Wasichana wachangamkia kununua kondomu madukani

Muktasari:

  • Zamani wengi waliona aibu kunua zana hiyo hasa wanawake. Lakini kazi ya maambukizi ya ukimwi iliwafanya wengi kuwa makini katika matumizi ya kondomu japo wapo wanaopuuzia bado.

Mbali na kumkinga mtumiaji na mimba zisizotarajiwa faida nyingine kubwa ya kondom ni kutopata maambukizi mapya ya virusi vya ugonjwa wa Ukimwi (VVU).

Zamani wengi waliona aibu kunua zana hiyo hasa wanawake. Lakini kazi ya maambukizi ya ukimwi iliwafanya wengi kuwa makini katika matumizi ya kondomu japo wapo wanaopuuzia bado.

Tanzania ni kati ya nchi zilizojitahidi kupambana na maambukizi hayo kwa kuwa na mikakati mbalimbali, moja wapo ikiwa ni kuihamasisha jamii ijikite katika matumizi ya kondom (mipira ya kike na kiume).

Takwimu za maambukizi ya VVU zilizotolewa mwaka jana kupitia utafiti wa Viashiria na Matokeo ya Ukimwi Tanzania zinaonyesha kiwango kimepungua kutoka asilimia 5.4 mwaka 2011/2012 hadi asilimia 4.7 mwaka 2016/2017.

Wauzaji wa kondom katika maduka ya dawa wanaizungumziaje biashara ya bidhaa hiyo

Wauzaji wa maduka ya dawa wanasema idadi ya wanawake wanaofika kununua kondom inaongezeka siku hadi siku. Mfanyabiashara wa duka la dawa katika eneo la Mabibo jijini Dar es Salaam, Mshino Nelson anasema wateja wake wengi ni wanawake wenye miaka kati ya 20 hadi 40.

“Kati ya wateja wangu watano wanaonunua kila siku, wawili ni wanawake na wao hununua bila woga na hawaoni aibu kabisa,” anasema.

Mfanyabiashara mwingine wa duka la dawa aliyepo Kariakoo, Anitha Neto anasema sio kama zamani, matumizi ya kondom kwa jamii limekuwa jambo la kawaida kwao.

Anasema wasichana na wanawake wengi wanaofika dukani hapo na kununua zana hiyo wanasema licha ya kuwapunguzia hatari ya kupata maambukizi ya VVU, lakini pia huwasaidia kujikinga na mimba zisizotarajiwa. “Nina mteja mmoja mwanamke, yeye huwa anaamua kuchukua paketi 10 kabisa na ananiambia hatapenda usumbufu wa kurejea mara kwa mara dukani,” anasema Anitha.

Anasema kwa wanaume, vijana na watu wazima wote hununua zana hiyo kwa kujificha ficha tofauti na wanawake na wasichana ambao hujiachia hata wakikuta kuna wateja wengine.

“Lakini kule kujitokeza kununua, hapa kwetu naweza kusema idadi inaweza kulingana yaani wanaume watu wazima kabisa, vijana na wasichana na wanawake idadi yao haipishani, sema tu wanaume hujisikia aibu kidogo,” anasema.

Matumizi ya kondomu za kike yakoje

Anitha anasema wanawake wengi hawapendi kutumia kondom za kike na nyingi haziuziki isipokuwa za kiume.

Alipoulizwa ni kwanini wateja wake hawapendi kununua kondomu za kike, Anitha alisema “Wanawake wengi wanasema ni bora wawahimize wanaume wanaokutana nao kuzivaa badala ya wao kuvaa za kike kwa sababu zinakero, ukiwaliza kero gani? Wanasema kwani wewe hujui.”

Watumiaji nao walonga

“Siku ya kwanza nilipofika dukani nilisubiri watu watoke kisha nikavuta pumzi nikijifanya kutafuta dawa baadaye nikamwambia muuzaji, nahitaji kondom” anasema Mercy Chuli (sio jina halisi).

Nia ya Mercy anasema hununua kondom ili kujikinga zaidi na mimba na siyo VVU, kwa madai kuwa anao uhakika kwamba mpenzi wake yupo salama.

