TFF yatishia kuwashtaki waliowachafu

Muktasari:

  • Viongozi wa shirikisho hilo wameshutumiwa kwa matumizi mabaya ya fedha katika mitandao ya kijamii

Dar es Salaam. Shirikisho la Soka Tanzania (TFF)  limetangaza kuwachukulia hatua  za kisheria waliosambaza ujumbe wa kuwachafua kwenye mitandao ya  kijamii.

Kaimu Katibu Mkuu wa shirikisho hilo, Wilfred Kidao alisema rais wa TFF, Wallace Karia ameshambuliwa katika mitandao ya kijamii kwa ujumbe unaoonyesha namna uongozi huo ulivyo na matumizi mabaya ya fedha kwenye mishahara na vikao vyao.

"Huo ujumbe uliosambaa hauna ukweli ndani yake hata kidogo, hatuji aliyeandika na kusambaza ujumbe huo alikuwa na lengo gani na taasisi, tunapenda kukosolewa, lakini iwe kwa mambo ambayo yanauhakika ndani yake.

"Tulichokiamua ni kuwashughulikia wale ambao wameamua kuichafua hii taasisi ambayo tupo kwenye jitihada ya kuiweka kwenye hadhi yake, haya mambo yanatufanya kuwa katika wakati mgumu tunaweza hata kupoteza wadhamini wetu.

"Uzuri kunasheria za mitandao hivyo hatutapata shida kabisa nimempa kazi ya kufanya mwanasheria wetu, kuna majina kama kumi ambayo tumeyapata hayo tutaanza nayo," alisema.

Hata hivyo Kidao aliongeza kwa kusema wamekuwa wakifanya mambo yao kwa uwazi na ndiyo maana wameboresha posho za wachezaji wa timu ya Taifa na kutumia fedha nyingine  kwenye  maendeleo ya mpira moja kwa moja na sio kujinufaisha wao wenyewe.