Upasuaji ubongo hospitali ya moi ulivyookoa maisha ya Lulu

Muktasari:

  • Tabasamu la mama huyo liliondoka usoni kila alipomuona mwanaye akishindwa kunyonya, kumeza, kupaliwa na kukohoa kutokana na maambukizi ya kifua ya mara kwa mara kutokana tatizo la ubongo.

Magreth Mhagama (sio jina halisi) alikata tamaa kama kuna wakati mwanae Lulu aliyezaliwa akiwa na ubongo kwenye mfuko mkubwa nje ya kichwa kitaalamu ‘Occipital Encephacele’, atapona.

Tabasamu la mama huyo liliondoka usoni kila alipomuona mwanaye akishindwa kunyonya, kumeza, kupaliwa na kukohoa kutokana na maambukizi ya kifua ya mara kwa mara kutokana tatizo la ubongo.

Hata hivyo, saa nne za upasuaji mkubwa uliofanywa na jopo la Madaktari Bingwa wa Taasisi ya Mifupa, Upasuaji wa Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Fahamu (MOI), zilirejesha upya tabasamu mama Lulu.

Uvimbe mkubwa uliohifadhi ubongo wake ulikuwa mkubwa mithili ya kichwa kingine.

“Sikuamini kama mwanangu atapona, nilikata tamaa. Nyumbani walinishauri niombe kurudi twende kwa waganga wa kienyeji wakiamini mtoto amechezewa kishirikina. Nawashukuru sana madaktari na manesi kwa kumsaidia mtoto wangu,” anasema mama huyo huku macho yake yakilenga machozi.

Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo na Uti wa Mgongo wa Moi, Nicephorus Rutabasibwa anasema haikuwa rahisi.

Anasema upasuaji wa ubongo unahitaji vifaa vya kisasa na umakini mkubwa kutokana na ukweli, hicho ni kiungo cha aina yake katika mwili wa binadamu.

Ubongo hutoa kila fikra, tendo, kumbukumbu, hisia na uzoefu wa kidunia.

Ubongo unapokuwa na hitilafu huathiri mfumo mzima wa fahamu wa mwanadamu.

Kwa mujibu wa jarida la New Scientist, Ubongo wa binadamu umetengenezwa na viungo laini vilivyo katika mfumo kama mafuta mazito yaliyoganda.

Dk Rutabasibwa anasema upasuaji huo wa kwanza kuwahi kufanyika nchini, uliwezekana kutokana na umakini mkubwa wa wataalamu sambamba na uwapo wa vifaa vya kisasa.

Mimba ilionekana kama mapacha walioungana

Mama wa mtoto anasema wakati wa ujauzito wake, alionekana kama ana watoto mapacha walioungana.

“Kwa hiyo nilijua ninamapacha kwa sababu, kulionekana vichwa viwili. Hivyo niliilea mimba yangu nikitegemea watoto wawili,”anasema.

Anasema alipopata uchungu, alienda kujifungua katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro lakini kutokana na mkao wa mtoto tumboni alilazimika kufanyiwa upasuaji.

“Nilipojifungua nikaona mtoto anavichwa viwili, basi nilimpokea kwa sababu siwezi kumtupa wala kumnyanyapaa mwanangu. Nilianza kumlea kwa upendo tu,”anasema.

Siku nane baadae, mama huyo alipewa rufaa hadi Moi ambapo alipokelewa na madaktari bingwa.

“Nilipokelewa vizuri nikalazwa. Daktari akawa anakuja anamuangalia mtoto wanampima anaondoka. Aliniambia atapona tu lakini nilikuwa siamini,” anasema.

Mtoto afanyiwa utafiti

Wakati mama huyo amelazwa Moi, madaktari hao bingwa walikuwa wanafanya uchunguzi.

Dk Rutabasibwa anasema walitumia muda wa miezi miwili kufanya utafiti huo kuona namna ya kumfanyia upasuaji makini, utakaookoa uhai wa mtoto.

“Tathmini ya uchunguzi ilionyesha uvimbe au mfuko huo ulikuwa umefunika sehemyu kubwa ya ubongo na mishipa ya damu inayolisha ubongo, hivyo kuhatarisha maisha yake. Upasuaji ulihitaji umakini wa hali ya juu na vifaa vya kisasa,” anasema.

Mtoto hakuwa na uwezo wa kunyonya wala kumeza hali ilimfanya awe anapaliwa mara kwa mara na kupata maambukizi ya kifua (Aspiration Pneumonia).

Daktari huyo bingwa aliyeongoza jopo la madaktari wenzake anasema Lulu hakuwa na uwezo wa kulala vizuri hali ilimpa wakati mgumu mama yake.

