Haji Mwinyi awangukia mashabiki Yanga

Muktasari:

  • Yanga inahitaji ushindi katika mchezo wake ujao ili kufufua matumani yake katika Kundi D

Dar es Salaam. Beki wa Yanga, Haji Mwinyi amewataka mashabiki wa timu hiyo kuungana kwa pamoja katika kipindi kigumu wanachopitia badala ya kugawanyika.

Mwinyi amekiri kwamba anajua namna wanavyoumizwa kutokana na mwenendo wa timu hiyo hasa kuambulia kipigo cha mabao 4-0 dhidi ya Gor Mahia ya Kenya, lakini aliwasihi kwamba mechi ya marudiano watapambana kurejesha furaha yao.

"Mcheza kwao hutunzwa basi tunawaomba wakati tunajiandaa na mechi ya marudiano watuunge mkono wachezaji ni wale wale ambao tulikuwa kwenye kikosi kilichomaliza msimu huu.

"Nguvu yao ya kutuunga mkono itatupa morali ya juu kuona tupambane mpaka tone la mwisho kwa ajili ya maendeleo ya klabu, hata msimu ulioisha walikuwa wanasema Yanga mbovu, lakini mashabiki hawakuchoka tuliweza kufika safari yetu," alisema mwinyi.