Msuva amfuata Samatta Algeria

Muktasari:

  • Msuva ni miongoni mwa wachezaji Saba wa Taifa Stars ambao walitajwa kuungana na wenzao nchini Algeria  kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa kirafiki dhidi ya wenyeji wao keshokutwa Alhamisi.

Mshambuliaji wa Kitanzania, Saimon Msuva anayeichezea Difaa El Jadida, ameanza safari asubuhi ya leo Jumanne kutoka Morocco kuelekea nchini Algeria kwa ajili ya kujiunga na kikosi cha Taifa Stars.

Msuva ni miongoni mwa wachezaji Saba wa Taifa Stars ambao walitajwa kuungana na wenzao nchini Algeria kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa kirafiki dhidi ya wenyeji wao keshokutwa Alhamisi.

“Baada ya kutoka, Congo na kuwasili hapa, Morocco salama ni muda wa kwenda kujiunga na wenzangu, Algeria,” alisema Msuva.

Nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta aliwasili jana Algeria akitokea Ubelgiji kwenye klabu yake ya KRC Genk.

Wachezaji wengine wa Taifa Stars ambao walitajwa kujiunga Na wenzano nchini humo ni Rashid Mandawa wa BDF XI  ya Botswana na Shiza Kichuya, Erasto Nyoni,Shomari Kapombe na Aishi Manula wa Simba.