Wadau walia na tuzo ya Aziz Ki

TUZO ya mchezaji bora wa mwezi Aprili ya Ligi Kuu Bara imezua gumzo kwa baadhi ya wadau wa soka nchini kutokana na kuteuliwa Stephane Aziz KI badala ya Joseph Guede ambaye ameonekana kuwa na mchango mkubwa zaidi katika pointi 10 ambazo Yanga imevuna ndani ya mwezi huo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Bodi ya Ligi Kuu Bara (TPLB), Aziz KI ametwaa tuzo hiyo kwa kuonyesha kiwango bora na kuwa msaada kwa Yanga katika ushindi wa michezo mitatu kati ya minne, jambo ambalo baadhi ya watu wamehoji kutokana na Guede kuwa juu kitakwimu kuliko fundi huyo wa kimataifa kutoka Burkina Faso.

Kivipi? Katika michezo minne ambayo Yanga imecheza ndani ya mwezi huo ambapo ni dhidi ya Singida FG, Simba, JKT Tanzania na Coastal Union, Guede amefunga mabao manne ambayo yaliifanya Yanga kuvuna pointi tatu katika michezo mitatu tofauti. 

Katika mchezo dhidi ya Singida FC, Muivory Coast huyo alifunga mabao mawili, la kwanza ndio lilifungua akaunti ya mabao kwa Yanga katika dakika ya 41 huku la pili kwake likiwa la tatu kwa Wananchi katika dakika ya 67, katika mchezo huo, Aziz alifunga moja katika dakika 65. Mzize alitoa asisti mbili katika ushindi huo wa mabao 3-0.

Wawili hao walifunga tena katika mchezo uliofuata dhidi ya Simba lakini bao la Guede ndilo lililoamua mchezo huo ambao ulimalizika kwa Wananchi kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Mkapa.

Wote wawili hakuna aliyefunga katika mchezo wa tatu lakini Guede aliendeleza moto wake katika mchezo wa tatu kwa kufunga bao pekee ambalo liliifanya Yanga kuvuna pointi tatu muhimu dhidi ya Coastal Union ya Tanga kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi. 

Takwimu zinamuonyesha Guede akihusika katika michezo mitatu tofauti tena katika mabao ambayo yaliamua ushindi kwa Yanga, hivyo taarifa ya bodi ya ligi iliyosema; "Kwa mwezi Aprili, Ki alionesha kiwango kikubwa na kuwa msaada kwa timu yake katika ushindi wa michezo mitatu kati ya minne ambayo timu hiyo ilicheza, hivyo Yanga kukusanya alama 10 na kuendelea kubaki kileleni mwa msimamo wa ligi."

Hiyo imewaibua wadau hao na kuwa na mitazamo tofauti, Innocent Mwambenja akiwa mmoja wao ambaye amesema: "Hii tuzo ilikuwa ya Guede lakini hakuna shida tunakubaliana tu na kamati kwa kile ilichoamua."

Kwa upande wake, Darcky Ginny amesema:"Hii tunzo ilistahili apewe Guede mnyonge mnyongeni ila haki yake mpeni. Guede havutii sana uchezaji wake ila kaisaidia sana Yanga katika mechi 4 dhidi ya Singida, Simba, Coastal hakufunga mechi moja tu dhidi ya JKT."

Mbali na upande wa tuzo ya mchezaji bora wa mwezi, kocha wa Yanga, Miguel Gamondi amebeba tuzo ya kocha bora akiiongoza kukusanya alama 10 katika michezo minne iliyocheza, ikishinda mitatu na sare moja hivyo kuendelea kuongoza ligi hiyo yenye timu 16. 

Gamondi amewashinda Bruno Ferry wa Azam na Malale Hamsini wa JKT Tanzania alioingia nao fainali.

Pia Kamati ya Tuzo imemchagua Meneja wa Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam, Amir Juma kuwa Meneja Bora wa Uwanja kwa mwezi Aprili kutokana na kufanya vizuri katika menejimenti ya matukio ya michezo pamoja na masuala yanayohusu miundombinu uwanjani.