Mambo yanayosababisha uvimbe wa kidoletumbo

Muktasari:

  • Kwa wastani, kidoletumbo kina urefu wa sentimeta tisa ingawa kinaweza kuwa na urefu wowote kati ya sentimeta mbili hadi 20 kwa baadhi ya watu.

Kidoletumbo maarufu kama Apendeksi ni sehemu ya utumbo iliyo na umbo kama kidole na uwazi kama bomba ambayo inaning’inia katika makutano ya utumbo mdogo na  mpana, upande wa kulia, chini ya tumbo kati ya kitovu na nyonga.
Kwa wastani, kidoletumbo kina urefu wa sentimeta tisa ingawa kinaweza kuwa na urefu wowote kati ya sentimeta mbili hadi 20 kwa baadhi ya watu.
 Historia ya utabibu inaonyesha kuwa kidoletumbo kirefu zaidi ni kile kilichoonekana kwa mgonjwa aliyefanyiwa upasuaji huko Zagreb, nchini Croatia ambacho kilifika urefu wa sentimeta 26.  Inakadiriwa kuwa, kipenyo cha kidoletumbo ni kati ya milimeta saba mpaka nane.
Kiungo hiki kinaweza kuathiriwa na vitu mbalimbali na kusababisha kuvimba, ugonjwa ambao uligunduliwa kwa mara ya kwanza na Dk Robert Lawson Tait mwaka 1886, na tangu hapo madaktari wamekuwa wakiutibu kwa upasuaji wa kukiondoa kiungo hicho.
Kidoletumbo husaidia katika mmeng’enyo wa chakula na uzalishaji wa kinga za mwili ambazo husaidia kupambana na kuua baadhi ya vimelea vya maradhi vinavyoingia katika tumbo kupitia chakula.
Utafiti wa kitabibu uliofanyika katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Winthrop iliyoko New York Marekani, na kuchapishwa mwaka 2011 katika jarida la Clinical Gastroentorology and Hepatology toleo namba 9, ulionyesha kuwa watu ambao hawana kidoletumbo walikuwa wanakabiliwa na hatari ya kupata uvimbejoto wa utumbo unaosababishwa na bakteria aina ya Clostridium difficile, mara nne zaidi wakilinganishwa na wenye nacho.
Utafiti mwingine uliofanywa mwaka 2007 na profesa wa upasuaji, Dk William Parker pamoja na jopo la wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Duke, ulibainisha kuwa kidoletumbo huhifadhi  bakteria rafiki kwa binadamu wanaosaidia umeng’enyaji au ulainishaji wa vyakula vya nyuzilishe (fibres) ambavyo tunakula kila siku.
Utafiti huo unaonyesha kuwa bakteria hawa hupotea kwa wingi wakati binadamu anapopata maradhi ya kuharisha, kipindupindu na kuhara. Wale wanaobaki salama ndani ya kidoletumbo, huzaliana na kurudi katika utumbo ili kusaidia mwili uendelee na kazi zake.

Pamoja na faida zake, Profesa Parker anasema haimaanishi kuwa ni lazima kidoletumbo kiendelee kuwapo kwa gharama yoyote. Muhimu watu wakaelewa kwamba hawana sababu ya kuking’angania kidoletumbo kilichovimba.

“Hatutaki matokeo ya utafiti wetu yasababishe madhara. Watu wasiseme, kidoletumbo changu kina kazi muhimu hivyo siendi kwa daktari. Nitajaribu kukilinda ili kisitolewa,” anasena Profesa Parker.

Ugonjwa wa kuvimba kwa kidoletumbo unaweza kuathiri mtu wa rika lolote, lakini wale wenye umri kati ya miaka 15 hadi 30 wana na uwezekano mkubwa wa kupatwa na tatizo hili. Pamoja na hali hiyo, inasemekana kuwa wanawake wana uwezekano mdogo wa kuugua ugonjwa huu ikilinganishwa na wanaume. Wataalamu wa afya pia wanabainisha kwamba siyo rahisi kwa watoto chini ya miaka miwili kupatwa na ugonjwa huu.

Uvimbe wa kidoletumbo ukikaa muda mrefu, huzuia mzunguko wa damu hivyo kusababisha kuta zake kuoza na kutunga usaha. Hali hii husababisha uvimbe wa ngozi laini inayofunika tumbo na kutokeza maumivu makali ya tumbo lote. Iwapo mgonjwa atachelewa kupata tiba sahihi, uambukizo kutoka katika uvimbe wa ngozi laini inayofunika tumbo husambaa katika mfumo wa damu na kusababisha matatizo mengine makubwa zaidi. Tatizo hilo linaweza kuwa baya zaidi endapo kidoletumbo kitapasuka kwani mgonjwa anakuwa katika hatari ya kupoteza maisha.

