Yanga wamrudia Domayo

Muktasari:

  • Domayo aliichezea Yanga kwa mafanikio ndani ya misimu miwili kabla ya kutua Azam, anatarajia kumaliza mkataba wake mwishoni mwa msimu huu wa ligi kuu.

MABINGWA wa Ligi Kuu Bara kikosi cha Yanga, kiko mbioni kumrudisha kiungo wao, Frank Domayo 'Chumvi' kikosini mwao.

Domayo ambaye aliichezea Yanga kwa mafanikio kwa misimu miwili kabla ya kutua Azam, anadaiwa kumaliza mkataba wake mwishoni mwa msimu wa ligi kuu.

Mtu wa karibu wa mchezaji huyo amesema: "Yanga imetuma watu kumfuata Domayo ili arudi kikosini kwao lakini mwenyewe bado hajafanya maamuzi ya kwenda huko."

Hata hivyo, Domayo alipoulizwa juu ya taarifa hizo alisema: "Mimi ni mchezaji wa Azam na habari za Yanga hata sizijui, kama zipo mtajua tu niacheni nifanye kazi kwanza."

Domayo mwenye miaka 24,  aliibuliwa na JKT Ruvu mwaka 2012 kabla ya kutua Yanga aliyoichezea kwa

kipindi cha miaka miwili hadi 2014, baada ya hapo alisajiliwa na Azam anayoichezea mpaka sasa.