Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hiki ndiyo kimemzuia Ronaldo kumzika Jota

Lisbon, Ureno. Cristiano Ronaldo ameonekana kwa mara ya kwanza tangu aache kuhudhuria mazishi ya staa wa Ureno la Liverpool Diogo Jota, ambaye alifariki kwa ajali ya gari wiki iliyopita.

Jota, mwenye umri wa miaka 28, na mdogo wake Andre Silva, mwenye umri wa miaka 25, walifariki dunia baada ya gari lao kupata ajali alfajiri siku ya Alhamisi, Kaskazini mwa mji wa Hispania.

Ajali hiyo ilitokea siku 11 tu baada ya Jota kufunga ndoa na mpenzi wake wa tangu utotoni, Rute Cardoso, ambaye pia ana miaka 28, mama wa watoto wao watatu Dinis (miaka minne) na Duarte (miaka miwili), pamoja na binti yao wa miezi minane, Mafalda.

Wawili hao walizikwa Jumamosi alasiri katika makaburi ya Gondomar, nchini Ureno, huku wachezaji wengi wa timu ya taifa ya Ureno, akiwemo Bernardo Silva na Ruben Neves, wakihudhuria kutoa heshima zao za mwisho.

Hata hivyo, nahodha wa Ureno Ronaldo ambaye awali alituma salamu za rambirambi hakuhudhuria, na inaaminika aliamua kutokwenda kutokana na matukio ya huzuni aliyopitia awali maishani mwake, lakini pia kuipa uhuru familia kumzika mpendwa wao.

Siku moja baada ya mazishi, Ronaldo alipigwa picha akiwa mapumzikoni kwenye boti huko Mallorca Hispania pamoja na mpenzi wake Georgina Rodriguez, huku ikiamini kuwa alikuwa ana nafasi ya kuhudhuria mazishi hayo.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Ureno, iliripotiwa kuwa mchezaji huyo mwenye miaka 40 alikuwa ndani ya mashua akila bata wakati wengi walitegemea angeruka hadi Gondomar, karibu na jiji la Porto kumzika rafiki yake.

Kwa mujibu wa gazeti la Record la nchini Ureno, Ronaldo huenda aliamua kutohudhuria tukio hilo kutokana na hisia zinazomhusu kuhusu kifo cha baba yake, Jose Diniz Aveiro, aliyefariki Septemba 2005 wakati Ronaldo alikuwa na umri wa miaka 20 pekee.

Ronaldo alishtushwa sana kusikia juu ya kifo cha Jota, lakini inasemekana hakusafiri kwa sababu hakutaka uwepo wake kuvuruga umuhimu wa watu wengine kutoa heshima zao kwa Jota na kaka yake, lakini pia aliogopa kuongeza uchungu moyoni mwake wakati wa mazishi.

"Kamera nyingi zingekuwa kwake na labda hali hiyo ingevuruga utaratibu wa mazishi," ilisema taarifa kutoka kwenye gazeti hilo.

Wakati mshambuliaji huyo wa Al-Nassr akikosolewa na baadhi ya watu kwa kutohudhuria, dada yake Katia alimtetea wazi wazi kupitia mitandao ya kijamii.

Kupitia  mtandao wa Instagram, aliandika: “Wakati baba yangu alifariki, pamoja na uchungu wa msiba, tulilazimika kukabiliana na mafuriko ya kamera na watu kuona kila tulipokwenda.

“Na wakati huo hakukuwa na upatikanaji mkubwa wa habari kama sasa, hatukuweza kutoka nje ya kanisa; iliwezekana tu wakati wa mazishi kutokana na msongamano.

“Wakati wa mazishi kulikuwa na marais, makocha wa timu ya taifa wakati huo, kama Luís Filipe Scolari, n.k. Sikumwona hata mmoja. Na hakika walinisalimia. Uchungu ulinipofusha."

“Kuhusu uchungu/familia ni msaada wa kweli, hautajua kinachomaanishwa hadi upitie hali hiyo. Iwapo mtu atanitumia ujumbe wa kumkosoa kaka yangu, nitamblock (sitajali kabisa), yaani, watafanya hivyo mara moja tu.

“Inachosha. Ushabiki kupita kiasi. Kukosoa bila sababu, narudia, bila sababu, sote tuna familia."

“Ni aibu kushuhudia vituo vya televisheni, mitandao ya kijamii kuzungumza kuhusu kutokuwepo kwa mtu mmoja tu msibani badala ya kuheshimu familia iliyopoteza ndugu wawili. Naona aibu hata kuangalia. La kusikitisha." alisema dada huyo.

Ronaldo na Jota walicheza pamoja kwa mara ya mwisho  Juni 8, 2025 wakati walipoiongoza Ureno kutwaa taji la Nations League kwa kuwachapa mabingwa wa Ulaya, Hispania, kwa mikwaju ya penalti mchezo ambao Jota aliingia akitokea benchi.

Nyota huyo wa zamani wa Real Madrid alikuwa miongoni mwa wachezaji wa kwanza kueleza huzuni kupitia mtandao wa Instagram baada ya taarifa za kifo cha mshambuliaji huyo wa Liverpool.

“Hakieleweki. Tulikuwa pamoja tu kwenye timu ya taifa, na ulikuwa umeoa juzi tu,” aliandika Ronaldo.

“Kwa familia yako, mkeo na watoto wako, natuma rambirambi zangu na kuwatakia nguvu familia yako.

“Ninajua utakuwa nao kila wakati. Pumzika kwa amani, Diogo na Andre. Tutawakumbuka daima.”