Simba: Hatuna mpango na Yondani

Mchezaji wa Yanga Kelvin Yondani akielekea kwenye ofisi za rais wa zamani wa klabu hiyo, Tarimba Abbas zilizopo Oysterbay, Dar es Salaam kwa ajili ya mazungumzo ya usajili wake. Picha na Michael Matemanga.

Muktasari:

  • Yondani ameibua taharaki baada ya kuibuka tetesi kwenye mitandano ya kijamii kwamba ana mpango wa kurejea katika klabu yake ya zamani Simba.

Dar es Salaam. Mamilioni anayotaka Kelvin Yondani katika dirisha la usajili yanaweza kuwa matunda ya karata zake anazochanga kwa klabu ya Yanga.

Yondani ameibua taharaki baada ya kuibuka tetesi kwenye mitandano ya kijamii kwamba ana mpango wa kurejea katika klabu yake ya zamani Simba.

Uvumi huo ulienea kwa kasi kuanzia juzi ukidai beki huyo tegemeo wa Yanga anahitaji Sh80 milioni kabla ya kutia saini mkataba wa kubaki kwa mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Ubora na umaarufu wa beki huyo wa kati, uliwaweka roho juu wadau wa michezo nchini kila mmoja akisema lake kuhusu usajili huo.

Itakumbukwa kuwa Yondani amegoma kuongoza na timu kwenda Kenya kucheza mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Gor Mahia, uliochezwa jana usiku kwenye Uwanja wa Kasarani, Nairobi.

Filamu ya usajili wa Yondani inatoa taswira halisi ya jinsi mchezaji huyo alivyoweza kupiga vyema hesabu akitambia uwezo wake wa kuhimili vishindo vya washambuliaji wa kila aina ndani na nje.

Hata hivyo, taarifa za Yondani kutakiwa na Simba hazikuwa za ukweli, ilikuwa ni uzushi kutoka kwa baadhi ya watu wachache waliotaka kumtengenezea ulaji mchezaji huyo.

Mmoja wa viongozi wa juu wa klabu ya Simba alisema Simba haikuwa na mpango wa kumsajili Yondani kwa namna yoyote na hakuwahi kujadiliwa katika kikao chochote ndani klabu hiyo.

“Nataka niwaambie ukweli hatukuwa na mpango wa kumsajili Yondani na hatuna nia ya kumsajili, hiyo ni presha tu kutoka kwa mchezaji mwenyewe,”alisema kigogo huyo aliyeomba hifadhi ya jina lake.

Yondani anayetarajiwa kutimiza miaka 34 mwezi Oktoba amekuwa mhimili wa Yanga kwa kipindi cha miaka minne tangu aliposajiliwa kutoka Simba mwaka 2012.

Beki huyo amejijengea umaarufu kwa uwezo wa kupoka mipira kutoka kwa washambuliaji, kuokoa mashambulizi langoni, kucheza mipira ya juu na uzoefu ni miongoni mwa sifa zinazobeba nguli huyo.

Atua kwa Tarimba

Jana asubuhi Yondani aliwasili kwenye Ofisi za Rais wa zamani wa Yanga, Tarimba Abbas Oysterbay, Dar es Salaam iliyopo Kampuni ya SportPesa.

Saa 4:26 asubuhi Yondani akiwa kwenye gari dogo aina ya Toyota Carina alionekana akiingia kwenye Ofisi za Tarimba.

Mazungumzo ya Yondani na Tarimba yalidumu kwa saa moja na nusu na baada ya kufikia mwafaka beki huyo kwa mara nyingine akiwa mwenye tahadhari aliondoka haraka katika eneo hilo.

Tarimba alisema Yondani alikwenda kwenye ofisi zake kumsalimia na aliahidi taarifa za usajili wake zinatarajiwa kutolewa leo.

“Unajua kuna watu wanataka kukuza vitu kama kutakuwa na kinachoendelea kuhusu Yondani mtajulishwa, isitoshe mimi sio Mwenyekiti wa kamati ya mpito ya Yanga, nilishatoka, lakini Yondani kuonekana ofisini kwangu sio tatizo uenda alikuja kusalimia tu,” alisema Tarimba ambaye alikataa kata kata kuweka wazi mazungumzo yake na Yondani.