Harmorapa amjibu Harmonize

Muktasari:

  • Asema hana kinyongo naye

Dar es Salaam. Siku moja baada ya msanii wa bongo fleva, Rajab Abdul maarufu Harmonize kuandika ujumbe mrefu wa kumtaka Athuman Omary ‘Harmorapa’ asikate tamaa, msanii huyo amemjibu akisema dunia ni ‘rangi rangile’ akimaanisha kuwa dunia ni mzunguko.

Harmorapa alipata umaarufu kutokana na kufananishwa na Harmonize, japokuwa katika kipindi chote msanii huyo kutoka lebo ya Wasafi hakuwa akikubaliana na hilo mpaka jana, Julai 24, 2018 alipoandika ujumbe huo kupitia ukurasa wake wa Instagram wa kumpa moyo kwa kumuita pacha wake.

Ujumbe huo uliambatana na picha ya wawili hao ambao kimuonekano wanafanana na kimitindo ya nywele, huku wachangiaji wakimsifu Harmonize kwa kumtia moyo Harmorapa.

Harmonize aliandika “mwiko kukata tamaa ama kukatishwa na mtu yeyote yule katika safari yako ya mafanikio hii, safari ni ndefu sana…!!! Utakutana na changamoto nyingi mno yakiwemo matusi, dharau, uonevu, chuki na mengine kibao.”

 

“Ila pale utakapokubali kukata tamaa ama kukatishwa utakuwa umewavunja moyo watu wengi sana, (1) familia yako ,(2) ndugu jamaa na marafiki (3), hata wale wachache waliokuwa wanakutia moyo na motisha uongeze jitihada na wengine wengi mno...Itakuwa umewavunja moyo...!!

 

“Lakini pia M/Mungu ni wa ajabu na hajawahi kukosea katika hii dunia, kila alifanyalo lina maana kubwa sana…!!! Kawaumbe binadamu wengine kwa mfano wako nikiwa na maana mnafanana ambalo ni jambo la heri na baraka,” unasomeka ujumbe huo.

 

Hamornize anaendelea kusema, “so ukikata tamaa nao pia utakuwa umeangusha jitihada zako, maarifa, kuzishinda changamoto ndio njia pekee inaweza kuleta faraja kwa wengi wanaokuzunguka, zingatia hili, maisha ni kombolela...!!! God bless my twin brother.”

 

Akizungumza na MCL Digital kuhusiana na ujumbe huo, Harmorapa amesema anachoamini dunia inazunguka na huwezi kujua wakati msanii huyo kutoka kundi la Wasafi anamponda alikuwa katika hali gani.

 

Amesema kilichomfanya msanii huyo kumwandikia maneno ya kumpa moyo ni kutokana na kuona namna gani anaendelea kupambana katika maisha licha ya matusi ambayo anayapata kutoka kwa jamii.

 

“Hata hivyo, mimi nilishamuachia Mungu. Yote aliyokuwa ananisema vibaya sikuwa na tatizo lolote na yeye kwani nilimchukulia ni binadamu na kila binadamu ana matatizo yake,” anasema.

 

“Pia, unaweza ukamfanyia mtu mabaya, halafu siku moja ukakaa ukajirudi kwamba ulichofanya sicho, jambo ambalo naliona kwa Harmonize ndilo lililomtokea, ila aelewe mimi pamoja na yote aliyokuwa anazungumza juu yangu sina kinyongo naye.”

 

Wakichangia ujumbe huo wa Hamornize, wengi wamempongeza ambapo msomaji aliyejiita de_last, amesema, “sijawahi kukubali hata siku moja, ila leo hii umeufanya moyo wangu kuamini kuwa we’ ni miongoni mwa watu ninaowakubali duniani. congratulations bro’ Harmonize.”

 

Naye thatniqqur, amesema, “basi safi...mnafanana ile kishenzi”, huku bignotoriuousDa akisema,  “umenigusaa sanaa Harmo.”

 

Jmattias amesema, “hii imekaa pouwa sana!! Palipo na ushirikiano wa nguvu daima kuna mafanikio, usisikilize f’lani kasema nini utaumia songa mbele na daima utawin.”