Tafiti mbalimbali za kitabibu ikiwa ni pamoja na ule uliochapishwa mwaka 2010 katika jarida la ‘Infectious Disease Clinics of North America’ toleo namba 24(4), zinaeleza kuwa uvimbe husababishwa na maambukizi ya bakteria, fangasi, virusi na minyoo kama vile kichocho, Enterobius vermicularis, Strongyloides stercoralis na minyoo mikubwa. Vilevile, tatizo hili linaweza kusababishwa na uvimbe kwenye tishu za limfu au wowote katika utumbo.

Kwa kuwa sehemu hii ya utumbo hupitiwa na chakula kilichoyeyushwa, inaweza kuzibwa endapo chakula hicho kitakuwa na mchanga au vitu vidogovidogo ambavyo ni vigumu kama vile nyama zisizotafunika au mbegu za matunda ambazo hujikita ndani na kushindwa kutoka. Wachunguzi wa mambo ya mfumo wa chakula wanadai kuwa asilimia tano ya vitu vigumu ambavyo mtu anaweza kumeza lakini visiyeyuke, vinaweza kujikusanya katika sehemu ya chini ya utumbo mpana na kuingia katika kidoletumbo.

Matokeo ya utafiti uliofanyika nchini Uturuki na kuchapishwa katika jarida la Asian Pacific Journal of Tropical Biomedicine, toleo namba 1(2) la mwaka 2011, yalionyesha kuwa mbegu za matunda na taka ngumu zinazotokana na mabaki ya chakula, zinaweza kusababisha uvimbe wa kidoletumbo. Taka hizo ngumu zinapojikusanya kwenye kidoletumbo au kuganda na kushindwa kutoka, huanza kuchochota, kuvimba, kupata maambukizi ya bakteria na hatimaye kusababisha maumivu makali kwa muhusika.

Dalili kuu ya ugonjwa huu ni maumivu makali ya tumbo ambayo huanzia katikati ya tumbo, eneo la kitovu na ambayo hudumu ndani ya saa moja au zaidi na baada ya hapo huhamia upande wa kulia, chini ya tumbo ambako ndiko kidoletumbo kilipo. Maumivu haya yanaweza kuwa makali zaidi wakati wa kupiga chafya, kukohoa au kutembea. Dalili nyingine zinazoweza kujitokeza ni pamoja na kuhisi homa, kufunga choo, kichefuchefu na kuharisha.

Uchunguzi wa kitabibu wa ugonjwa huu unategemea maelezo na historia ya mgonjwa, dalili zinazojitokeza. Vipimo vya damu na mkojo wa mimba kwa wanawake wenye umri wa kuzaa pia vinaweza kufanyika pamoja na vipimo vya CT scan na Ultrasound ya tumbo ili kuweza kubaini hali na ukubwa wa tatizo la kidoletumbo. Hakuna kipimo rahisi na cha moja kwa moja kinachoweza kuthibitisha haraka ugonjwa wa kidoletumbo kwa wanawake hasa wakiwa wajawazito.

Kutokana na hali hiyo iwapo daktari ataona dalili za wazi baada ya kubaini sehemu yenye maumivu tumboni, anaweza kuamua kufanya upasuaji wa tumbo haraka ili kuondoa kidoletumbo kilichovimba, kuziba au kuoza. Lakini mgonjwa anaweza kufanyiwa upasuaji baada ya kuelezwa hali halisi ya tatizo lake na kusaini fomu za kukubaliana na tiba ya upasuaji ili kuokoa maisha yake kutokana na hali aliyonayo. Mgonjwa anaweza kupewa matibabu ya dawa za kundi la antibaiotiki kwa kudungwa sindano ambazo zinaweza kuuwa bakteria wanaoshambulia kidoletumbo.

Kutokana na hatari zinazoambatana na tatizo hili, mgonjwa anashauriwa kuwahi mapema kituo cha afya mara anapoona dalili. Ni busara kuepuka matumizi ya dawa za asili na tiba mbadala kama baadhi ya watu wanavyofanya pindi wanapohisi maumivu makali ya tumbo jambo ambalo linaweza kuhatarisha afya na maisha yao.

Ingawa ni vigumu kujikinga na kuepuka hali hii, lakini ni vyema kutambua kuwa katika jamii zinazotumia vyakula vyenye nyuzilishe, matunda na mbogamboga kwa wingi, tatizo hili halitokei mara kwa mara. Pia ni busara kujiepusha na utumiaji wa vyakula vyenye mchanga kama vile mchele na dagaa wanaokaushwa na kuhifadhiwa katika hali duni. Vilevile, inashauriwa kuepuka kuweka mdomoni vitu vigumu, ambavyo si chakula vinavyoweza kumezwa. Wataalamu pia wanashauri kwamba wakati wa kula ni vyema chakula kitafunwe vizuri kabla ya kumeza.