Ulemavu wa miguu pinde unatibika

Muktasari:

  • Mwanzilishi wa tiba ya Miguu Pinde duniani ni Dk Ignancio Ponseti, mhispania aliyekuwa akifanya kazi kwenye Chuo Kikuu cha Iowa nchini Marekani. Tabibu huyu alizaliwa Juni 3, 1914 na kufariki 18 Oktoba mwaka 2009. Ili kumkumbuka, wadau waliamua kuifanya siku yake ya kuzaliwa kuwa siku ya kuadhimisha siku hiyo ya Miguu Pinde.

Dunia huadhimisha Siku ya Miguu Pinde Juni 3 kila mwaka. Ni siku iliyotengwa maalumu kwa ajili ya kutoa uelewa kuhusiana na changamoto hiyo. Kila jamii hupanga ni jinsi gani itaadhimisha siku hiyo muhimu.

Mwanzilishi wa tiba ya Miguu Pinde duniani ni Dk Ignancio Ponseti, mhispania aliyekuwa akifanya kazi kwenye Chuo Kikuu cha Iowa nchini Marekani. Tabibu huyu alizaliwa Juni 3, 1914 na kufariki 18 Oktoba mwaka 2009. Ili kumkumbuka, wadau waliamua kuifanya siku yake ya kuzaliwa kuwa siku ya kuadhimisha siku hiyo ya Miguu Pinde.

Mapema mwaka huu Hospitali ya CCBRT kwa kushirikiana na Kampuni ya simu za mkononi ya Tigo, iliwaleta pamoja wadau mbalimbali nchini na kuzungumza nao, lengo hasa ni kuwafanya wawe mabalozi wa kusambaza elimu kwa umma juu ya tatizo hilo.

Kaimu Mkurugenzi wa CCBRT, Haika Mawala analielezea tatizo hilo kuwa ni la kuzaliwa, na halitokani na kitu chochote, hivyo Watanzania wasiogope kufika hospitali kupata matibabu.

“Si hivyo tu, tatizo hili linatibika hivyo ni vyema mzazi atakayemgundua mtoto wake kuwa nalo, amlete hapa kwetu mara moja kwa ajili ya kupata matibabu,” anasema.

Mawala anaeleza kuwa kila mwaka watoto 2,200 huzaliwa wakiwa na tatizo la miguu pinde, asilimia 50 ya watoto hao huwa wameathirika miguu yote miwili. Idadi ya watoto wa kiume wanaopatwa na tatizo hili ni kubwa kuliko ya wa kike akisema kuwa uwiano wao ni 5:2.

Ikiwa tatizo hili litawahishwa mapema, matibabu hufanyika na mtoto hupona kabisa, ila ikiwa mzazi atamchelewesha mwanae, kuna athari kadhaa zinazoweza kumpata.

Miongoni mwa athari hizo ni pamoja kumfanya mtoto ashindwe kutembea vizuri jambo litakalokuwa na madhara kadri anavyokua. “Wapo watoto wengi waliokataa kwenda shule kwa kujiona kama wana utofauti na wenzao. Kuna watu wazima wanaoshindwa kufanya kazi zao kutokana na ulemavu uliosababishwa na tatizo hili, ” anasema na kuongeza: “Ningependa kuwahakikishia Watanzania kuwa tatizo hili linatibika, halina hata chembe ya ushirikina kama wengi wanavyodhani.”

CCBRT na matibabu ya Miguu Pinde

Matibabu ya kawaida ya tatizo hili katika hospitali ya CCBRT yalianza mwaka 2001 ingawa hayakutumia njia ya Ponseti ambayo ilianza kutumika mwaka 2008.

“Tangu kuanza kwa matibabu hayo, maelfu ya watoto wametibiwa hospitalini hapo na kupona, licha ya kuwapo changamoto kadhaa katika ukamilishaji wa hatua za matibabu.

Katika kipindi cha mwaka 2015, watoto 1,024 walio chini ya miaka mitano walipata matibabu hayo bure na kurudi katika hali yao ya kawaida,” anasema Mawala

Pamoja na kutoa matibabu katika Hospitali yao iliyopo jijini Dar es Salaam, Mawala anasema timu yake imekuwa ikitoa matibabu na mafunzo katika mikoa mbalimbali nchini.

