Mastaa Yanga wamtisha mzungu wa Gor Mahia

Muktasari:

  • Kerr aliyeiongoza Gor Mahia kufuzu hatua hiyo baada ya kuitoa Supersport United ya Afrika Kusini kwa faida ya bao la ugenini, aliinoa Simba msimu 2015/2016.

Kitendo cha Yanga kupangwa kundi moja na Rayon Sports ya Rwanda na Gor Mahia ya Kenya kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, kitawarudisha nchini kiungo Pierre Kwizera na kocha Dylan Kerr.

Kerr aliyeiongoza Gor Mahia kufuzu hatua hiyo baada ya kuitoa Supersport United ya Afrika Kusini kwa faida ya bao la ugenini, aliinoa Simba msimu 2015/2016.

Kocha huyo raia wa Uingereza alisema mchezo dhidi ya Yanga utakuwa mgumu kwa kuwa ina kikosi bora cha ushindani.

“Nina furaha kurejea Tanzania. Watu wake ni wakarimu wanapenda soka, naamini mashabiki watanipokea vizuri kwasababu sikuwahi kuwa na tatizo nao,”alisema Kerr.

Kwizera na Kerr waliwahi kuitumia klabu ya Simba inayoshiriki mashindano ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Hii itakuwa mara ya pili kwa wawili hao kutua Tanzania tangu walipoachana na Simba mwaka 2014 na 2016, baada ya mikataba yao kuvunjwa na uongozi wa klabu hiyo.

Kwizera aliyekuwa akicheza nafasi ya kiungo alicheza Simba miezi mitano baada ya kusajiliwa Agosti 2014 kabla ya kutemwa Desemba na nafasi yake kujazwa na beki Murshid Juuko raia wa Uganda.

Kiungo huyo ni tegemeo Rayon Sports iliyopangwa na Yanga katika Kundi D na anatarajiwa kuwemo katika kikosi kitakachoteremka uwanjani Mei 16.