#WC2018: Beckham azitabiri ubingwa England, Argentina Kombe la Dunia

Muktasari:

  • Nyota huyo wa zamani wa Manchester United na Real Madrid amesema mataifa hayo mawili ndiyo yanayoweza kucheza fainali ya mashindano hayo makubwa ya soka yanayoendelea nchini Russia.

Nyota huyo wa zamani wa Real Madrid na Manchester United amesema timu hizo mbili zina nafasi kubwa ya kufika fainali.

 

Beijing. Kwa maneno mengine, unaweza kusema nahodha wa zamani wa England, David Beckham ametabiri ubingwa wa fainali za Kombe la Dunia za mwaka huu utachukuliwa na ama England au Argentina.

Nyota huyo wa zamani wa Manchester United na Real Madrid amesema mataifa hayo mawili ndiyo yanayoweza kucheza fainali ya mashindano hayo makubwa ya soka yanayoendelea nchini Russia.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 43 amesema England inaweza kumudu kuvuka raundi zote hadi fainali ambako itakutana na Argentina, inayoongozwa na Lionel Messi.

"Ninaamini Argentina itacheza dhidi ya England katika fainali," Beckham alisema mbele ya mashabiki nchini China. "Nadhani, ni dhahiri kuwa hili ni chaguo langu kuwa England itakuwa bingwa, lakini hilo ni kutokana na maoni yangu na kuwa mapenzi kwa nchi yangu."

Kwa mujibu wa ratiba, kama Argentina itakutana na England, basi itakuwa katika hatua ya nusu fainali au fainali, kwa hiyo timu hiyo inayoongozwa na nyota wa Tottenham, Harry Kane italazimika kufanya kazi ya ziada kukutana na kikosi cha Messi.

"Nimefurahi sana kwamba tulishinda mechi ya kwanza ya makundi," alisema. "England ni timu inayoundwa na vijana, hawana uzoefu mkubwa na safari ya Kombe la Dunia itakuwa ngumu zaidi kwa sababu kuna timu nyingi nzuri katika mashindano ya mwaka huu."

Beckham alisema hayo alipoendesha klini ya soka ya watoto.

Kuhusu China, Beckham alisema nchi hiyo ina uwezo mkubwa wa kuwa moja ya mataifa makubwa katika soka duniani.

“hapo baadaye, nchi hii itakuwa na nafasi ya kuwa moja ya vigogo katika mchezo huu, lakini inahitaji uwekezaji mkubwa na jitihada kubwa, lakini iko katika mwelekeo sahihi,” alisema Beckham.

Beckham alikuwa katika hafla ya kusaini mkataba baina ya kampuni ya vifaa vya michezo ya Adidas na Shirikisho la Michezo la Shule la China.

Katika hafla hiyo, Beckham alicheza mpira na watoto wanafunzi na kupiga picha nao.