Wakulima walia na lumbesa, walaumu mamlaka kushindwa kudhibiti

Muktasari:

  • Na katika maeneo mengi tumezoea kuona wanunuzi wakilalamikia kupunjwa na mizani zinazotumika hata kuulazimu Wakala wa Vipimo kufanya ukaguzi wa mara kwa mara.

Katika kufanya manunuzi ya bidhaa yoyote kuna utaratibu wa vipimo maalum vilivyopangwa na wahusika na kusimamiwa na serikali kupitia wakala wa vipimo ili kuhakikisha mnunuzi wa bidhaa haibiwi.

Na katika maeneo mengi tumezoea kuona wanunuzi wakilalamikia kupunjwa na mizani zinazotumika hata kuulazimu Wakala wa Vipimo kufanya ukaguzi wa mara kwa mara.

Hali ni tofauti kwa wakulima nchini hupunjwa wauzapo mazao yao. Wanunuzi wamekuwa wakijipangia ujazo wanaoutaka bila kuzingatia vipimo. Mazao mengi ya wakulima yamekuwa yakipimwa kwa magunia, ndoo au galoni bila kuzingatia mizani zenye vipimo vya kitaalam hivyo kuwapunja.

Mtandao wa vikundi vya wakulima hapa nchini (Mviwata) umeliona hili hivyo kuandaa kongamano la wakulima wakati wa maonyesho ya nanenane yaliyofanyika kikanda mkoani Morogoro ili kulitafutia ufumbuzi.

Mkurugenzi wa Mviwata, Steven Luvuga anasema kutozingatia vipimo vya kitaalam ni kuwanyonya wakulima kwani magunia yanajazwa mpaka kupitiliza maarufu kama lumbesa hivyo kuwadhulumu wakulima.

“Tumeona tutumie maadhimisho haya kuwakutanisha wakulima kutoka maeneo mbalimbali nchini ili kujadili kwa kina tatizo la lumbesa,” anasema.

Mkurugenzi huyo anaeleza kwamba lumbesa haina tofauti na makinikia kwani yanasababisha hasara kwa mkulima na serikali katika ukusanyaji wa ushuru wa mazao.

Kukabiliana na hali hiyo, Luvuga anasema serikali inapaswa kusimamia ili kuhakikisha vipimo halali vinatumika katika maeneo yote yanayosafirisha mazao na kumsaidia mkulima kupata tija kwenye kilimo chake.

Mshiriki wa kongamano hilo na mkulima kutoka mkoani Njombe, Jema Msigwa anasema kwa kawaida eka moja ya viazi hutoa gunia 100 lakini kutokana na lumbesa mkulima anaambulia gunia 60 tu.

Jema anasema wakulima wamekuwa wakipata hasara kutokana na wanunuzi kugoma kutumia mizani zenye vipimo halisi huku serikali ikiwa kimya katika hilo.

“Si wakulima tu tunaopata hasara kutokana na lumbesa hata serikali inapoteza mapato kwani hutoza ushuru kutokana na idadi ya magunia. Sasa kwenye eka moja badala ya kupata ushuru wa magunia 100 huambulia ushuru wa magunia 60 tu,” anasema Mkulima huyo.

Mkulima mwingine kutoka wilayani Kilosa iliyopo Morogoro, Msumule Isa anaulaumu uongozi wa Soko la Kariakoo kwa kushindwa kuzuia lumbesa kwani ndilo soko kuu linalotegemewa na wakulima wa mikoa mbalimbali.

Issa anasema ni vema vita ya lumbesa ikapiganwa kuanzia vijijini hadi sokoni yanakouzwa mazao hayo kwani wanunuzi wengi husema bila lumbesa hawawezi kupata wateja Kariakoo.

“Tuwaombe wenzetu wa Dar es Salaam watusaidie kudhibiti lumbesa katika masoko ya mjini ili, wakati sisi tukidhibiti ngazi ya vijiji nao watusaidie katika ngazi za mikoa na taifa,” anasema.

