Arusha yaita 12, Taifa Cup

Muktasari:

  • Mara ya mwisho Mkoa wa Arusha kuwa wenyeji wa michuano ya Taifa Cup ilikuwa mwaka 2011.

Katibu Mkuu wa chama cha netiboli Mkoani hapa Grace Sihuyi alisema timu ya Mkoa wa Arusha imeundwa na wachezaji 12 itashiriki mashindano ya Taifa Cup yatakayoanza kesho mkoani Arusha.

Sihuyi alisema kikosi hicho kinafundishwa na Kocha Pilly Bonye wamejifua kwa muda mrefu ili kuhakikisha wanafanya vyema kwenye mashindano hayo.

“Maandalizi ya kupokea ugeni wa mikoa 12 ambayo tumetaarifiwa na Chaneta kuwa wamethibitisha ushiriki wao, yanakwenda vyema na tumeandika barua ya kumwoma katibu tawala wa Mkoa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa mashindano hayo.”

Alisema ratiba ya michezo hiyo haijatolewa kutokana na Chaneta kuhofia timu zinaweza kuchelewa kuwasili katika eneo husika hivyo ratiba kamili itajulikana baada ya uongozi kamili kuwasili Arusha.

Mikoa iliyothibitisha ni pamoja na Kilimanjaro, Kinondoni, Ilala, Temeke, Songwe, Kigoma, Kagera, Manyara na wenyeji Arusha japo kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Chaneta Dk Devota Marwa alisema kuwa hadi jana alipokea simu za mikoa Kagera na Songwe kuwa wameanza safari.