Serikali yaingilia kati sakata la Wambura

Muktasari:

  • Kamati ya Maadili ya TFF ilimfungia Wambura hivi karibuni baada ya Sekretarieti ya TFF kumshtaki kwenye kamati hiyo kwa makosa matatu ya kimaadili ambayo ni kupokea pesa za TFF isivyo halali, kugushi na kushusha hadhi ya TFF.

Dar es Salaam.Siku chache baada ya Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Michael Wambura kufungiwa maisha kujihusisha na masuala ya soka na Kamati ya Maadili ya shirikisho hilo, Serikali imetaka maelezo ya sakata hilo zima.

Kamati ya Maadili ya TFF ilimfungia Wambura hivi karibuni baada ya Sekretarieti ya TFF kumshtaki kwenye kamati hiyo kwa makosa matatu ya kimaadili ambayo ni kupokea pesa za TFF isivyo halali, kugushi na kushusha hadhi ya TFF.

Habari kutoka ndani ya TFF zimepasha kuwa Serikali kupitia Baraza la Michezo la Taifa, (BMT) limeipa shirikisho hilo barua ikitaka ufafanuzi wa sakata zima la Wambura pamoja na mchakato wa ajira ya Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao.

Rais wa TFF, Wallace Karia alikiri kupokea barua ya Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo ikitaka maelezo juu ya suala la kufungiwa maisha kwa makamu wa rais huyo wa TFF.

Karia alisema, taarifa hizo hazitaishia Wizarani bali watazipeleka hata Shirikisho la Soka Afrika, CAF na lile la Kimataifa, (Fifa).

“Ni kweli Wizara ilituuliza juu ya suala hilo, tumewajibu namna lilivyokuwa hadi kusimamishwa Wambura,” alisema Karia.

Habari zaidi kutoka TFF zimelidokeza Mwananchi kuwa, Serikali ilipinga mchakato uliotumika kumsimamisha Wambura na kutompa nafasi ya kumsikiliza hata kama amekosea na ndiyo maana ilitaka maelezo hayo.

“Ilichokitaka Serikali ni kufahamu kama utaratibu mzima wa kumsimamisha Wambura ulifuatwa na ilisema kama kakosea bado alikuwa na haki ya kusikilizwa,”

Mbali na hayo, Kifungu cha tano (d) cha ibara ya 31 ya Katiba ya TFF, inayofafanua juu ya muundo wa Kamati ya Utendaji, kinazuia mjumbe yeyote wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho hilo kung’olewa kwenye nafasi yake kwa makosa ya jinai ambayo hayajathibitishwa.

Hata hivyo, Karia alisema jana kwamba Wambura atasikilizwa kwani ni haki yake na tayari amekata rufaa kupinga hukumu yake.

Wakati hayo yakiendelea, Mwananchi limedokezwa kuwa, mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Athuman Nyamlani ndiye anapigiwa chapuo la ‘kuvaa viatu’ vya Wambura TFF.

Chanzo hicho cha kuaminika kilidokeza kuwa, pamoja na mpango huo, Serikali imeiwekea ngumu TFF katika mchakato huo ikitaka utaratibu ufuatwe.

Hata hivyo, Karia alisisitiza kuwa mrithi wa Wambura TFF atapatikana kwa kuchaguliwa kwenye uchaguzi mdogo utakaopangwa baadaye.

Kuhusu suala la Kidau, Serikali pia imetaka maelezo ya hili na Rais Karia alisema wako kwenye mstari na hawajavunja Katiba ya TFF kwenye mchakato wa kumpata mtu wa nafasi hiyo.

Inaelezwa kuwa Kidau ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF kupitia Tafca kabla ya kuteuliwa kuwa kaimu katibu mkuu hatua inayoelezwa kuwa ni kinyume na Katiba ya TFF.

Katiba ya TFF kifungu cha 41 (3) kinasema waajiriwa wa TFF akiwemo katibu mkuu hatakiwi kuwa mjumbe wa chombo chochote ndani ya TFF kwa, aidha kuteuliwa au kuchaguliwa.

“Taarifa za kukiukwa Katiba zinaenezwa na baadhi ya watu, lakini TFF haijakiuka kwani Kidau kwanza hajaajiriwa TFF tumemuomba tu akaimu, lakini tayari alishaachia ngazi Tafca,” alisema Karia.

Alisema hata ikitokea Kadau akawa Katibu Mkuu wa TFF, bado hawajavunja Katiba ya TFF kwa kuwa si Mwenyekiti wa Tafca kwa sasa.