Wanawake Iran watizama soka

Teheran, Iran. Katika kile kinachoonyesha kuwa ni mabadiliko makubwa yanayofanyika hivi sasa katika ulimwengu wa nchi za kiislamu, wanawake nchini Iran juzi waliruhusiwa kuingia uwanjani kuangalia soka.

Hiyo ni mara ya kwanza kwa wanawake nchini Iran kuruhusiwa kuingia viwanjani kutizama soka tangu mapinduzi ya serikali mwaka 1979.

Tangu mwaka huo Serikali zote zilizoongoza nchini Iran kwa nyakati tofauti, ziliwazuia wanawake kuingia uwanjani hivyo ruhusa ya juzi kwenye dimba la Iran stadium lilipokelewa kwa shangwe.

Wanawake walijitokeza kwa wingi na kuujza uwanja wakiangalia timu yao ya Taifa ikicheza mchezo wa pili wa fainali za Kombe la Dunia dhidi ya Hispania, waliofungwa kwa bao 1-0.

Uongozi wa Iran ulitoa ruhusa hiyo baada ya kufurahishwa na matokeo ya mchezo wa kwanza wa timu yao ilipoizamisha Morocco kwa bao 1-0.

Wakishangilia kwa nguvu, wanawake hao waliovalia nguo zinazofanana na bendera za Taifa lao, huku wachache wakiwa na vibendera na vitambaa mikononi ambavyo walikua wakivipeperusha muda wote.

Hata hivyo serikali haijazungumza zaidi kuhusiana na hilo hivyo haijajulikana kama ruhusa hiyo imetolewa moja kwa moja ama itakua ruhusa maalumu kwa ajili ya michuano ya Kombe la Dunia.