau wa soka kwa madai kwamba wamekuwa hawathibitishi thamani yao wanapopewa nafasi.

Kwa mtazamo wa wadau hao, mchezaji wa kigeni anatakiwa awe na kiwango bora zaidi ya wazawa yota ili asajiliwe na iwapo anakuwa na uwezo sawa au amezidiwa na wazawa, hafai kuendelea kuwepo.

“Timu zetu zimekuwa zinapenda kusajili wachezaji wa kigeni, lakini wengi hawana uwezo mkubwa kulinganisha na wazawa wanaocheza kwenye nafasi zao na wamekuwa wakipokea fedha za bure tu,” anasema kocha wa Dodoma FC, Jamhuri Kihwelu.

Unajua sifa kubwa ya mchezaji wa kigeni ni kwamba anapaswa aonyeshe uwezo wa ziada ili aonyeshe utofauti wake na wazawa lakini inapokuwa kingine, ni vyema klabu zetu zikawapa nafasi wachezaji wazawa tu,” anasema kocha John Tegete.

Hata hivyo, katika mechi za Ligi Kuu zinazoendelea hadi sasa, wapo nyota wa kigeni waliofanya vizuri ambao wanaweza kuunda kikosi kikali ambacho kinaweza kuifunga klabu yoyote nchini.

Pia kinaweza kuwa mazoezi mazuri kwa timu ya taifa ya Tanzania Bara inayojiandaa na Kombe la Chalenji.

Festi 11 ya mapro wanaochezea timu zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu ni hawa wafuatao.

Razack Abalora- Azam FC

Hapana shaka yoyote kwamba Abalora ndiye kipa anayefanya vizuri kwenye Ligi Kuu msimu huu kwa sasa na amekuwa chanzo cha ngome imara ya Azam FC ambayo imekuwa ngumu kwa washambuliaji wa timu pinzani kuipenya.

Hadi sasa, Abalora ambaye Azam FC imemsajili akitokea klabu ya WAFA inayoshiriki Ligi Kuu ya Ghana, amefungwa mabao mawili tu huku akiwa amecheza mechi nane bila kuruhusu nyavu zake kutikiswa.

Michael Rusheshangoga- Singida United

Huyu ni beki wa kulia wa Singida United aliyesajiliwa akitokea APR inayoshiriki Ligi Kuu nchini Rwanda.

Tangu aliposajiliwa amethibitisha ubora wake kwa kuwa chaguo la kwanza kwenye nafasi hiyo mbele ya beki mzawa, Miraji Adam.

Shafiq Batambuze- Singida Utd

Kabla ya ujio wa Batambuze ambaye Singida United ilimsajili alitokea Tusker ya Kenya, beki bora mgeni wa kushoto alikuwa akitajwa kama Mzimbabwe, Bruce Kangwa wa Azam FC.

Hata hivyo, ndani ya kipindi kifupi alichoichezea Singida United kwenye Ligi Kuu, Batambuze ameonekana kuzima nyota ya Kangwa na kutokana na uwezo wake wa kusaidia mashambulizi na kulinda jambo lililofanya achaguliwe kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu mwezi Septemba.

Asante Kwasi- Lipuli FC

Sifa yake kubwa ni kucheza kwa bidii, kujitolea na kuhakikisha anakuwa wa kwanza kuucheza mpira wowote ambao anauwania na washambuliaji wa timu pinzani uwe wa juu au chini jambo ambalo limekuwa msaada mkubwa kwa safu ya ulinzi ya timu yake.

Mbali na kujilinda, Kwasi pia ana uwezo mkubwa katika kusaidia mashambulizi pamoja na kufunga na hadi sasa amehusika katika mabao matatu ya Lipuli na amefunga mawili na kutoa pasi ya bao moja.

Yakubu Mohammed-Azam FC

Ameziba pengo lililoachwa na Paschal Wawa kutokana na matumizi bora ya nguvu na akili pindi anapokabiliana na washambuliaji wa timu pinzani.

Ni kiongozi mzuri wa safu ya ulinzi ya Azam FC na amefanya timu hiyo kuwa na kuta mgumu zaidi msimu huu, ikiwa imeruhusu mabao mawili tu hadi sasa katika mechi tisa.

Kabamba Tshishimbi-Yanga

Kiungo wa shoka aliyemaliza tatizo la Yanga katika eneo la kiungo wa ulinzi, na zaidi ni kutokana na uwezo wake wa kupora mipira kutoka kwa wachezaji wa timu pinzani na kuziba mianya ya wapinzani kutengeneza nafasi za mabao.

Ubora wake katika eneo hilo umenifanya Yanga iruhusu mabao manne tu hadi sasa.

Haruna Niyonzima- Simba

Hakuna pasi yoyote ya bao ambayo amepiga hadi sasa wala kufunga lakini uwepo wake umekuwa ukiisaidia Simba kutengeneza na kufunga idadi kubwa ya mabao kutokana na mchango wake wa kumiliki dimba la kati mbele na kupiga chenga jambo linalofanya afungue nafasi kwa wenzake.

Thaban Kamusoko-Yanga

Ni injini ya kutengeneza mabao katika klabu ya Yanga, ana uwezo wa hali ya juu katika kumiliki mpira, kusoma mchezo, kupiga pasi za mwisho pamoja na kufunga bao pindi apatapo nafasi.

