Ninje: Wachezaji tatizo Kili Stars

Muktasari:

  • Tanzania Bara mara ya mwisho kuchukua ubingwa wa Chalenji ilikuwa 2010 jijini Dar es Salaam.

Wakati ‘watalii’ wa Tanzania Bara, ‘Kilimanjaro Stars’ walirejea nchini jana, jina la timu hiyo limepata umaarufu usiotarajiwa na wadau wa michezo.

Matokeo mabaya iliyopata Kilimanjaro Stars yamewachukiza wadau wa michezo na kila mmoja kwa nafasi yake amekuwa akiizungumzia vibaya baada ya kuboronga katika mashindano ya Kombe la Chalenji.

Wadau wa soka wanaopatikana kwenye ‘vijiwe’ mbalimbali wamepaza sauti kuonyesha hasira zao dhidi ya Kilimanjaro Stars ambayo iliaga kwa aibu katika mashindano hayo yanayoendelea nchini Kenya.

Baadhi ya wadau wamekuwa wakitoa maoni tofauti, wakimtwisha zigo la lawama kocha wa timu hiyo Ammy Ninje wakidai hana uwezo na wengine wamelishutumu Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambao ndio waajiri wake.

Kilimanjaro Stars ilikamilisha ratiba ya mashindano kwa kuchapwa bao 1-0 na Kenya ‘Harambee Stars’ katika mchezo wa Kundi A uliochezwa juzi jioni kwenye Uwanja wa Kenyatta, Machakos.

Timu hiyo ilianza kwa kutoka suluhu na Libya, ililala mabao 2-1 dhidi ya Zanzibar Heroes, ilichapwa 2-0 na Rwanda ‘Amavubi’. Kilimanjaro Stars iliambulia pointi moja katika mechi nne ilizocheza.

Ninje amebebeshwa mzigo wa lawama akidaiwa uteuzi wake ulikuwa wa kutia shaka kutokana na rekodi yake tangu akiwa ‘mchezaji’ hadi kocha wa Kilimanjaro Stars.

Kocha huyo alipewa kazi ya kuinoa Kilimanjaro Stars ikiwa ni mara yake ya kwanza kufundisha soka nchini. Ninje hakuwahi kufundisha timu yoyote kabla ya kuibukia Taifa Stars akiwa msaidizi wa Salum Mayanga.

Ninje atema cheche

Baada ya shutuma nyingi kuelekezwa kwake, Ninje ameibuka na kudai amefanya kazi kubwa, lakini wachezaji walimuangusha kwa kukosa umakini.

Alisema wachezaji wa Kilimanjaro Stars walicheza kwa mazoea siyo kuiwakilisha nchi kama ilivyokuwa kwa ndugu zao Zanzibar Heroes.

“Nawapongeza wachezaji wa Zanzibar Heroes walicheza kwa nguvu, kujituma na walionyesha kabisa wanapambana kwa ajili ya taifa lao,” alisema Ninje kuhusu tofauti ya wachezaji wake na timu hiyo.

Ninje alisema wachezaji wa timu ya Taifa wanatakiwa kuandaliwa kiakili na kisaikolojia kujua maana ya uzalendo kwa kuwa amebaini ‘nyota’ hao hawakujituma kwa niaba ya Watanzania.

Pia, alidai wachezaji wa timu ya Taifa wanatakiwa kuchaguliwa kutokana na ubora, nidhamu na kuzingatia maisha wanayoishi ndani ya jamii kwa kuwa baadhi yao amebaini hawana uzalendo.

Makocha wafunguka

Wakati Ninje akitoa sababu lukuki za Kilimanjaro Stars kuboronga, Katibu Mkuu wa Klabu ya Yanga, Charles Mkwasa, alisema timu ya Taifa inaweza kufanya vibaya katika mashindano ya kimataifa kutokana na sababu tofauti ikiwamo mazingira au mfumo wa ufundishaji.