“Pamoja na kununua kondom yangu, bado uamuzi wa mwisho upo kwa mwanaume mwenyewe kwamba atumie au asitumie. Lakini bora uwe nayo kwanza, sasa usiulize alikubali au alikataa kuitumia, hiyo ni hoja nyingine” anasema Mercy huku akicheka na kuondoka kwenye eneo tulilokuwa tunaongea.

Mtumiaji mwingine wa zana hiyo anasema amani huwa inamuishia kama hatatumia kondom hasa anapokutana na mpenzi mpya, ambaye hawajawahi kupima afya.

“Kwa sababu ya kukosa amani, ilibidi nipate ujasiri wa kuingia dukani na kununua kondom. Huwa sijali kama kuna watu au hakuna lakini huwa siingii duka moja kila wakati, na huwa naenda maduka ya mbali na eneo ninalofahamika,” anasema.

Jonas George anasema isingekuwa matumizi ya kondom huenda angekuwa ameshaambukizwa VVU.

“Tangu nianze kutumia kondom nimeshafanya mapenzi na wanawake wengi wanafikia hata 50, ninajiamini kwa sababu nina uwezo mkubwa wa kutumia zana hiyo” anasema.

Kijana huyo mwenye miaka 35, anasema matumizi ya kondom yamemuondolea kesi za kuwa na watoto wengi na uhakika wa afya yake.

Anasema mara nyingi hupendelea kondom zenye harufu ya matunda hasa ndizi, japo sio mara zote humudu kuzipata.

“Sina mtoto wa nje na hakuna anayeweza kuniambia amepata mimba kwa sababu bila kondom huwa sithubutu kufanya chochote,” anasema.

Anasema zamani alikuwa anapata zana hiyo bure katika nyumba za wageni lakini hivi sasa hulazimika kununua.

“Siku hizi zimeadimika, zinauzwa huwezi kupata bure kama zamani,’ anasema.

Maoni yake ni tofauti na Jumanne Idris ambaye anasema hajawahi kufurahia mapenzi bila kondom.

Ukweli kuhusu Kondomu

Tunaelezwa kuwa kondom zilitengenezwa kwa ustadi mkubwa na haziwezi kupitisha kitu chochote.

Hata hivyo, tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa kondom sio salama kwa asilimia 100 kwa sababu zinaweza kuvuja kutokana na mazingira halisi au zikikaa muda mrefu.

Wataalamu hao kwenye tafiti zao wanabainisha kuwa kondom haziwezi kupitisha mbegu za kiume.

Daktari kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi Shirikishi, Kituo cha Tiba Muhimbili, Tawi la Mloganzila Shindo Lawa anasema kondom ni salama lakini sio kwa asilimia 100.

Upana wa kifurushi cha ukimbi ni makroni 0.1 wakati uana wa mbegu ya kiume ni makroni 5 kwa hiyo, mbegu ni kubwa zaidi ya kirusi.

Dk Kilawa anasema kondom kutokuwa salama husababishwa na mambo kadhaa ikiwamo watumiaji kutokujua matumizi sahihi, kutengenezwa kwa kiwango cha chini na wakati mwingine inaweza kupasuka wakati wa matumizi.

“Kondom inavaliwa kuishia kwenye shina la uume kwa mwanaume na hata ile ya mwanamke haizui maji maji ya mwanamke kugusana na sehemu nyingine kama zinazokaribia na mazingia ya uke na uume hivyo, maji maji yale kama yana wadudu yanaweza kumgusa mwingine na kama anamichubuko ni rahisi kumwambukiza,” anasema Kilawa.

Anasema kihalisia, kuna baadhi ya wanaume hujikuta hawatumii kondom hata kama wapo nazo na hiyo ni hatari kwa maambukizi ya ukimwi na maradhi ya zinaa.

“Mwanaume anaweza kutembea na kondom kabisa na akajihakikishia kuvaa, lakini katika kupurushani za kutaka kufanya mapenzi mwanaume anajikuta kasimamisha mzuka umempanda na kujipa matumaini na kumbuka akili huwa inahama, inarudi baada ya tendo kufanyika,” anasema.

Makala hii itaendelea Ijumaa ya wiki ijayo, usikose nakala yako ya Mwananchi