#WC2018: Kikosi bora Kombe la Dunia hiki hapa

Muktasari:

Wachezaji hao walichaguliwa tangu mechi ya kwanza ya ufunguzi iliyochezwa Alhamisi iliyopita kati ya Russia dhidi ya Saudi Arabia hadi mchezo wa juzi baina ya Senegal na Poland.

Moscow, Russia. Baada ya kukamilika mechi za raundi ya kwanza ya Fainali za Kombe la Dunia 2018, tayari jopo la wataalamu limefanya uteuzi wa wachezaji waliofanya vyema na kuingia katika kikosi cha kwanza cha dunia ‘Best XI’

Wachezaji hao walichaguliwa tangu mechi ya kwanza ya ufunguzi iliyochezwa Alhamisi iliyopita kati ya Russia dhidi ya Saudi Arabia hadi mchezo wa juzi baina ya Senegal na Poland.

Wachezaji waliochaguliwa ni wale walitoa mchango mkubwa mbali na kung’ara au kufunga mabao katika mechi mbalimbali za raundi ya kwanza.

Kipa: Guillermo Ochoa (Mexico). Ndiye kipa bora katika raundi ya kwanza baada ya kupangua mashuti sita yaliyopigwa na washambuliaji wa Ujerumani.

Ochoa aliisaidia Mexico kupata ushindi wa kushitusha wa bao 1-0 dhidi ya mabingwa watetezi Ujerumani kutokana na umahiri wake.

Mabeki: Jose Gimenez (Uruguay). Katika ushindi wa Uruguay dhidi ya Misri, Gimenez anayecheza beki wa pembeni alikuwa chachu ya mafanikio.

Mchezaji huyo wa Atletico Madrid ya Hispania, sio tu alibana washambuliaji wa Misri, pia alianzisha mashambulizi mengi kutoka pembeni.

Andreas Granqvist (Sweden). Beki huyo wa kati, aliisaidia Sweden kuibuka na ushindi walipocheza na Korea Kusini.

Diego Godin (Uruguay). Mmoja wa mabeki waliokuwa chachu ya ushindi wa Uruguay katika mechi ya ufunguzi.

Licha ya umri wake mkubwa wa miaka 32, Godin alikuwa imara akiwadhibiti vijana wenye kasi wa Misri jambo lililodhihirisha anastahili kuwa nahodha wa kikosi hicho.

Viungo: Eden Hazard (Ubelgiji). Kiungo huyu ‘mpishi’ alithibitisha ubora wake kwa kutengeneza mabao mawili yaliyofungwa na Romelu Lukaku dhidi ya Panama waliposhinda mabao 3-0.

Hazard alikuwa nyuma ya kila mpira timu yao ilipopandisha mashambulizi mbele akisaidia pia kukaba waliposhambuliwa akicheza vyema na Kevin De Bruyne dhidi ya Panama.

Denis Cheryshev (Russia). Wengi walihofia mabadiliko ya mapema kutolewa Alan Dzagoev na nafasi yake kujazwa na Denis Cheryshev katika mchezo ambao Russia ilishinda mabao 5-0 dhidi ya Saudi Arabia.

Hata hivyo, hofu za wengi zilimalizika dakika chache baada ya kuingia kwake kwani Cheryshev aliifungia Russia bao la pili kabla ya kuendelea kuwatesa mabeki wa Saudi hadi kuwalaza kwa mabao 5-0.

Aleksandr Golovin (Russia). Achana na bao la mpira wa adhabu aliofunga dakika za majeruhi, Golovin alitoa pasi za mwisho za mabao mawili ya Russia dhidi ya Saudi Arabia.

Golovin amethibitisha ubira kwa kutengeneza nafasi za kufunga na alikua mwiba mkali kwa vijana wa Saudia.

Isco (Hispania). Kiungo huyu wa Real Madrid amejipambanua ni mmoja wa viungo bora waliopo Hispania kwa sasa.

Ni mchezaji mwenye kasi ingawa kuna wakati alionekana kuchoka walipocheza na Ureno lakini bado alitengeneza nafasi.

Washambuliaji: Romelu Lukaku (Ubelgiji), mshambuliaji huyo wa Manchester United alidhihirisha uwezo wake katika mchezo dhidi ya Panama.

Lukaku aliyechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mechi hiyo ‘man of the match’, alifunga mabao mawili katika ushindi wa Ubelgiji 3-0.

Bao lake la kwanza alipounganisha kwa kichwa cha kuchupia krosi ya Kevin De Bruyne, linamfanya aingie kushindania bao bora la mashindano ya mwaka huu.

Cristiano Ronaldo (Ureno). Nahodha huyo wa Ureno ameingia kwenye kikosi bora cha Dunia, baada ya raundi ya kwanza, kutokana na kazi kubwa aliyoifanya walipocheza na Russia.

Ronaldo alifunga mabao matatu ‘hat trick’ na kuiwezesha Ureno kupata sare ya mabao 3-3, ni wachezaji wachache waliofunga mabao matatu katika historia ya Kombe la Dunia.

Diego Costa (Hispania). Nyota ya mshambuliaji huyo imeendelea kung’ara kimataifa.

Costa sio tu kwamba alifunga mabao mawili wakati wa mechi dhidi ya Ureno, alifanya kazi nzuri kusaka bao la kusawazisha mara mbili katika mchezo huo.