Mkwasa, aliyewahi kuzinoa timu za Taifa kwa nyakati tofauti, alidokeza mfumo unaotumika unaweza kuwa kikwazo kwa mchezaji au wachezaji kushindwa kuumudu.

“Mazingira ya mchezaji alivyokulia tangu akiwa mdogo kabla ya kuanza kucheza soka ya ushindani yanaweza kumuathiri kwa namna moja au nyingine,” alisema kocha huyo wa zamani wa Yanga.

Kocha wa Dodoma FC, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ licha ya kumlaumu Ninje lakini amewataka wachezaji wa timu ya Taifa kuweka mbele maslahi ya nchi kama Zanzibar Heroes.

“Wachezaji wetu lazima wajitoe ili kupata mafanikio, waige kwa wenzao Zanzibar ambao wanajitolea sana wanapotaka kushinda, bila kujitoa hawawezi kufika kokote,”alisema Julio.

Naye kocha wa Tanzania Prisons, Abdallah Mohammed alidai wachezaji wa Kilimanjaro Stars wanastahili kubeba lawama kwa kucheza chini ya kiwango katika mashindano hayo.

Mohammed alisema amefuatilia mashindano hayo na kubaini wachezaji wa timu hiyo walishindwa kuweka mbele uzalendo wakiamini kwamba wameitwa kwa bahati mbaya timu ya Taifa.

“Wachezaji hawakulipigania Taifa, ari ya kujituma haikuwepo na baadhi yao walionekana wavivu, wachache waliojitolea kucheza kwa nguvu walivunjika moyo,”alisema kocha huyo.

Mrange Kabange, kocha wa Njombe Mji alisema wachezaji wa timu hiyo walionyesha udhaifu wa kutokujituma katika mechi zote walizocheza katika mashindano.

Hata hivyo, alisema Kilimanjaro Stars iliwekwa kambini muda mfupi kulingana na mazingira hatua iliyomnyima kocha fursa ya kuwapa wachezaji dozi ya kutosha.

“Uwezo wa kushindana kimataifa hatuna hata aje kocha gani, pia moyo wa kujituma kwa wachezaji wetu haupo tumeona kila mmoja anacheza kivyake.Tunaweza kumlaumu kocha ni sawa, lakini tumeangalia uwezo wa wachezaji wetu? hawajitumi,”alisema Kabange.

Kocha wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila alisema katika uchunguzi wake amebaini idadi kubwa ya wachezaji wana tatizo la kisaikolojia ambalo limekuwa sugu ndani ya vichwa vyao.

Alisema Tanzania ina wachezaji hodari, lakini wameathirika kisaikolojia hatua inayowanyima fursa ya kuonyesha ubora wao katika mashindano mbalimbali.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar na Taifa Stars, alisema tatizo hilo limechangia wachezaji wengi kutokuwa na nidhamu ya mchezo.

“Naweza kuifananisha Kilimanjaro Stars na Kagera Sugar ambayo ina wachezaji wazuri, wazoefu lakini haipati ushindi. Hayo ni matokeo ya kutokuwa na nidhamu ya mchezo,”alisema Katwila.

Kocha Msaidizi wa Yanga na nahodha wa zamani wa Taifa Stars, Shadrack Nsajigwa alisema huenda Kilimanjaro Stars imeboronga katika mashindano hayo kutokana na mazingira.

“Unajua ni ngumu kidogo kulizungumzia suala la wachezaji, lakini mazingira ya kule sijui yalikuwa vipi, ningefahamu hilo ningeweza kulizungumzia vizuri,” alisema Nsajigwa kwa ufupi.

Naye kocha wa kituo cha kuendeleza vipaji vya soka kilichopo Kimara, Dar es Salaam Joseph Zumba Kilimanjaro Stars ilicheza vibaya mechi zote kwa kuwa kila mchezaji alicheza kivyake na aliipongeza Zanzibar Heroes kwa mchezo mzuri.