Mzee Ngassa afunguka mwanaye kutua Yanga

Muktasari:

  • Ngassa ambaye alikuwa katika klabu Ndanda ambayo ilinusurika kushuka daraja msimu uliopita dakika za mwisho, amejiunga na Yanga kwa kandarasi ya miaka miwili kuitumikia msimu ujao.

BAADA ya Straika Mrisho Ngassa kumwaga wino kwenye klabu yake ya zamani ya Yanga, baba mzazi wa mchezaji huyo, Khalfan Ngassa amempa neno zito katika kazi yake ya soka.

Ngassa ambaye alikuwa katika klabu Ndanda ambayo ilinusurika kushuka daraja msimu uliopita dakika za mwisho, amejiunga na Yanga kwa kandarasi ya miaka miwili kuitumikia msimu ujao.

Baba Ngassa alisema kuwa mchezaji huyo anapaswa kuitumia vyema nafasi hiyo ili kufikia malengo ambayo alikuwa anayahitaji katika maisha yake.

Alisema kuwa kutokana na mwanaye huyo kutegemea zaidi soka, hapaswi kusikiliza porojo za vijiweni badala yake aangalie anachokifanya kwa faida yake.

 

"Lazima ajitambue kuwa hiyo ndio kazi yake hivyo awe makini na nafasi hiyo kufikia malengo yake na asisikilize maneno ya vijiweni," alisema Ngassa.

Aliongeza kuwa Straika huyo kiwango chake kilikuwa kimeshuka kutokana na kuchezea timu ambayo hakuwa na mapenzi nayo,hivyo kutua Yanga kutaibua morali yake na atafanya vizuri.

Alisema kuwa iwapo atapambana uwezekano wa kukipiga tena kimataifa upo kwani uwezo anao katika kusakata kandanda na ana nidhamu ya hali ya juu.

"Uwezo anao licha ya kwamba mapema kiwango chake kilishuka kutokana na kucheza soka kwenye timu ambayo haikuwa chaguo lake,lakini kutua Yanga morari itaamka na atafanya vizuri" alisema Baba huyo Mzazi.