Makipa Manula, Dida wakabana koo Simba

Muktasari:

  • Dida aliyewahi kucheza Simba kabla ya kutimkia Yanga, amerejea katika klabu hiyo na sasa anakwenda kupigania namba na Manula ambaye ni kipa chaguo la kwanza Simba na Taifa Stars.

Dar es Salaam. Presha ya ushindani wa namba imeanza kuonekana kwa makipa wa Simba, Aishi Manula na Deogratius Munishi ‘Dida’ kutokana na ubora wao katika kusimama vyema langoni.

Dida aliyewahi kucheza Simba kabla ya kutimkia Yanga, amerejea katika klabu hiyo na sasa anakwenda kupigania namba na Manula ambaye ni kipa chaguo la kwanza Simba na Taifa Stars.

Makipa hao wameibua mjadala nani atakuwa chaguo la kwanza kwa kuwa wote wawili wana uzoefu wa kutosha katika Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano ya kimataifa.

Dida kama ilivyokuwa kwa Manula, aliwahi kuwa kipa namba moja Yanga na Taifa Stars kabla ya kutimkia Afrika Kusini alipokwenda kucheza soka ya kulipwa.

Ujio wa Dida unatajwa kuwa utaongeza presha kwa Manula ambaye awali hakuwa na changamoto ya kuwania namba kwa kuwa Said Mohammed ‘Nduda’ na Emmanuel Mseja hawakuwa tishio.

Licha ya Simba kuwa na makipa watano, Manula na Dida wanapewa nafasi kubwa ya kuwa katika kikosi cha kwanza wakisaidiwa na Nduda, Mseja, Ally Salum.

Katika mazungumzo yao kwa mwandishi wa gazeti hili, wachezaji hao walidai kila mmoja ana ndoto ya kupata namba katika kikosi cha kwanza.

Makipa hao kila mmoja ana amini ana uwezo mzuri wa kucheza vyema katika mashindano mbalimbali yakiwemo ya Ligi Kuu.

Manula alisema ataendelea kupambana ili kubaki katika ubora wake ulioisaidia Simba kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu uliopita.

“Nafanya mazoezi binafsi kwa siku mara mbili, hiyo ndiyo ratiba yangu hata kama kutakuwa na mazoezi ya timu, lakini lazima nijifue binafsi, nina programu ya asubuhi na jioni, sitarajii kukaa benchi na ili nitimize ndoto yangu mazoezi ndio kila kitu,”alisema Manula.

Dida aliyekuwa akicheza klabu alisema ana sifa ya kucheza kikosi cha kwanza Simba na matarajio yake ni kuisaidia klabu hiyo kupata mafanikio.

“Nahitaji nafasi ya kikosi cha kwanza Simba, najua makipa waliopo ni wazuri lakini ili upate nafasi lazima uwe na kitu cha ziada kuzidi mwingine natambua hilo na ndio sababu nimejiongeza kwenye mazoezi,” alisema Dida.

Alisema ana ratiba ya kufanya mazoezi binafsi ufukweni na mtaani anakoishi lengo ni kupata nafasi ya kucheza muda wote katika kikosi cha Simba.

“Kikosi cha Simba msimu huu ukiteleza kidogo umeachwa, kila idara imekamilika, upande wetu makipa ndiyo usiseme kuna watu wanadhani mimi na Dida ndiyo tunachuana lakini Nduda naye yuko moto kweli kweli,” alisema Manula.

Ubora wa makipa hao umewaibua wakongwe Mohammed Mwameja na Peter Manyika ambao kila mmoja amechambua uwezo wao huku wakisisitiza yeyote ana sifa ya kuwa kipa namba moja Simba.

Manyika alisema Manula amepata mtu wa kumpa presha, hivyo hawezi kubweteka kwa kuwa atahofia kupokwa namba na Dida anaweza kuwa chaguo la kwanza Simba na Taifa Stars.

“Makipa wote wawili nawafahamu vizuri, uchezaji wao unalingana lakini Dida ni mtu wa kujituma sana hasa anapotaka nafasi, ana nidhamu ya kazi ni mtu wa kupambana,” alisema Manyika.

Mwameja alisisitiza msimu ujao utakuwa wa ushindani kwa makipa hao na huenda wakagawana mechi kucheza sawa kulingana na mazingira.

“Ni makipa wenye ushindani, Manula bila shaka hatakubali kushuka na Dida atapambana ili kuwa juu, kitendo ambacho kitaongeza ushindani zaidi na hata nafasi ya mmoja kumuweka benchi mwingine itategemea na hali ya kiafya lakini sio kiwango,” alisema Mwameja.