Ng’ombe ukimkamua bila kumlisha atakufa tu

Kuna wale wazazi ambao walikwepa majukumu ya kutunza watoto wao. Hawakuwapa elimu nzuri, hawakuwapa maisha mazuri lakini kiubishiubishi watoto wakatoboa katika maisha. Sasa mzazi huyo kwa kujisifu kuhusu mwanaye, utashangaa.

Ukweli ni kwamba haki ya kuwa mzazi si kumleta tu kiumbe duniani, inajumuisha kumpa haki zake za msingi. Ukikwepa majukumu yako haki yako inapotea. Habari ndiyo hiyo!

Kuna wafugaji wanaohesabu lita za maziwa kila asubuhi na jioni. Mfugo wake umekunywa maji, umekula hiyo haimuhusu. Unadhani mfugo huu utakuwa na maisha marefu au utampa maziwa ya kutosha?

Juzi kati kulikuwa na zogo kuhusu tozo za wasanii wanapofanya kazi zao. Si ajabu kusikia sanaa inatozwa. Dunia kote haya yanafanyika na ni moja ya sekta yenye fedha nyingi kweli kweli.

Lakini sanaa pamoja na kuwa inatokana na vipaji, mafanikio yake hayadondoki kutoka mbinguni. Kuna mipango na kuna uwezeshaji uliofanyika ili iwape fedha.

Kama ambavyo baba anamtunza mwanaye na kumpa elimu nzuri, kama mfugaji anavyolisha mifugo yake, ndivyo sanaa inavyostawishwa.

Kabla mamlaka zetu hazijaanza kutaka kodi kutoka kwa Billnas na Maua Sama, zijiulize zimemfanyia nini huyu msanii au hii sanaa.

Haiwezekani watendaji wakae vitini ofisini wakizungukazunguka kusubiri msanii atoboe kama Mangi anayesubiri wateja asiowafahamu.

Maisha ya wasanii ni ya kuunga unga tu. Diamond, Alikiba, Vanessa Mdee na wengine wanapitia changamoto nyingi kabla ya kufika walipo. Pengine baba angekuwa anafanya kazi yake sawasawa, vilio visingekuwapo au tungekuwa na wasanii kama hawa wengi kwa sababu wengi wanaishia njiani na tunawajua.

Matatizo yanayowapata wasanii ni taswira ya sanaa halisi. Yaani maisha wanayoishi ni tofauti na uhalisia kwa kuwa mengi yamejaa kujikweza na hii ni kujitofautisha na mashabiki au wasanii wenzao.

Wasanii wana njaa kuliko mamlaka zinazotaka kuwatoza ada, hivyo muhimu ni kuwatatulia kero zao, kuwatengenezea mazingira ya kupata fedha nyingi kabla ya kutaka kuzichota.

Vyuo vya sanaa, majumba ya sanaa, maonyesho yanayoratibiwa na mamlaka hizo au kuwezeshwa yapo wapi?

Kama Serikali imepiga hesabu ikaona kuna hela nyingi kwenye hizo tozo, basi iwekeze. Isitake kuwa kama baba au mfugaji niliyemtolea mfano hapo juu. Nimemaliza.