Rais wa Soka Ufaransa ashangaa yaliyotokea Hispania

Muktasari:

Rais huyo amesema kutokana na uhusiano mzuri alionao na kocha wa timu ya taifa na benchi lake la ufundi, tukio kama hilo haliwezi kutokea kwa timu ya Ufaransa.

Matukio yaliyosababisha kutimuliwa kwa kocha wa timu ya taifa ya Hispania, Julen Lopetegui siku moja kabla ya kuanza kwa fainali za Kombe la Dunia, hayawezi kutokea Ufaransa, kwa mujibu wa kiongozi wa soka wa nchi hiyo.

Rais wa Chama cha Soka cha Ufaransa, Noël Le Graët amesema kutokana na uhusiano mzuri alionao na benchi la ufundi, ni vigumu tukio kama hilo kutokea.

Rais wa Shirikisho la Soka la Hispania (RFEF), Luis Rubiales alilazimika kupanda nde juzi (Jumatano) asubuhi kurudi nchini kwake kutangaza kumtimua Lopetegui baada ya kutangazwa kuwa kocha mpya wa Real Madrid.

Real Madrid haikufanya mawasiliano yoyote na RFEF wakati ikijadiliana na Lopetegui, ambaye alisaini mkataba wa kuifundisha Hispania hadi mwaka 2020, na badala yake ikamtaarifu rais huyo dakika tano kabla ya kumtangaza kocha huyo mpya.

Lakini La Graet amesema hilo haliwezi kutokea Ufaransa.

"Nchini Ufaransa, haiwezekani kwa sababu ya uhusiano nilionao na (kocha wa timu ya taifa) Didier (Deschamps) na wenzake," alisema rais huyo.

"Haiwezekani. Nadhani kitu kibaya kwa rais wa shirikisho la Hispania ni kwamba alipata habari hizo dakika tano kabla ya mkutano na waandishi wa habari, na hatuwezi kusema hilo ni jambo zuri.

"Ulikuwa ni uamuzi wake, haukuwa rahisi. Kubadili makocha saa 48 kabla ya mechi muhimu, kwa sababu watacheza na Ureno, si kitu rahisi. Si kitu rahisi kwa Wahispania, lakini wana timu nzuri na kimbinu ni wazuri."

Kocha huyo anatarajiwa kutambulishwa wakati wowote leo.