Zawadi ya studio inavyomrahisishia Linah kazi zake

Unaweza kupewa zawadi yoyote na mpenzi wako, lakini ukweli ni kwamba haiwezi kufikia thamani kama ile ambayo inakurahishia kufanya shughuli yako unayotegemea kuendeshea maisha.

Hii ilimtokea Linah, msanii wa Bongo Fleva kutoka THT, wakati wa kumbukumbu yake ya kuzaliwa mwaka jana wakati mzazi mwenzake alipomzawadia studio!

“Unajua kuna wanaume wakishakumiliki hata kazi uliyokuwa unaifanya wanataka uiache, lakini sio kwa baba Tracy Paris,” anasema Linah akimzungumzia baba wa watoto wake anayeitwa Shaaban.

“Pamoja na kuwa mshauri kwangu, amekuwa akinipiga tafu (akinisaidia) kuhakikisha nakuwa na vitendea kazi kama studio aliyonizawadia mwaka jana.”

Studio ya Linah, ambaye jina lake la kuzaliwa ni Esterlinah Sanga, iko Mbezi Beach jijini Dar es Salaam.

Katika mazungumzo na Mwananchi, Linah anaeleza jinsi anavyomzimia Shaaban kwa kujali kazi zake.

Lakini Linah anao wajibu kwa mzazi mwenzake ambaye hataki awe anazururazurura.

“Zamani nilikuwa nikijisikia nimewamisi marafiki zangu tu, basi natoka. Na, si unajua tena ubachela hakuna anayekupangia,” anasema.

“Lakini sasa hivi nimekuwa nikitoka kwa sababu (maalum), na huwa namshirikisha baba watoto. Akiona kuna haja ndipo anaponiruhusu.”

Pengine ni kutokana na mzazi huyo mwenza kutotaka azurure, ndipo alipoamua kumzawadia nyota huyo wa “Anatamani” studio hiyo.

“Tangu nipate studio hiyo, imekuwa ikinirahishia kazi wakati napotaka kurekodi nyimbo zangu,” anasema Linah.

“Badala ya kwenda kupanga foleni kwenye studio nyingine, nakodisha watayarishaji na kwenda kupiga nao kazi kwa muda ambao nautaka.”

Pia anasema kwa kuwa bado analea mtoto mdogo, siku hizi kapunguza hata muda wa kurudi nyumbani usiku mwingi.

“Nikichelewa sana ni saa 6:00 usiku na hii inakuwa ni kwa sababu maalumu.”

Anasema akialikwa kutumbuiza inakuwa vigumu kwenda shoo ambazo mara nyingine humalizika usiku mwingi na hivyo kuchelewa kurudi nyumbani.

“Lakini kwa kuwa ndiko kunakonipatia riziki ya kila siku, sina budi kuvumilia. Lakini nahakikisha namuandalia mtoto kila kitu,” anasema Linah.

Akizungumzia kuhusu mipango ya ndoa, msanii huyo anasema bado iko mbali kwa kuwa kwa sasa anapambana kufikia malengo aliyojiwekea katika maisha na pia anataka kuifanya harusi yake kuwa ya aina yake.

Kuhusu mpango wa kuzaa tena, Linah anasema ataendelea kufanya hivyo kwa kuwa amejipangia kuwa na watoto watatu, jambo ambalo anaamini Mungu akipenda litatimia.

Nitasimamia uamuzi wa mwanangu

Linah pia alizungumzia maisha ya baadaye ya mwanae kama atafuata nyayo zake.

“Sijafikiria mtoto wangu awe nani katika maisha yake, bali nitasimamia uamuzi wowote atakaouchukua,” alisema Linah aliyetokea katika nyimbo za injili.

“Hata mimi hakuna aliyenipangia niwe msanii wa Bongo Fleva, bali ni moyo wangu ulitaka japokuwa kulikuwa na vipingamizi vingi kutoka kwa wazazi wangu. Hivyo kwa mwanangu nisingependa kuona hayo yanatokea, badala yake nitaheshimu chochote atakachotaka afanye, ilimradi kisiwe kinavunja sheria ya nchi.

Linah aliyewahi kusajiliwa na kampuni ya Pana Musiq na No Fake Zone za Afrika Kusini, anasema atajitahidi kumlea mtoto wake huyo ili asije kuingia kwenye matatizo ambayo amewahi kuyapitia, matatizo ambayo anasema baadhi yamekuwa magumu kufutika katika fikra zake