Maulana Nassor kutoka Iringa anaiomba serikali kuandaa utaratibu wa kuanzisha vituo vya kuuzia mazao kwa kununua mizani na kuzigawa kwa kila kijiji ili wakulima wawe na uhakika wa sehemu ya kupimia mazao yao.

Anasema kwa kiasi kikubwa wakulima wanachangia pato la halmashauri zao na taifa kwa ujumla hivyo yawepo malengo ya kununua mizani kwa kila kijiji na baadaye kila kata ili kuhakikisha mazao yote yanapitia katika vipimo sahihi.

“Wakulima tupo tayari kuchangia hili kama serikali itaamua kununua mizani kwa vijiji vyetu maana tunakerwa na vipimo visivyo rasmi vinavyotunyonya na mkulima hawezi kukataa kuuza kwa utashi wake wakati wenzie wanauza,” anasema.

Hatua kadhaa zinachukuliwa kukabiliana na changamoto hii. Idara yake ya Sera,Mipango na Utawala ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) ilifanya utafiti kubaini matumizi ya vipimo kwenye mazao ya kilimo.

Akiwasilisha ripoti ya utafiti huo kwenye kongamano hilo Mwalimu Rodgers Andrew anasema lumbesa inasababisha serikali kupoteza asilimia 30 ya mapato yake kila mwaka.

Anasema mapato hayo hupotea kwa sababu lumbesa ihusababisha kati ya kilo 120 hadi 130 kuwekwa kwenye gunia la kilo 100 hivyo kumnyonya mkulima na kuisababishia hasara serikali.

Anasema iwapo maofisa ugani watatumika vyema wanaweza kusaidia kudhibiti changamoto hiyo. “Maofisa hawa huwa hawatembelei wakulima na ukihoji unaambia hakuna usafiri wala hakuna fedha za kufanya hivyo lakini hakuna siku zimekosekana fedha za posho kwa madiwani” anasema mwalimu huyo.

Kukabiliana na hali hiyo, anasema halmashauri zinapaswa kuwajali wakulima kwani kwa kiasi kikubwa zinajiendesha kutokana na ushuru unaotokana na mazao yao.

Chuo hicho kinapendekeza Serikali kuweka utaratibu wa kutoza kiwango kimoja cha ushuru wa mazao katika halmashauri zote nchini ili kuwawezesha wakulima kuwa na ushindani sawa wanapofikisha mazao yao sokoni.

Licha ya serikali kufuta tozo kwa mazao yanayosafirishwa kutoka whalmashauri moja kwenda nyingine kwa yale yasiyozidi tani moja, kwa sasa ushuru wake unapangwa na madiwani hivyo viwango kutofautiana wakati soko wanalolitegemea zaidi ni moja ambalo ni la Kariakoo la jijini Dar es Salaam.

“Wakulima kutoka mikoa karibu yote wanategemea kuuza mazao yao sokoni Kariakoo hivyo wanapaswa kuwa na bei moja lakini wakati mwingine wanashindwa kutokana na kulipa ushuru tofauti,” anasema.

Wakala wa Vipimo

Meneja wa Wakala wa Vipimo mkoani Morogoro, Wilson Kachori anaunga mkono hoja ya kuwa na mizani kwa kijiji na kuzishauri halmashauri kuhakikisha utekelezaji wa mpango huo ili mazao yanapimwe kwa usahihi badala ya kutumia ndoo au vipimo vingine.

Anasema wakati halmasahuri zikiwa katika utaratibu wa kununua mizani ni vema wanunuzi wanaoenda vijijini wakaanzia katika ofisi za kata ili wajiandikishe na kupewa utaratibu wa kufanya ununuzi.

“Ofisi za vijiji na kata zikitumika vizuri zinaweza kudhibiti lumbesa. Ziwekwe sheria za kupiga marufuku na mnunuzi atakayekutwa na lumbesa achukuliwe hatua” anashauri Kachori.

Kwenye kongamano hilo, wakulima na wadau wengine wa kilimo waliazimia lumbesa iwe mwisho mwaka huu.