Tshishimbi yamemkuta

HUKO Yanga bado mambo hayapoi, kwani wakati nyota wa timu hiyo wakitimka zao kwenda Ruangwa mkoani Lindi kwa mwaliko maalumu wa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kiungo fundi Papy Kabamba Tshishimbi yamemkuta mazito huko.

Tshishimbi hali yake bado tete na ameachwa jijini Dar es Salaam huku Mwenyekiti wa Usajili wa klabu hiyo, Hussein Nyika akifunguka ishu nzima ya kikao chao na Kamati ya Uchaguzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Hata hivyo, wakati Nyika akianika kilichotokea kwenye kikao chao juu ya mustakabali wa uchaguzi wao na hasa nafasi ya Mwenyekiti wao, Yusuf Manji, Mwanaspoti limepenyezewa Yanga wataitumia ziara kwa Waziri Mkuu kwenda kuishtaki TFF.

Kwa mujibu wa Mratibu wa Yanga, Hafidh Saleh, Yanga ilitimka alfajiri ya jana Jumamosi na kikosi cha nyota wake wote isipokuwa wachezaji wanne waliopo Taifa Stars na timu ya Taifa ya Vijana U23 na wengine wenye matatizo ya kiafya, akiwamo Tshishimbi ambaye hali yake bado tete.

Akizungumza na Mwanaspoti, Hafidh alisema Yanga leo Jumapili itaumana na Namungo FC iliyopo Daraja la Kwanza ikiwa ni mchezo wao wa tatu wa kirafiki kujiandaa na viporo vyao vya Ligi Kuu Bara dhidi ya Mwadui FC na Kagera Sugar.

Alisema Tshishimbi ameachwa sambamba na Juma Mahadhi na Burhan Akilimali kutokana na kukabiliwa na matatizo ya kifundo cha mguu.

“Tshishimbi alianza mazoezi mepesi lakini kwa mujibu wa daktari hajatakiwa kusafiri kwa kuwa bado anatakiwa kuendelea kuangaliwa hivyo, tumemwacha nafikiri hadi tukirudi kama atakuwa salama tunaweza kusafiri naye tayari kwa michezo yetu ya viporo,” alisema Hafidh.

Mratibu huyo alisema pamoja na kukosekana kwa nyota huyo, bado nafasi yao ya kufanya vizuri katika mchezo huo ipo palepale kwani wana nyota wengi wanaoweza kucheza nafasi ya kiungo akiwemo chipukizi Maka Edward.

“Kuna Rafael Daud na Maka wote wanacheza kiungo, ndio tuliowatumia michezo miwili ya kirafiki tuliyocheza dhidi ya Reha na African Lyon, hata mchezo huu pia tunaamini tutafanya vizuri,” alisema.

NYIKA AFUNGUKA

Katika hatua nyingine wanachama na mashabiki wa Yanga wamesikia uamuazi wa TFF kupitia Mwenyekiti wake wa Kamati ya Uchaguzi, Malangwe Ally Mchungahela lakini bosi wao mmoja ameibuka na kuishangaa TFF.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Nyika alisema wao kama wajumbe wa Kamati ya Utendaji hawataki kupingana wala kusumbuana na serikali, lakini kikao cha juzi hakikuisha kwa maafikiano tofauti na kilichotangazwa na Kamati hiyo ya TFF.

Nyika ameliambia Mwanaspoti kuwa TFF walionekana mapema kuja na maagizo yao hata kabla ya wao kuwasilisha hoja zao na kila walichokileleza walipingana nacho.

Mjumbe huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano alisema, wanaiheshimu TFF na hata wao wanahitaji uchaguzi, lakini haoni kama itakuwa rahisi kwa wanachama wao kukubaliana na suala la nafasi ya Mwenyekiti wao, Yusuf Manji nafasi yake kugombewa wakati yupo.

“Sisi ni wajumbe wa kamati ya utendaji na mabosi wetu ni wanachama sasa wao hawataki kusikia Manji anaondolewa, TFF inaweza kutusaidia kwa kufika katika mkutano mkuu kisha kuwaelewesha wanachama wakikubali na sisi tutashukuru.

“Kikao wakati kinaendelea nililazimika kumwita faragha mwenyekiti Mchungahela na nikamwambia kwa jinsi kikao kinavyokwenda hakutakuwa na mwafaka ni vyema afute mpango wake wa kutangaza maamuzi waliyokuwa tayari kufanya hivyo.”

KESI KWA MAJALIWA

Habari kutoka ndani ya Yanga zinasema mabosi wa klabu hiyo wamepanga kumshtakia Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa juu ya kinachoendelea katika mchakato wa uchaguzi wao, wakisisitiza wanaamini kiongozi huyo kama mwanamichezo ataweka mambo sawa na Yanga itaendelea kutulia.

“Tukiwa Ruangwa tutazungumza na Waziri Mkuu, juu ya kinachofanywa na TFF na Kamati ya Uchaguzi, wakati TFF hao hao walitangaza kumtambua Manji, lakini leo wanalazimisha nafasi yake igombewe,” chanzo cha kuaminika ndani ya Yanga likidokeza Mwanaspoti.