Aliyenyukwa Russia akingiwa kifua

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Kamati ya Kusimamia Ngumi (TPBRC) Jovic  Anea, amesema bondia Idd Mkwera alizidiwa maarifa na mpinzani wake katika pambano la ngumi lililofanyika Russia hivi karibuni.

Anea alisema hakuna ujanja uliofanyika kumpeleka bondia asiyekuwa na uwezo kama inavyodaiwa na baadhi ya wadau wa ngumi nchini.

Dar es Salaam.Siku chache baada ya bondia Idd Mkwera kupigwa kwa Technical Knock Out (TKO) nchini Russia, Kamati ya Kusimamia Ngumi (TPBRC) imesema matokeo hayo ni sehemu ya mchezo.

Mkwera alipigwa kwa TKO na Makhmud Gaipov katika raundi ya tatu ya pambano lililofanyika katika mji wa Ekaternburg, Russia.

Mwamuzi, Roman Petrov alimuokoa Mkwera asiendelee kuchezea kipigo kutoka kwa mpinzani wake aliyekuwa akimshambulia kuanzia dakika ya kwanza ya raundi ya tatu kabla ya pambano kusimamishwa.

Baada ya pambano hilo kuibua minong'ono kwa baadhi ya wadau wa ngumi wakihoji ubora wa Mkwera, Makamu Mwenyekiti wa TPBRC, Jovic Anea alisema bondia huyo alifanya maandalizi ya kutosha.

Anea alisema hakuna ‘fitna’ iliyofanywa ya kumpeleka bondia asiyekuwa na kiwango bora cha kushindana  kama inavyodaiwa na baadhi ya wadau wa ngumi.

"Sijui kilichotokea hadi kupigwa TKO huenda mabondia wetu wakifika nje ya nchi wanapakini, lakini mazoezi yake yalikuwa mazuri,"alisema Anea.

Kigogo huyo alisema matokeo aliyotangaza mwamuzi ni sahihi kwa kuwa Mkwera alizidiwa kwa makonde mazito ya mpinzani wake.

Alisema mwamuzi wa pambano hilo alifanya uamuzi wa busara kumuokoa bondia huyo asiendelea kuchapwa baada ya kuzidiwa na makonde ya mpinzani wake.