Sido kuanza ujenzi wa viwanda vya mfano Dodoma

Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage 

Muktasari:

Makabidhiano hayo yalifanyika jana mbele ya viongozi wa Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido).

Dodoma. Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage amekabidhi eneo la eka 13 kwa mkandarasi Suma JKT ili kujenga mabanda ya viwanda vya mfano mkoani hapa.

Makabidhiano hayo yalifanyika jana mbele ya viongozi wa Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido).

“Lengo la Serikali ni kutengeneza ajira kwa wananchi wake na ujenzi wa mabanda ya viwanda Dodoma ni moja ya njia ya upatikanaji ajira,” alisema Mwijage.

Mwijage alisema hiyo ni fursa kwa wakazi wa Dodoma na mikoa mingine ya Kanda ya Kati kupata ujuzi wa namna ya kuongeza thamani mazao yao badala ya kuyauza kwa bei ya chini yakiwa ghafi.

“Katika kanda hii ya Kati tunaanzia Dodoma ikiwa ndiyo mji mkuu wa Tanzania, hivyo wananchi wa mkoa huu watumie fursa hii kujiunga na Sido ili wapatiwe mafunzo na mitaji kuanzisha viwanda,” alisema Mwijage.

Mbunge wa Dodoma Mjini na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Watu Wenye Ulemavu Antony Mavunde aliishukuru Serikali kupitia wizara ya viwanda kwa uamuzi wa kujenga mabanda hayo katika jimbo lake.