“Kwa kipindi cha mwaka 2015, tulitoa matibabu kwa zaidi ya watoto 605 kutoka mikoa mbalimbali waliokuwa wakisumbuliwa na tatizo hilo,” anasema.

Bingwa wa mifupa wa CCBRT, Dk Prosper Alute anasema matibabu ya Miguu Pinde ni rahisi zaidi kwa watoto kuliko watu wazima, hivyo ni vyema wagonjwa wafikishwe mapema na ikiwezekana muda mfupi baada ya kuzaliwa.

“Ponseti ina hatua kama tano hivi ambazo mgonjwa huzipitia kabla ya kukamilisha matibabu yake. Kikubwa ni kuhakikisha mzazi anafutatilia hatua hizo kama tunavyomwagiza,” anasisitiza.

Meneja wa Huduma za Jamii kutoka Tigo, Woinde Shisael anasema kampuni yake iliingia mkataba wa miaka mitano na CCBRT ili kutoa matibabu hayo bure kwa watoto.

“Baada ya kugundua kuwa watu wengi hawawezi kumudu gharama za matibabu kwa watoto wao, tuliona ni vyema tukaisaidia hospitali ya CCBRT kutoa matibabu bure kwa watoto hao,” anasema Woinde.

Mwaka 2015, Tigo ilisaini mkataba wenye thamani ya Sh330 milioni kulipia matibabu ya watoto wenye Miguu Pinde.

Wakizungumza wakati wa kuwatembelea wagonjwa, wasanii wa kizazi kipya; Ben Pol na Chege Chigunda wanasema watatumia umaarufu wao kuwahamasisha wazazi kuwapeleka watoto wenye changamoto hiyo kutibiwa.

“Sikuwahi kufahamu kanma huu ni ugonjwa na unatibika, lakini leo nimeona na ninaahidi kuwaelewesha mashabiki wangu ili wayajue maradhi haya,” anasema msanii Ben Pol.

Miguu Pinde inatibika

Shamim Rajab (23), ni mama mwenye mtoto wa miezi miwili. Ni miongoni mwa maelfu ya wazaziwenye watoto waliozaliwa na tatizo la Miguu Pinde.

Anasema aligundua tatizo la mwanawe baada ya kujifungua: “Kiukweli nilikosa raha na sikujua cha kufanya hadi pale dada yangu alipokuja na kunipa moyo kuwa Miguu Pinde siyo kitu kipya duniani. Ni tatizo linalowapata watoto wengi tu, na pia si ugonjwa wa kudumu kwani unatibika,” anasema. Anasema ni dada yake aliyempeleka CCBRT kuanza matibabu ambako alipata ushauri wa daktari na kwa sasa mwanaye amekamilisha hatua ya kwanza ya matibabu yake.

Agatha Chape, muuguzi na mkunga ambaye pia anahudumu katika wodi ya mifupa ya CCBRT.

Ni miongoni wa wauguzi walio katika timu inayohudumia watoto wenye Miguu Pinde.

Anasema kuwa licha ya kufanikiwa kuwapatia matibabu watoto kadha, bado kuna changamoto.

“Unajua tatizo la Miguu Pinde hutokana na kupinda kwa mifupa hususan ya miguu. Hivyo, matibabu yake huhusisha kuinyoosha miguu hiyo kwa kutumia POP na kabla ya kuvalishwa viatu, ” anasema.

Anaongeza, “Kwa kifupi ni matibabu yanayohitaji ufuatiliaji wa karibu zaidi.”

Anasema mzazi hutakiwa kumaliza hatua zote ili kupata matokeo sahihi, ila changamoto iliyopo ni wengi huwa hawazimalizi na matokeo yake kuwafanya watoto kuwa walemavu.

“Ningependa kuwaambia Watanzania kuwa miguu pinde inatibika, wasisite kuwaleta watoto kwenye matibabu, ” anasisitiza.