Mama Lulu anasema hakuwa na uwezo wa kumbeba kwa sababu ya uvimbe mkubwa kuning’inia na kumfanya mtoto aonekane na vichwa viwili.

Siku ya upasuaji

Mama Lulu anasema siku moja kabla alipatiwa taarifa za mwanaye kufanyiwa upasuaji.

“Nilifurahi kwa sababu wenzangu wote watoto wao walikuwa wanafanyiwa ila mimi. Basi nilijiandaa kama nilivyoelekezwa ikiwamo, muda wa mwisho kumnyonyesha,” anasema.

Anasema siku hiyo aliamka mapema, akamuandaa mwanawe japo wakati wote hakuwa anaamini kama kweli atapona.

“Sikuwa na imani kabisa, nilimpeleka mtoto kwenye chumba cha upasuaji wakanipokea. Walinituma dawa nikaenda kununua, nikawaletea. Nikawa nakaa tu pale sielewi chochote,” anasema mama huyo.

Anasema alikaa tangu asubuhi hadi saa saba mchana bila kujua kinachoendelea japo wakati wote aliambiwa ni salama.

“Basi mara nikaambiwa niende ICU nikamuone mtoto, nikaenda nikaona ameondolewa uvimbe. Nilifurahi sana,” anasimulia.

Hali ilivyokuwa ndani ya chumba cha upasuaji

Rutabasibwa anasema changamoto kubwa waliyokumbana nayo wakati wa maandalizi ya upasuaji ilikuwa ni upatikanaji wa mishipa ya damu ya mtoto kwa kuwa ilikuwa midogo.

“Madaktari bingwa wa usingizi walipata changamoto kubwa ya kumpatia dawa ya usingizi mtoto Lulu kutokana na shingo yake kuwa fupi na maumbile ya shingo hiyo kuwa madogo,” anasema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Moi, Dk Respicious Boniface anasema upasuaji uliotumia saa nne ni upasuaji mkubwa.

Kama ungefanywa nje ungeweza kugharimu kati ya Sh25 hadi 30 milioni.

“upasuaji wa saa nne ni mkubwa, kama ungefanyika nje ya nchi pamoja na gharama zake zote za matibabu, ungegharimu fedha nyingi,” anasema Dk Boniface.

Anasema upasuaji huo umewezekana kutokana na umahiri wa madaktari wazalendo, chumba cha upasuaji chenye vifaa vya kisasa na huduma bora ya matibabu ikihusisha chumba cha uangalizi maalumu (ICU).

Anasema mkakati walionao ni kuhakikisha kesi zote kubwa zilizokuwa zinapelekwa nje, zinafanyia matibabu ndani ya nchi kwa sababu tayari wapo madaktari bingwa wanaoweza kufanya hivyo.

Hata hivyo, anasema kwa sasa wapo kwenye maandalizi ya mwisho ya kutowasafirisha wagonjwa nje ya nchi, kutokana na kuwa na madaktari bingwa wa kutosha.

“Huu ni upasuaji mkubwa wa aina hii wa kwanza, tunao madaktari bingwa hapa kwetu na tuwahakikishie Watanzania kwamba safari za nje kwa ajili ya matibabu hazitakuwapo,”anaeleza.

Simulizi ya imani za kishirikina

Mama Lulu alipoambiwa huenda mwanawe amerogwa alianza kuamini.

Alipoambiwa aombe ruhusa kurejea kwao Morogoro, alitaka kufanya hivyo lakini alishauriwa asubiri matibabu.

“Nilipigiwa simu nikaambiwa kuna wenzangu wananizunguka, yaani wananichezea kishirikina wakasema niombe nirudi nyumbani,” anasema na kuongeza;

“Nilipomuuliza mwenzangu, aliniambia hayo ni mambo ya Mungu kwa hiyo tuvumilie matibabu. Hata hivyo, Daktari alikuwa ananipa moyo siku zote, nilidhani ananizungusha kumbe alikuwa akimchunguza mtoto,” anasema mama huyo.

Anasema kupona kwa mtoto wake ni kielelezo kwamba badala ya kutegemea waganga wa kienyeji na imani za kishirikina, huduma za afya zinatosha.

Ushauri wa Daktari

Dk Boniface anasema ni wakati wa jamii kubadili mtizamo wake kwa kuwapeleka watoto hospitali ili wahudumiwe kitaalamu.

“Waandishi wa habari iambieni jamii ni vizuri kutegemea utaalamu wa madaktari kuliko kuwapeleka watoto kwa waganga. Mtoto akiwa na tatizo, inabidi aletwe hspitali,” anasema.