Mwameja: Ushindi wa Simba kwa Nkana upo kwa Manula

Dar es Salaam. Kipa wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Mohamed Mwameja ‘Tanzania One’, amesema nafasi ya Simba kusonga mbele katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Nkana Rangers ya Zambia ipo mikononi mwa kipa, Aishi Manula.

Simba itacheza mechi ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Nkana ugenini Desemba 15, kabla ya kurudiana wiki moja baadaye Dar es Salaam, mshindi wa jumla atafuzu hatua ya makundi, ile itakayoshindwa itacheza hatua ya mtoano ya Kombe la Shirikisho.

Akizungumza na gazeti hili jana, kuelekea mchezo huo, Mwameja mmoja wa makipa mahiri kuwahi kutokea nchini, alisema kwa mtazamo wake Simba inao uwezo wa kushinda mchezo huo.

Mwameja alionya sehemu pekee inayompa wasiwasi ni kwa Manula ambaye anaonekana kuwa na wasiwasi muda mwingi wa mchezo kiasi cha kufungwa mabao rahisi katika kona, krosi na mipira ya adhabu.

Mwameja alisema anajua hilo linatokana na wasiwasi na kushindwa kuzungumza na kuwapanga wachezaji wake kwa haraka wakati faulo au kona inapoelekezwa langoni kwake.

Alisema ikiwa Manula ataepuka kufungwa mabao ya kona, mipira ya mbali pamoja na krosi ambayo yanaonekana kuwa changamoto kwake anaipa nafasi kubwa Simba ya kuibuka na ushindi kutokana na ubora wa kikosi chake.

“Unajua mafowadi hivi sasa wako vizuri kwa mashuti ya mbali hawakosei, ni wajibu wa kipa tu kuwa makini, hata Manula cha kwanza asikilize maelekezo ya kocha, pia aongeze umakini ndani ya 18 na azungumze sana na mabeki wake, hiyo ndiyo itakayomsaidia,” alisema Mwameja.

Kipa huyo mkongwe nchini alisema amemfuatilia mara nyingi Manula na kubaini anafungwa mabao kwa makosa yale yale kila mara, hivyo anamshauri kipa huyo ahakikishe hapotezi kujiamini kwake pale anapoaminiwa na kocha.

“Kikubwa kwa Manula ni kujiamini tu na kufuata maelekezo ya kocha, kwani hivi sasa yeye siyo kipa namba moja wa Simba tu bali hata Taifa Stars ndiye kipa tegemeo, hivyo atulie na kuhakikisha makosa hayajirudii,” alisema.

Kitu kingine alichoshauri Mwameja katika mchezo huo wa wikiendi hii ni kuwataka wachezaji wote kuwa makini katika kuzitumia nafasi watakazozipata dhidi ya Nkana, ili kujiwekea mazingira rafiki katika mchezo wa marudiano utakaopigwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, wiki moja baadaye.

Mwameja alisema anaunga mkono mfumo wa kocha Patrick Aussems wa kusaka ushindi akiwa ugenini badala ya kujilinda kwani kwa mbinu hiyo hata timu ikikosa ushindi inakuwa na nafasi kubwa ya kupata sare na kama ni kupoteza sio kwa idadi kubwa ya mabao.

“Kwenye mechi za kimataifa kufungwa mabao mawili au zaidi ni mtihani kwenye mechi ya marudiano, lakini sina shaka kwa mabeki wa Simba, naamini watakuwa makini na kufuata maelekezo ya kocha ili wasiruhusu mabao,” alisema.

Alisema kwa jinsi alivyokiona kikosi cha sasa cha Simba, kila idara imekamilika, cha msingi ni wachezaji kufuata maelekezo ya benchi la ufundi na kutulia kama walivyofanya kwenye mchezo wa raundi ya awali dhidi ya Mbabane Swallows ya Swaziland.

Katika hatua nyingine uongozi wa Klabu ya Simba umeandaa utaratibu kwa wanachama, mashabiki wao pamoja na Watanzania kwa ujumla watakaopenda kwenda Zambia kuishangilia timu hiyo.

Katika utaratibu huo limeandaliwa basi maalumu kwa nauli ya Sh 130,000 kwa kila mmoja kwenda hadi Kitwe, Zambia na kurudi Dar es Salaam, mwisho wa kujiandikisha na kulipa kwa anayehitaji kusafiri itakuwa kesho jioni, ambapo msafara huo utaondoka Dar Alhamisi.