Rais Samia aionya Simba fainali Muungano

Muktasari:

  • Akizungumza leo kwenye kilele cha Miaka 60 ya Muungano, Rais Samia amesema Simba haitakiwi kuidharau Azam kwenye mechi hiyo ya fainali itakayochezwa kesho kuanzia saa 2:15 usiku kwenye Uwanja wa New Amaan, Kisiwani Zanzibar.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan ameionya klabu ya Simba wakati ikijiandaa kukutana na Azam kwenye fainali ya Kombe la Muungano.

Akizungumza leo kwenye kilele cha Miaka 60 ya Muungano, Rais Samia amesema Simba haitakiwi kuidharau Azam kwenye mechi hiyo ya fainali itakayochezwa kesho kuanzia saa 2:15 usiku kwenye Uwanja wa New Amaan, Kisiwani Zanzibar.

"Timu ya mdogo wangu Kassim (Majaliwa, Waziri Mkuu) imeingia kwenye fainali hizi za Muungano lakini wasiwadharau Azam huenda matokeo yakawa tofauti," amesema Samia huku akitabasamu.

Simba ilitangulia kutinga kwenye fainali hiyo baada ya juzi Aprili 24 kuichapa KVZ kwa mabao 2-0 kwenye mchezo wa nusu fainali ya mashindano hayo.

Azam nayo ikaifuata Simba baada ya jana kuichapa KMKM kwa mabao 5-2 na sasa timu hizo zitakutana katika mechi ambayo itakuwa ni kama maandalizi ya kukutana kwenye mechi yao ya raundi ya pili ya Ligi Kuu Bara itakayochezwa Mei 9. Mechi ya raundi ya kwanza ya Ligi Kuu timu hizo zilitoka sare ya 1-1.

Michuano hiyo imerejea mwaka huu baada ya kukosekana kwa miaka 20 tangu iliposimama kufanyika.