Mzimbabwe huyo kukosekana kwake kwa muda mrefu kumekuwa kukiipa wakati mgumu Yanga kwani huwa haitengenezi nafasi kwa kiasi kikubwa pindi anapokuwa nje.

Emmanuel Okwi-Simba

Siku zote namba zimekuwa hazidanganyi na hilo ndilo linaloonekana kwa Okwi ambaye takwimu za mabao aliyofunga hadi sasa, zinamfanya awemo katika kundi la nyota wanaounda kikosi bora cha wachezaji wa kigeni.

Okwi aliyesajiliwa na Simba kwa mkataba wa miaka miwili akitokea SC Villa ya Uganda, hadi sasa ndiye mfungaji anayeongoza kwa kufumania nyavu akiwa amefunga mabao nane.

Tafadzwa Kutinyu-Singida Utd

Ana jicho la goli, uwezo wake wa kutengeneza na kufunga mabao ni wa hali ya juu lakini pia ana akili ya kukabiliana na mabeki hata pale anapokuwa kwenye mazingira magumu.

Pamoja na hilo anabebwa na uwezo wake wa kucheza nafasi tofauti za mbele kwa ustadi wa hali ya juu jambo ambalo ni nadra kuliona kwa wachezaji wengine

Obrey Chirwa-Yanga

Pambano la Mbeya City alipiga hat trick na mara zote unapotaja mafanikio ya Yanga kwa sasa, jina la Chirwa haliwezi kukosa katika orodha ya nyota wanaochangia mafanikio.

Hiyo kutokana na uwezo wake wa kutengeneza nafasi na kufunga, akibebwa na nguvu pamoja na kasi aliyonayo.

Hadi sasa mshambuliaji huyo ameifungia Yanga mabao sita kwenye ligi huku akitoa pasi mbili zilizozaa mabao.

WACHEZAJI WA AKIBA

Youth Rostand, Yanga

Huu ni msimu wa kwanza kwa Rostand kuichezea Yanga akitokea African Lyon ambayo ilishuka daraja, uwezo wake umemfanya kuwa kipa namba moja mbele ya Beno Kakolanya, amefungwa mabao manne pekee.

Juuko Murshid, Simba

Mbali na kutopata nafasi ya kucheza mara kwa mara kwenye kikosi cha Simba atabaki kuwa moja ya mabeki bora wa kati wa kigeni, Juuko anaweza kucheza na Kwasi au Yakubu kwenye kikosi hiki.

Bruce Kangwa, Azam FC

Faida anayoitoa Kangwa kwenye kikosi cha Azam ni kucheza kwake kwenye nafasi zaidi ya moja, anaweza kutumika kama beki wa kushoto ama akacheza kama beki wa kati.

James Kotei, Simba

Uwezo wake wa kukaba umemfanya kupata nafasi ya kuanza mara kadhaa kwenye kikosi cha Simba huku Jonas Mkude ikimlazimu kutumika kama mchezaji wa akiba na muda mwingine huanza wote, Kotei anaweza kucheza kwenye eneo la Tshishimbi.

Danny Usengimana, Singida

Ubora wa Singida United umechangiwa na uwepo wa Usengimana kwenye idara ya ushambuliaji, Usengimana anaweza kuwa mbadala sahihi wa Okwi au Kutinyu ambaye amekuwa na muunganiko naye mzuri kwenye kikosi cha Singida United.

KOCHA MKUU

Kocha Joseph Omog ni miongoni mwa makocha bora wa kigeni alitua Azam na kuipa ubingwa wa ligi msimu wa 2013/2014 akiwa ametoka kuiongoza klabu ya A.C Leopards ya Jamhuri ya Kongo (Brazaville) kutwaa ubingwa wa ligi ya nchi hiyo kwa misimu miwili mfululizo (2012 na 2013).

Pia 2012 aliiwezesha A.C Leopards kunyakuwa ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Afrika kwa kuzipiga kumbo timu ngumu na zenye uzoefu mkubwa kama vile Mas de Fes ya Morocco, Heartlands ya Nigeria na Sfaxien ya Tunisia.

Kadhalika mwaka huu 2013, A.C Leopards chini ya ukufunzi wa Omog ilitinga hatua ya makundi ya Ligi ya mabingwa Afrika na kupangwa katika kundi moja na timu mbili zilizocheza fainali; Al Ahly ya Misri (bingwa) na Orlando Pirates ya Afrika Kusini.

KOCHA MSAIDIZI

George Lwandamina amejiunga na Yanga, Desemba 2016, akitokea Zesco ya kwao Zambia, aliyoifundisha kwa mafanikio makubwa na kuifikisha nusu fainali ya michuano ya Ligi ya mabingwa Afrika na kutwaa mataji mawili mfululizo ya Ligi Kuu ya Zambia.

Ugeni wake haukumzuia kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita, mbinu za Lwandamina na Omog hazina utofauti sana kutokana na makocha hao kuamini kwenye kujilinda kwanza.

Hivyo wanaweza kuendana na kufanya kazi kwa pamoja na kutengeneza muunganiko wa kikosi chetu cha wachezaji wa kigeni wanaocheza Ligi Kuu Tanzania Bara.